LIVE STREAM ADS

Header Ads

Waziri Mavunde ataka watanzania kupewa kipaumbele utoaji huduma migodini

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde ameitaka Tume ya Madini kuwapa kipaumbele watanzania kwenye usambazaji wa huduma na bidhaa kwenye migodi ya madini ili kujipatia kipato, kuongeza mzunguko wa fedha nchini hivyo Sekta ya Madini kuendelea kuwa na mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa.

Mhe. Waziri Mavunde ameyasema hayo mapema leo Juni 17, 2025 jijini Mwanza kwenye ufunguzi wa Jukwaa la Nne la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini linalokutanisha wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wizara ya Madini na Taasisi zake, Taasisi za Serikali, Taasisi Binafsi, Taasisi za Fedha, Kampuni za Uchimbaji wa Madini na Watoa Huduma kwenye Migodi ya Madini.

Amesema kuwa katika kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini na kuhakikisha watanzania wananufaika na rasilimali madini, Serikali imeendelea kusimamia ipasavyo Sheria ya Madini, Sura 123 Kifungu Na. 102 na Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania za Mwaka 2018 ili kuweka usimamizi thabiti katika utekelezaji wa masuala ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini nchini.

Amesisitiza kuwa lengo la uwepo wa Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini ni kuhakikisha watanzania wanashiriki ipasavyo kupitia usambazaji wa bidhaa na huduma kwenye migodi ya madini badala ya kampuni kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi.

Aidha Mhe. Mavunde ameitaka Tume ya Madini kufanya mabadiliko ya Kanuni ili kuruhusu uhaulishwaji teknolojia kwa Kampuni za Kigeni ambapo itatoa fursa kwa kampuni za kitanzania kushirikiana na kampuni za kigeni kwenye utoaji wa huduma migodini na kujifunza teknolojia mpya kutoka kampuni za kigeni.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mavunde amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake makubwa ya kuendeleza Sekta ya Madini hali iliyopelekea mabadiliko makubwa ambapo mpaka sasa mafanikio makubwa yamepatikana.

“Mpaka sasa mafanikio makubwa yamepatikana hasa kwa wachimbaji wadogo ambapo wameanza kukopesheka kutoka kwenye Taasisi za Fedha, ushiriki wa watanzania kwenye shughuli za uchimbaji, uchenjuaji, biashara ya madini na utoaji wa bidhaa na huduma kwenye migodi ya madini umeongezeka na mchango wa wachimbaji wadogo kwenye makusanyo ya maduhuli umeendelea kuimarika,” amesisitiza Mhe. Mavunde.

Akielezea mafanikio ya utekelezaji wa kanuni za ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini, Waziri Mavunde amesema katika kipindi cha mwaka 2023/2024 jumla ya ajira rasmi 19,874 zilizalishwa katika migodi ya madini ambapo ajira 19,371 sawa na asilimia 97 zilitolewa kwa Watanzania na ajira 503 sawa na asilimia 3 zilitolewa kwa wageni.

Aidha, amewataka watanzania kuchangamkia fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini hasa kwenye usambazaji wa bidhaa na huduma kwenye migodi ya madini kama vile usambazaji wa vifaa, vyakula na huduma na kuzitaka Taasisi za Kifedha kuendelea kuwakopesha mitaji.

Amesema kuwa kampuni za madini zinatumia kiasi cha shilingi Trilioni 5.3 kila mwaka kwa ajili ya manunuzi ya bidhaa na huduma zinazotumika migodini na kuwataka watanzania kuchangamkia fursa hizo.

Naye Mkuu wa Wilaya Ilemela, Mhe. Hassan Masala akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda amempongeza Waziri Mavunde kwa usimamizi mzuri wa Sekta ya Madini hali iliyopelekea mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na ongezeko la wawekezaji nchini.

Ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kuwekeza katika mkoa wa Mwanza hasa katika eneo la uchimbaji wa madini na utoaji wa huduma mbalimbali kwenye migodi ya madini.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo amesisitiza kuwa Wizara ya Madini itaendelea kufungamanisha Sekta ya Madini na sekta nyingine muhimu za kiuchumi ili kuongeza ushiriki wa watanzania kwenye shughuli za madini nchini.

Wakati huohuo akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dkt David Mathayo, Mbunge wa Ilemela, Dkt. Angeline Mabula amepongeza kazi kubwa inayofanywa na Waziri Mavunde hali iliyochangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa.

“Kupitia uongozi wa Mhe. Mavunde tumeshuhudia mapinduzi makubwa kwenye Sekta ya Madini ambapo Tanzania imepiga hatua kubwa ya kihistoria kwa kufikia mchango wa asilimia 10.1 katika Pato la Taifa kwa Mwaka 2024, ikiwa ni Mwaka mmoja (1) kabla ya lengo la asilimia 10 lililowekwa kwenye Sera ya Madini ya Mwaka 2009 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026),” amesisitiza Dkt. Mabula

Naye Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo amesema kuwa Tume imeanza kukusanya takwimu za bidhaa zinazoingizwa nchini ili kushauri Serikali kuhusu uanzishwaji wa viwanda vinavyotoa bidhaa husika na kuongeza mzunguko wa fedha nchini huku wananchi wakijipatia ajira.

Katika hatua nyingine, Kamishna wa Tume ya Madini ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini, Dkt. Theresia Numbi ameeleza mikakati iliyowekwa na Tume ya Madini ya kuongeza ushiriki wa watanzania katika Sekta ya Madini kuwa ni pamoja na mikutano, majukwaa na vyombo vya habari.

No comments:

Powered by Blogger.