LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wizara ya Madini yaweka wazi Utekelezaji wa Vipaumbele vyake

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
HOTUBA YA WAZIRI WA MADINI DKT. DOTO M. BITEKO AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI WAKATI AKIFAFANUA UTEKELEZAJI WA VIPAUMBELE VYA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2022/23 TAREHE 12 JULAI, 2022 – MKOANI GEITA

NAWASALIMU KWA JINA LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA.

Ndugu Wanahabari,

Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa wingi wa Rehema zake ambazo zimetuwezesha kukutana mahali hapa tukiwa wazima na kutuwezesha kukamilisha mwaka wa Fedha 2021/22 kwa mafanikio makubwa. 


Ndugu Wanahabari,

Kwetu sisi Sekta ya Madini, Mwaka wa Fedha 2021/22 ulikuwa ni mwaka wa kazi na matokeo. Kwanza, tumeweza kukusanya Maduhuli ya Serikali ya shilingi bilioni 622.5 sawa na asilimia 96.


Mwaka 2021 sekta ya Madini iliendelea kuifungua nchi yetu kiuchumi kwa kuchangia asilimia 45.9 ya thamani ya bidhaa zote zilizouzwa nje ya nchi na kuliingizia Taifa dola za Marekani milioni 3,103.20, huku kasi ya ukuaji wa sekta mwaka 2021 ilikua na kufikia asilimia 9.6 ikilinganishwa na asilimia 6.7 mwaka 2020 na kuwa ya tatu miongoni mwa sekta nyingine kutokana na ongezeko la uwekezaji. 


Mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa uliendelea kuimarika ambapo katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2021, uliongezeka hadi kufikia wastani wa asilimia 7.3 kutoka wastani wa asilimia 6.5 katika kipindi kama hicho mwaka 2020. Pia, katika robo ya mwaka ya Julai hadi Septemba 2021 mchango wa sekta uliongezeka hadi kufikia asilimia 7.9 ikilinganishwa na mchango wa asilimia 7.3 kwa kipindi kama hicho mwaka 2020.


Ndugu Wanahabari,

Mwaka 2021/22  kwa Sekta ya Madini ulikuwa wa matokeo kwa sababu tulifanikiwa kutoa leseni za uchimbaji mkubwa kwa madini ya nikeli na dhahabu, sambamba na kusainiwa kwa mikataba ya madini ikiwemo ya kinywe (graphite), madini mazito ya mchanga wa baharini ambayo itapelekea kuanzishwa kwa migodi mikubwa na ya kati jambo ambalo litazidi kuongeza thamani ya madini yetu, kukuza ajira, kukuza uchumi wetu na kuongeza mchango wa sekta kwenye Pato la Taifa na kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025 kama ilivyoainishwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo.


Ni mwaka ambao kama Wizara na Sekta tulipata bahati ya kutembelewa na wageni kutoka nchi za Burundi, Zimbabwe, Sudani ya Kusini, Zambia na nyingine ambazo zilikuja kujifunza kwetu namna tulivyofanikiwa kuisimamia sekta hii na ikatoa manufaa makubwa ya kiuchumi kwa nchi yetu. Hii ni ishara tosha kwamba, Sekta ya Madini imeleta mapinduzi makubwa Tanzania na ya kuigwa na mataifa mengine.


Ndugu Wanahabari,

Nipende kusema, pamoja na mafanikio machache niliyoyataja tuliyoyapata Mwaka wa Fedha 2021/22, mafanikio hayo yalitokana na dhamira ya dhati ya Serikali yetu inayoongozwa na Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ambaye anataka kuona thamani halisi ya madini yetu ikichangia kwa tija kubwa kwenye maendeleo ya watu wetu na taifa letu. Na pia kupitia filamu yake ya The Royal Tour.


Aidha, mafanikio haya yametokana na kutekelezwa kikamilifu kwa vipaumbele tulivyojipangia mwaka 2021/22 ya kuhakikisha madini yetu yanaleta thamani halisi ya maendeleo. 


Ndugu Wanahabari

Katika Mwaka wa Fedha 2022/23, Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha bajeti ya jumla ya shilingi 83,445,260,000.00 kwa ajili ya Wizara na Taasisi zake ili kuiwezesha Wizara kutekeleza majukumu yake. Aidha, kati ya fedha hizo, shilingi 22,000,000,000.00 ni fedha za maendeleo. Shilingi 61,445,260,000 ni fedha kwa ajili ya matumizi ya kawaida, shilingi 20,209,600,000.0 ni kwa ajili ya mishahara na shilingi 40,835,660,000.00 ni matumizi mengineyo. Aidha, bajeti hii ni sawa na ongezeko la asilimia 19.95 ya bajeti iliyopitishwa Mwaka wa Fedha 2021/22.


Ndugu Wanahabari,

Utekelezaji wa bajeti hii ya Mwaka wa Fedha 2022/23, utazingatia utekelezaji wa  vipaumbele vya wizara kama tulivyopanga ambavyo vinalenga kuhakikisha rasilimali madini zinazidi kulinufaisha taifa letu kiuchumi na kimaendeleo kwa kuzingatia miongozo mbalimbali ya kitaifa ikiwemo Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2020-2025, Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22-2025/26, Sera ya Madini ya Taifa 2009, Mpango  Mkakati wa Wizara wa Mwaka 2019/20 – 2023/24 na Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2025.


Vipaumbele ambavyo wizara imepanga kutekeleza Mwaka wa Fedha 2022/23 ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli na kuongeza mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa; kuwaendeleza wachimbaji wadogo na kuwawezesha wananchi kushiriki uchumi wa madini; kuhamasisha biashara na uwekezaji katika Sekta ya Madini; kusimamia mfumo wa ukaguzi wa shughuli za migodi;


Vipaumbele vingine ni pamoja na kusimamia na kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya wizara na kuendeleza rasilimaliwatu na kuboresha mazingira ya kufanyia kazi.


Ndugu Wanahabari,

Utekelezaji wa vipaumbele hivyo utahusisha utekelezaji wa mikakati mbalimbali ikiwemo ya kuanzisha na kusimamia migodi mikubwa na ya kati ya uchimbaji madini ya dhahabu na kinywe (graphite) pamoja madini mengine na kuhakikisha migodi yote mikubwa, kati na midogo inaajiri watanzania na kununua bidhaa huduma na bidhaa kutoka hapa nchini kwa kiwango cha kuridhisha kwa kadri ya upatikanaji wake na kutoa huduma za kijamii katika maeneo husika. Manufaa ya kufungua migodi hii ni kuongezeka mchango wa sekta katika Pato la Taifa, Uongezekaji wa ajira, na manufaa yatokanayo na uwajibikaji wa kampuni za madini kwa jamii (CSR) na ushiriki wa watanzania katika uuzaji wa bidhaa na utoaji huduma katika shughuli za madini (Local Content).


Mkakati mwingine ni kukusanya jumla ya shilingi bilioni 894.3 kiasi ambayo ni ongezeko la asilimia 22.12 ikilinganishwa na shilingi bilioni 696.4 zilizopangwa kwa Mwaka wa Fedha 2021/22. Kati ya fedha zitakazokusanywa, shilingi bilioni 822.0 sawa na asilimia 91.9 zitakusanywa na kuwasilishwa hazina na shilingi bilioni 72.3, sawa na asilimia 3.1 zitakusanywa na kutumika na Taasisi zilizo chini ya Wizara. Manufaa ya hatua hii ni kuongeza mapato yasiyokuwa ya kodi na hivyo kuchangia katika mapato ya Serikali.


Pia, ili kuwaendeleza wachimbaji wadogo na kuwawezesha wananchi kushiriki katika uchumi wa Madini, wizara imepanga kuendelea kuwatengea maeneo au kuwapatia leseni kwenye maeneo ambayo yana taarifa za msingi za kijiolojia, kutoa huduma za utafiti kwa gharama nafuu; kuwaendeleza wachimbaji wadogo kuwa wa kati na hatimaye kuwa wakubwa ikiwemo kuwapa mafunzo yanayohitajika kuhusu uchimbaji, uchenjuji na biashara ya madini. Manufa  ni kuona Sekta ya Madini inakuwa kupitia wachimbaji wadogo  na wanachangia kiasi kikubwa kwenye Pato la Taifa. Mchango wa wachimbaji mdogo umeongezeka kufikia asilimia 44 Mwaka 2021/2022 ukilinganisha na asilimia  30 ya Mwaka wa Fedha 2020/2021


Aidha, kama mtakumbuka, serikali imekuwa ikisisitiza na kuweka jitihada za kuhakikisha shughuli za uongezaji thamani madini zinafanyika nchini. Katika mwaka wa fedha ujao, wizara itaendelea kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya uchenjuaji, uyeyushaji, usafishaji na utengenezaji wa bidhaa za madini; na kusimamia na kuhamasisha uwekezaji katika shughuli za uongezaji thamani madini. Manufaa kuona ni bidhaa zinazalishwa hapa nchini kwa kutumia rasimali madini inayozalishwa hapa hapa Tanzania.


Aidha, wizara katika mwaka ujao itaendelea kuhamasisha biashara na uwekezaji katika sekta ya Madini kwa kuweka mazingira yatakayohamasisha uwekezaji katika Sekta ya Madini bila kuathiri ustawi na matarajio ya nchi kutokana na uwekezaji huo.  Pia, wizara itabuni na kutekeleza mikakati ya kuthaminisha uwekezaji katika Sekta ya Madini kwa kufanya tafiti za madini ya kimkakati, madini ya viwandani ya metali; kujenga imani kwa biashara ya madini nchini kwenye uwanja wa kimataifa kwa kutekeleza wajibu wa nchi kama wanachama wa Extractive Industries Transparency Initative (EITI). TEITI ambayo inajukumu la kuhakikisha uwazi na uwajibikaji katika uvunaji wa rasilimali madini, mafuta na gesi asilia


Ndugu Wanahabari,

Napenda kuwashukuru wadau kwa kuendelea kushirikiana na wizara katika utekelezaji wa majukumu yake, rai yangu kwa wadau wa madini tuendelee kushirikiana kwa kutekeleza kikamilifu majukumu yetu kwa kufuata Sheria, Taratibu na Kanuni zilizopo.


Mwisho, napenda kuendelea kuwakumbusha wadau wote wa Sekta ya Madini kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika tarehe 23 Agosti, 2022. Kama mtakumbuka, katika Sensa itakayofanyika mwaka huu, itahusisha kipengele maalum kitachohusu masuala yanayohusu wachimbaji wadogo. Hivyo, ushiriki wetu, utaiwezesha Serikali kupanga mipango ya maendeleo kikamilifu katika sekta yetu ya Madini.


ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA NA KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA WIZARA KATIKA KUWAELIMISHA WANANCHI KUHUSU MASUALA YANAYOHUSU SEKTA HII YA MADINI.

No comments:

Powered by Blogger.