LIVE STREAM ADS

Header Ads

KOTECHA achaguliwa tena nafasi ya Naibu Meya

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Diwani wa Kata ya Nyamagana jijini Mwanza, Bhiku Kotecha amechaguliwa kwa kishindo katika nafasi ya Naibu Meya ikiwa ni awamu ya pili katika uchaguzi uliofanyika Jumatatu Septemba 19, 2022.

Uchaguzi huo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji Mwanza uliambatana na Mkutano Mkuu wa mwaka kwa ajili ya Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kupokea taarifa ya utendaji na uwajibikaji wa shughuli mbalimbali kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Katika uchaguzi huo, Kotecha alishinda nafasi ya Naibu Meya kufuatia wajumbe wote 22 wa Baraza la Madiwani kumpigia kura za ndiyo. Itakumbukwa mwaka 2020/21 Kotecha alichaguliwa kushika nafasi hiyo na kisha ikaenda kwa diwani wa Kata ya Pamba, Rodrick Ngoye mwaka 2021/22 ambapo ameirejesha tena kwa mwaka huu 2022/23. Uchaguzi wa Naibu Meya hufanyika kila mwaka.

Akizungumza baada ya ushindi huo, Kotecha aliwashukuru wajumbe wa Baraza kwa kumchagua kushika nafasi hiyo.

Alisema matarajio yake ni kutekeleza ahadi na mipango ya maendeleo katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza ikiwemo kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

"Nitashirikiana na madiwani wenzangu, Mstahiki Meya na Mkurugenzi Mtendaji ili tuweze kufanikisha mahitaji ya wananchi na kutekeleza kwa vitendo Ilani ya Chama cha Mapinduzi" alisema Kotecha.

Katika hatua nyingine diwani wa Kata ya Buhongwa, Joseph Kabadi alimuomba Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Mwanza, Yahya Sekiete kufanyia matengenezo gari la kukwangua barabara (Greda) ambalo limeharibika ili lisaidie kukwangua barabara korofi katika Mitaa mbalimbali.

"Tumekuwa na changamoto kubwa katika barabara zetu za mitaa na kila tunapokaa kwenye vikao vya baraza tumekuwa tukizungumzia suala la kutengeneza Greda letu la Halmashauri, mvua zimeanza kunyesha kuna baadhi ya barabara zitashindwa kutumika hivyo namuomba sana Mkurugenzi aweze kuharakisha matengenezo ya Greda hilo" alisisitiza Kabad

Kwa upande wake diwani wa Kata ya Igoma, Mussa Ngollo alisema moja ya changamoto wanayokutana nayo ni ukosefu wa huduma ya choo katika soko la Mbao liliko katika Kata hiyo hali inayosababisha adha kwa wafanyabishara na wateja ikiwemo kujisaidia kwa majirani ambao wanaishi jirani na soko hilo.

"Soko hili linawafanya biashara wengi na wateja wanaofika kwa ajili ya kununua mbao ni wengi hivyo naiomba sana Halmashauri ya Jiji la Mwanza ijenge choo ili watu wafanye shughuli zao katika mazingira salama" aliomba Ngollo.

Akitoa majibu ya maombi hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Yahya Sekiete alisema Halmashauri inaendelea kuimarisha miundombinu na wanategemea kupata fedha kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya kuimarisha miundombinu katika masoko madogo ikiwemo soko la Mbao la Igoma.

Alisema kwa sasa wanaendelea na mradi mkubwa wa ujenzi wa soko la machinga katika Kata ya Mkuyuni eneo la mchafukuoga ambao utawafanya wafanyabishara wadogo kufanya shughuli zao kwa amani hivyo masoko ambayo bado hayajawekewa miundombinu, wananchi waendelee kuwa na subira.

Kwa upande wa Greda, Sekiete alisema tayari liko kwenye matengenezo na kwamba matarajio ni kuanza kufanya kazi kuanzia wiki ijayo katika Kata zote 18 za Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Naibu Meya wa Jiji la Mwanza, Bhiku Kotecha akizungumza baada ya kutangazwa rasmi kuwa mshindi wa nafasi hiyo.
Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, Sima Constantine Sima akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa Baraza la Madiwani uliolenga kupokea taarifa ya utendaji na uwajibikaji wa shughuli za Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Yahya Sekiete akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa Baraza la Madiwani wa kupokea taarifa ya utendaji na uwajibikaji wa shughuli za Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Diwani wa Kata ya Buhongwa, Joseph Kabadi Akichangia hoja kwenye mkutano huo.
Naibu Meya wa Jiji la Mwanza, Bhiku Kotecha (kulia) akishiriki zoezi la uchaguzi. Kushoto ni Msimamizi wa Uchaguzi, James Lin'gwa.

No comments:

Powered by Blogger.