Tume ya Madini yatakiwa kuimarisha ushirikishwaji watanzania migodini
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ameitaka Tume ya Madini kupitia upya na kuboresha Kanuni ya 8, Kanuni Ndogo ya 6 ili kuhakikisha kuwa ubia kati ya kampuni za kigeni na wazawa unaleta uhamishaji halisi wa teknolojia badala ya kusalia kuwa maigizo tu kwenye maandishi.
Akizungumza Juni 17,2025 wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Nne la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini, liliofanyika jijini Mwanza, Mavunde alisema baadhi ya kampuni za kigeni zimekuwa zikikwepa matakwa ya sheria kwa kushirikiana na kampuni zisizo na uwezo wala uhusiano na shughuli wanazozifanya.
“Hii ni kinyume na dhamira ya sheria na Kanuni ya 4(b) inayolenga kuwajengea Watanzania uwezo wa kushiriki kikamilifu katika sekta ya madini” alisema Mavunde.
Aidha, Mavunde ameeleza kuwa Sheria ya Madini, kifungu cha 100, kinazuia usafirishaji wa madini ghafi nje ya nchi, na kwamba serikali imeendelea kuhamasisha uanzishaji wa viwanda vya kuongeza thamani ya madini nchini kama njia ya kuongeza ajira na pato la taifa.
Amesema mpaka sasa kuna viwanda vinane (8) vya usafishaji wa dhahabu nchini, huku vingine tisa (9) vikiwa vinajengwa kwa ajili ya kuongeza thamani ya madini ya metali kama shaba na nikeli. Pia, miradi mikubwa inaendelea, ikiwemo ujenzi wa kiwanda cha usafishaji na kuongeza thamani ya madini chenye thamani ya dola milioni 500 wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga.
“Huu ndio mkakati wetu: kuhakikisha mchimbaji mdogo anapochimba shaba, haiuzi kama jiwe la kawaida bali kama bidhaa yenye thamani” alisema Mavunde".
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, alisema sekta ya madini ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi, ajira, uhamasishaji wa teknolojia ya ndani, ubunifu, na uongezaji wa pato la serikali.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Janet Lekashingo, alieleza kuwa shughuli za sekta hiyo si uchimbaji pekee bali ni pamoja na usimamizi endelevu na udhibiti kwa manufaa ya Watanzania na mazingira.
“Tuna wajibu wa kulinda mazingira, kushirikisha Watanzania na kuongeza thamani katika mnyororo mzima wa madini” alisema Lekashingo.
Nae Kwa upande wake Dkt. Theresia Numbi, Kamishna wa Tume ya Madini na Mwenyekiti wa Kamati ya Ushirikishwaji wa Watanzania, alifichua kuwa sekta hiyo imepiga hatua kubwa katika utoaji wa ajira. Kwa mujibu wa takwimu, idadi ya wafanyakazi katika migodi imeongezeka kutoka 6,668 mwaka 2018 hadi kufikia 19,371 mwaka 2025.
Jukwaa hilo ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha sekta ya madini inatoa mchango mkubwa katika pato la taifa na kuunganishwa na sekta nyingine za kiuchumi kwa maendeleo jumuishi ya taifa.
Na Chausiku Said, Mwanza
No comments: