LIVE STREAM ADS

Header Ads

SINGIDA: DC Muro akoshwa na mradi wa maji Urafiki-Ikungi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Jerry Muro (katikati) akivuta pazia kuashiria uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa maji ya bomba wa Rafiki-Ikungi uliopo wilayani humo katika hafla iliyofanyika juzi. Mradi huo utahudumia Kata mbili za Unyahati na Ikungi na umejengwa kwa zaidi ya Sh. Milioni 548.7 ambazo ni sehemu ya fedha za Uviko -19.
Kaimu Meneja Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Wilaya ya Ikungi, Mhandisi Michael Ndunguru (kushoto) akitoa taarifa ya mradi huo.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Ikungi, Winfrida Funto akizungumza katika hafla hiyo.
Hafla hiyo ikiendelea.
Picha ya pamoja baada ya uwekaji wa jiwe la msingi la mradi huo.
Na Dotto Mwaibale, Ikungi
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Jerry Muro ameridhishwa na kufurahishwa na mkandarasi wa kampuni ya M/S Chakwale aliyekuwa akijenga mradi wa maji wa Urafiki-Ikungi kwamba amefanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa sana.

Kufuatia hali hiyo, ameiagiza Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kumlipa mkandarasi huyo fedha zilizobaki baada ya kukamilisha ujenzi wa mradi huo ambao umegharimu zaidi ya Sh.Milioni 548.7.

Alitoa agizo hilo wakati akiweka jiwe la msingi mradi wa maji ya bomba wa Rafiki-Ikungi utakaohudumia kata mbili za Unyahati na Ikungi ambao umejengwa kwa zaidi ya Sh. Milioni 548.7 ikiwa ni sehemu ya fedha za Uviko -19.

"Katika mradi huo hakuna hata shilingi iliyoliwa na hata ukiangalia fedha aliyolipwa mkandarasi ni kidogo ukiangalia na thamani ya kazi iliyofanyika, nitowe rai kwa RUWASA sasa tumalizane na mkandarasi, kazi yake ni njema kabisa" alisema.

Muro alisema baada ya kukamilika kwa mradi huo wananchi sasa waachane na tabia ya kunywa maji ya mabondeni na mito badala yake watumie ya bomba ambayo ni safi na salama.

Alisema serikai inatumia mamilioni ya fedha kujenga miradi hii ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.

"Tabia ya kwenda kunywa maji bondeni au mtoni kwa kisingizio mumeyazoea yana radha nzuri iishe, tunywe maji ya bomba ili afya zetu ziwe nzuri, tuachane na maji ya visima" alisema.

Muro alisema serikali inawapenda wananchi wake hivyo inataka kuhakikisha dhamira ya kumtua mama ndoo kichwani ambayo imekuwa ikisisitizwa na rais Samoa Suluhu Hassan inatimia.

Alisema kukamilika mradi huu kutafanya upatikanaji wa huduma za maji katika Wilaya ya Ikungi kufikia asilimia 57.3 na kwamba malengo ya serikali ni kuhakikisha kiwango cha upatikanaji wa maji kinafikia asilimia 60 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2022.

Alisema serikali wikayani Ikungi imeshapitisha kwenye vikao vya Kamati ya Maendeleo ya Wilaya (DCC) mpango wa uboreshaji wa usambazaji wa maji katika tarafa ya Ikungi na maeneo mengine ambapo Ikungi sasa itaanza kuhudumiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Singida (SUWASA).

Muro alisema katika utekelezaji wa mradi huu hakuna hata shilingi moja iliyoliwa na kuiagiza Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kumlipa fedha zilizobaki Mkandarasi wa Kampuni ya M/S Chakwale Company Limited ambaye amelipwa fedha za awali Sh.milioni 98.7 tu.

Aliongeza kuwa mradi huo katika awamu ya kwanza utakuwa na maeneo nane ya umma ya kuchotea maji (vilula) na pia umetengenezwa ukiwa na uwezo wa kutoa huduma ya kuwaunganisha wananchi maji majumba kutokana na miundombinu yake kupita kwenye maeneo ya makazi ya watu.

Meneja Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Singida, Lucas Said, alisema ipo miradi tisa inayotekelezwa mkoani hapa kwa fedha za Uviko-19.

Said alisema katika utekelezaji wa miradi hiyo mkoa wa Singida ulipewa kiasi cha Shilingi bilioni nne.

Kwa upande wake Kaimu Meneja Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Wilaya ya Ikungi, Mhandisi Michael Ndunguru, alisema mradi huo umelenga kuwahudumia wakazi 7500 wa eneo la makao makuu ya Wilaya ya Ikungi linalojumuisha vijiji vya Ikungi na Muungano.

Ndunguru alisema kukamilika kwa mradi huu kutasaidia kupunguza maambukizi ya magonjwa yatokanayo na ukosefu wa maji safi na salama na kusaidia wananchi kufanya shughuli za kiuchumi na hivyo kuondokana na kero ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji.

No comments:

Powered by Blogger.