LIVE STREAM ADS

Header Ads

Viongozi wa Serikali watakiwa kuwasaidia wafanyakazi wa nyumbani, kunufaika na mikopo ya Halmashauri

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Viongozi wa Serikali za Mitaa jijini Mwanza wamehimizwa kuwasaidia vijana hususani wafanyakazi wa nyumbani ili kuunda vikundi vya uzalishaji mali vitakavyowawezesha kujiimarisha kiuchumi na kuondokana na utegemezi.

Rai hiyo imetolewa Ijumaa Septemba 30, 2022 wakati wa kikao cha kutambulisha mradi wa 'kuhamasisha haki za kiuchumi na kijamii kwa wafanyakazi wa nyumbani' unaotekelezwa katika Kata za Buhongwa na Mahina jijini Mwanza.

Mradi huo unasimiwa na shirika la kutetea haki za wafanyakazi wa nyumbani WoteSawa kwa ufadhili wa shirika la 'Foundation For Civil Society' kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia mwaka huu hadi mwezi Aprili 2023.

Akizungumza wakati wa kikao hicho kilichowashirikisha wafanyakazi wa nyumbani, Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka Kata za Buhongwa na Mahina, Msimamizi wa Mradi huo kutoka shirika la WoteSawa, Esther Petro amesema;

"Malengo ya mradi huu ni pamoja na kuhamasisha vijana hasa wafanyakazi wa nyumbani kuunda vikundi vya uzalishaji mali, kunufaika na asilimia nne za mikopo inayotolewa na Halmashauri, kusaidia upatikanaji wa masoko ya bidhaa watakazozalisha na pia kushiriki kwenye vikao vya maamuzi" amesema Petro akiwahimiza viongozi walioshiriki kikao hicho kusaidia malengo hayo kutimia.

Ameongeza kuwa kupitia mradi huo, watakutana na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa Kamati ya Jamii ngazi ya Wilaya ili kufanya uchechemuzi utakaosaidia vijana wakiwemo wafanyakazi wa nyumbani kunufaika na fedha za mikopo zinazotolewa na Halmashauri na kuwatembelea waajiri 150 wa wafanyakazi wa nyumbani ili kuhamasisha kazi zenye staha, mazingira salama na kuwapa mikataba ya ajira wafanyakazi wao.

Msimamizi wa Makao na Uwezeshaji kutoka Shirika la WoteSawa, Demitila Faustine amesema tayari shirika hilo limewasaidia vijana wakiwemo wafanyakazi wa nyumbani kuunda vikundi saba vya uzalishaji mali (CBO) na kuvisajili katika ngazi ya Halmashauri ambapo kikundi kimoja tayari kimekamilisha taratibu za kunufaika na mkopo kutoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza.

Naye Afisa Miradi kutoka shirika la WoteSawa, Elisha David amesema mradi huo pia utasaidia kuboresha maisha ya wafanyakazi wa nyumbani ikiwemo kupata fursa ya kumiliki rasilimali kwani wengi wao wanatoka katika familia duni kiuchumi hatua ambayo huwalazimu kukimbilia mjini kutafuta kazi itakayowasaidia kukidhi mahitaji ya familia waliyoiacha kijijini.

"Tuwasaidie kuunda vikundi na kunufaika na mikopo ya Halmashauri, tukasaidie kutatua pia changamoto za ukatili wa kijinsia wanazokumbana nazo na tutoe elimu ya kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi yao kupitia vikao na mikutano mbalimbali" David amewahimiza Viongozi wa Serikali za Mitaa na Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka Kata za Buhongwa na Mahina.

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Buhongwa, Moshi Masinde amesema ni vyema elimu ikatolewa pia kwa wazazi, walezi na waajiri wa wafanyakazi wa nyumbani kutowazuia kujiunga na vikundi vya uzalishaji mali hatua itakayowasaidia kujitegemea kimaisha hapo baadae kwani hawataishia kufanya kazi za nyumbani maisha yao yote.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Shibayi Kata ya Buhongwa, Simon Msakaji amesema ni vyema wadau mbalimbali wakaungana na Shirika la WoteSawa kuwasaidia vijana kupata mitaji ya kuanzisha miradi ya uzalishaji mali na si kutegemea tu mikopo inayotolewa na Halmashauri ambayo inadhaniwa kuwa na masharti mengi.

Katika kikao hicho, baadhi ya wafanyakazi wa nyumbani wameeleza kupitia changamoto mbalimbali ikiwemo kuamka alfajili sana, kufanya kazi bila kupumzika, kudhurumiwa mshahara na vipigo kutoka kwa waajiri hivyo matarajio yao ni kuona mradi huo ukiwasaidia kuondokana na changamoto hizo.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Msimamizi wa Mradi wa kuhamasisha haki za kiuchumi na kijamii kwa wafanyakazi wa nyumbani kutoka shirika la WoteSawa, Esther Petro akitoa ufafanuzi kuhusiana na mradi huo.
Viongozi wa Serikali za Mitaa na Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka Kata za Mahina na Buhongwa wakifuatilia kikao hicho.
Msimamizi wa Makao na Uwezeshaji kutoka Shirika la WoteSawa, Demitila Faustine akizungumza kwenye kikao hicho.
Msimamizi wa Makao na Uwezeshaji kutoka Shirika la WoteSawa, Demitila Faustine akiwa pamoja na washiriki wa kikao hicho wakati wa majadiliano ya kuweka mikakati ya kusaidia kuwatambua vijana wakiwemo wafanyakazi wa nyumbani ili kujiunga na vikundi vya uzalishaji mali.
Afisa Miradi kutoka shirika la WoteSawa, Elisha David akizungumza wakati wa kikao hicho.
Washiriki wa kikao hicho wakimsikiliza Afisa Miradi kutoka shirika la WoteSawa, Elisha David.
Neema Rodvick ambaye ni mmoja wa wafanyakazi wa nyumbani aliyeshiriki kwenye kikao hicho.
Neema Mussa ambaye ni miongoni mwa wafanyakazi wa nyumbani akichangia mada kwenye kikao hicho kilichofanyika Buhongwa jijini Mwanza.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Shibayi Kata ya Buhongwa, Simon Msakaji akichangia hoja kwenye kikao hicho.
Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Buhongwa, Moshi Masinde akieleza taratibu za vijana kunufaika na mikopo ya Halmashauri amesema ni pamoja na kuunda kikundi, kukisajili, kuandaa andiko mradi na kufungua akaunti ya benki.
Washiriki wakiwa kwenye majadiliano.
Majadiliano yakiendelea.
SOMA PIA>>> Habari zaidi hapa

No comments:

Powered by Blogger.