LIVE STREAM ADS

Header Ads

UVCCM Nyamagana wamchagua Mwenyekiti mpya

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza umempitisha Mussa Abdallah Magana kuwa Mwenyekiti wa umoja huo.

Uchaguzi huo ulifanyika Ijumaa Septemba 23, 2022 kupitia Mkutano Mkuu wa UVCCM Wilaya ya Nyamagana ambapo kila baada ya miaka mitano wanafanya uchaguzi wa kuwapata viongozi wa ngazi mbalimbali.

Katibu wa UVCCM Wilaya Nyamagana ambaye pia alikuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi huo, Ramadhani Omary alisema lengo ni kuwapata viongozi bora ambao watawavusha vijana na kufanya mabadiliko makubwa katika Mkoa Mwanza kwa kuipeperusha vyema bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza kweye Mkutano huo, Katibu wa CCM, Jofrey Kavenga alisema maandalizi yalifanyika vizuri na uchaguzi ulifanyika kwa amani na utulivu.

Alisema anaamini viongozi waliochaguliwa ni bora na watapambana kumsemea vyema Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na mafanikio makubwa yanayotekelezwa na Serikali huku akiwataka kuendelea kuwa wazalendo kwa kulitumikia Taifa la Tanzania.

Akizungumza wakati wa kumtangaza mshindi, Msimamizi wa Uchaguzi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi alisema wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti walikuwa watatu idadi ya wapiga kura walikuwa 387 ambapo kura zilizopigwa ni 387, kura moja iliharibika na hivyo kura halali kuwa 386.

Alisema Sara Sanga alipata kura 29 sawa na asilimia 7.91, Boniphace Boniphace Mwenyekiti aliyemaliza muda wake alipata kura 173 sawa na asilimia 44.81 na Mussa Magana alipata kura 184 sawa na asilimia 47.66.

"Kwa mujibu wa Kanuni ya uchaguzi inasema ili kiongozi atangazwe mshindi ni lazima awe amepata nusu ya kura hivyo tulilazimika kurudia uchaguzi kwa mara ya pili, wagombea walikuwa wawili Boniphace Boniphace na Mussa Magana ambapo Mussa alipata kura 221 na Boniphace kura 155" alieleza Makilagi.

Aidha Makilagi alitumia nafasi hiyo kuwasihi vijana na viongozi kufanya kazi kwa kushirikiana ili waweze kudumisha nguvu kazi kuanzia kwenye Matawi, Kata, Wilaya, Mkoa na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Magana alisema atahakikisha anawaunganisha vijana na fursa mbalimbali ikiwemo za kiuchumi ili waweze kujikwamua kimaendeleo.

Baadhi ya wajumbe wa UVCCM walisema uchaguzi ulifanyika kwa haki na wamemchagua kiongozi ambaye wanaamini atawaongoza katika misingi bora.
Mwenyekiti UVCCM Wilaya Nyamagana, Mussa Maganga.
Katibu wa CCM Wilaya Nyamagana, Jofrey Kavenga.
Mkuu wa Wilaya Nyamagana, Amina Makilagi ambaye alikuwa Msimamizi wa Uchaguzi huo.
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa UVCCM Wilaya Nyamagana.
Na Hellen Mtereko, Mwanza

No comments:

Powered by Blogger.