LIVE STREAM ADS

Header Ads

RC Mwanza afungua Mashindano ya UMITASHUMTA 2022

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mashindano ya Umoja, Michezo na Taaluma katika Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) yamefunguliwa mkoani Mwanza yakiambatana na kauli mbiu isemayo "Takwimu Sahihi ni Msingi wa Mipango Bora ya Taifa" inayolenga kuhamasisha wananchi kujiandaa kuhesabiwa katika Sensa ya Watu na Makazi Agosti 23, 2022.

Ufunguzi wa mashindano hayo umefanyika Jumanne Julai 19, 2022 katika viwanja vya Shule ya Wasichana Nsumba jijini Mwanza.

Mratibu wa UMITASHUMTA Mkoa wa Mwanza, Joseph Mambo amesema mashindano hayo yamekuwa yakifanyika kila mwaka kwa lengo la kuibua na kuendeleza vipaji mbalimbali vya kimichezo, kisanaa, kiutamaduni pamoja na kitaaluma.

Amesema Halmashauri zote za Mkoa wa Mwanza zimewakilishwa na ushiriki wa wachezaji 120 na viongozi 18 hivyo kuwa na kikosi cha wanamichezo 138 kutoka kila Halmashauri mkoani Mwanza.

Amesema mashindano hayo yatafanyika kwa muda wa siku tano na baada ya hapo vijana watakaoteuliwa wataweka kambi kabla ya kusafiri kuelekea kwenye viwanja vya mapambano mkoani Tabora ambao ndio wenyeji wa mashindano hayo kitaifa.

"Michezo itakayochezwa na kushindaniwa kwa mwaka 2022 ni soka wavulana, soka wasichana, soka wenye mahitaji maalumu, riadha wavulana kwa wasichana, wavu (volleyball), mikono (handball), mpira wa kengele kwa wenye mahitaji maalumu, netball pamoja na sanaa. Kukamilika kwa mashindano haya watapatikana wachezaji 120, viongozi 18 watakaobeba dhamana ya Mkoa wa Mwanza kwenye mashindano ya kitaifa huko Tabora" amesema Mambo.

Ameongeza kuwa Mwanza ni Mkoa wa kihistoria kwa ushindi hivyo hawana shaka na mashindano ya kitaifa, zaidi wataendelea kuweka historia kwa vitendo kwani wamekuwa wakifanya vizuri kwa miaka mitatu mfululizo.

Kwa upande wake Afisa Elimu Mkoa wa Mwanza, Mwl. Martin Nkwabi amesema takwimu zinaonyesha kuwa mahali ambapo michezo inaendelea hususani mashuleni huchochea matokeo mazuri kitaaluma pamoja na kuwafanya wanafunzi kuwa na nidhamu nzuri kuanzia kwenye ngazi ya familia na jamii kwa ujumla.

Amesema michezo ni ajira pia inaondoa ubaguzi kwani inawakusanya watoto pamoja, inasaidia kuongeza umri wa kuishi na hivyo kupunguza vifo ambavyo vinatokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Awali akifungua mashindano hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel ametoa wito kwa wachezaji kujituma kwa viwango vya juu ili waweze kuchaguliwa kwenye mashindano ya kitaifa kwani fursa hiyo ya kuibua vipaji itawasaidia kutimiza ndoto walizonazo.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Mkuu wa Mkoa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel akizungumza kwenye ufunguzi wa mashindano hayo.
Afisa Elimu Mkoa Mwanza, Mwl. Martin Nkwabi akizungumza wakati wa ufunguzi wa mashindano ya UMITASHUMTA 2022 mkoani Mwanza.
Mratibu wa UMITASHUMTA Mkoa Mwanza, Joseph Mambo akisoma taarifa ya mashindano hayo.
Washiriki kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela wakipita wakati wa ufunguzi wa mashindano ya UMITASHUMTA 2022 mkoani Mwanza.
Washiriki kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Magu wakipita wakati wa ufunguzi wa mashindano ya UMITASHUMTA 2022 mkoani Mwanza.
Washiriki kutoka Halmashauri ya Wilaya Kwimba wakipita wakati wa ufunguzi wa mashindano ya UMITASHUMTA 2022 mkoani Mwanza.

No comments:

Powered by Blogger.