LIVE STREAM ADS

Header Ads

Vijana wataja vikwazo vinavyochochea uvunjifu wa Amani na Usalama

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Imelezwa kuwa utawala bora unaozingatia sheria pamoja na uchumi imara hususani kwa vijana ni miongoni mwa mambo muhimu yanayoweza kuondoa migogoro ambayo huchochea uvunjifu wa amani na Usalama katika mataifa mbalimbali duniani.

Hayo yalibainika jijini Mwanza kwenye mkutano wa kitaifa wa siku mbili ulioanza Agosti 10, 2022 ukiwajumuisha wadau pamoja na vijana kutoka mikoa ya Mwanza, Geita, Kagera na Kigoma wanaoshiriki mradi wa kuhamasisha amani na Usalama katika nchi za Maziwa Makuu (Great Lakes Youth Network for Dialogue and Peace).

Katika mkutano huo wa kitaifa uliowakutanisha pia wadau wa amani wakiwemo viongozi wa dini, polisi, wanazuoni pamoja na mashirika ya kijamii, vijana walitakiwa kuwa chachu ya kuhamasisha amani katika jamii.

"Vijana tunapaswa kujitambua na kutokubali kutumika kwa kujiingiza kwenye makundi yanayochochea migogoro kwani ni wajibu wetu kubadili jamii kuwa mahali salama" alisema Kwaresima Manko kijana kutoka mkoani Geita.
Naye Jovin Rutawulwa kutoka mkoani Kagera alisema changamoto ya vijana kujikwamua kiuchumi ni moja ya sababu inayowashawishi kuingia kwenye vitendo vya uvunjifu wa amani.

"Kagera kuna kesi nyingi za ukatili kutokana na changamoto ya uchumi, mtu anaweza kupewa elfu 50 akaenda kumuua mwenzake, hakuna vyanzo vikubwa vya mapato, hata wanaotegemea kilimo mfano kahawa, soko limekufa na hiyo inafifisha uchumi na vijana kujiingiza kwenye vitendo vya ukatili" alisema Lutawulwa.

Kwa upande wake Vivian Kori kutoka mkoani Mwanza alisema vijana ni hazina ya kwa Taifa wakiinuliwa kiuchumi kupitia fursa mbalimbali ikiwemo mikopo inayotolewa na Halmashauri.

"Tatizo kuna vikwazo vingi kwenye mikopo, pia vijana hawana taarifa sahihi kuhusu mikopo hiyo na hata wanaofanikiwa kuipata hawasimamiwi vyema na hivyo wanashindwa kufika malengo yao. Ni wakati sasa kuwa mabalozi wazuri, tutumie mitandao ya kijamii kuelimisha wenzetu, kutangaza fursa zilizopo ikiwemo biashara zetu na hiyo itasaidia kuondokana na mkwamo wa kiuchumi" alisema Kori.

Hata hivyo Beatrice Kahoya kutoka mkoani Kigoma alisema kupitia mradi wa kuhamasisha amani katika nchi za Maziwa Makuu, tayari wameanza kuandaa vipindi vya redio kwa ajili ya kuleta mabadiliko katika jamii.
Kwa Tanzania mradi huo unasimamiwa na Shirika la Demokrasia na Utawala Bora (Actions for Democrancy and Local Governance- ADLG) la jijini Mwanza ambapo Mkurugenzi wa Shirika hilo Jimmy Luhende alisema washiriki wengine ni vijana kutoka mataifa ya Rwanda, Congo na Uganda.

"Vijana wanapata fursa ya kujadili namna ya kuimarisha amani katika mataifa yao, pia wanashiriki darasa la amani (peace class) ambalo huwakutanisha vijana kutoka Tanzania, Uganda, Rwanda na Congo. Baadae mawazo yao yatawasilishwa kwa mamlaka/ wabunge tukiamini yatasaidia kuimarisha amani katika nchi za Maziwa Makuu" alisema Luhende.
Mradi wa Mtandao wa Vijana wa Nchi za Maziwa Makuu kuhusu Amani na Usalama (Great Lakes Youth Network for Dialogue and Peace) unafadhiliwa na Umoja wa Nchi za Ulaya (European Union) pamoja na Shirika la Konrad Adenauer Stiftung (KAS) la nchini Ujerumani ambapo kwa Tanzania ulizinduliwa Juni 30, 2021 jijini Mwanza.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG


No comments:

Powered by Blogger.