LIVE STREAM ADS

Header Ads

TIRA yawanoa wadau wa Bima Kanda ya Ziwa

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imeandaa mkutano wa wadau wa bima Kanda ya Ziwa ili kuwajengea uelewa kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi. 

Akifungua mkutano huo Oktoba 24, 2022 jijini Mwanza, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Masoko TIRA, Abubakar Ndwata aliyemwakilisha Kamishna wa TIRA aliwahimiz wadau hao kujipanga na kukushirikiama kutoa elimu ya bima kwa wananchi kutambua umuhimu wake.

"Mkakati wetu ni kuhakikisha hadi kufikia mwaka 2025 asilimia 80 ya watanzania wawe wamepata uelewa kuhusu umuhimu wa bima na kujiunga" alisema Ndwata.

Aliwataka wadau hao ambao ni pamoja na makampuni ya bima, mawakala wa bima, jeshi la polisi na watoa huduma za usafiri kuongeza jitihada katika utoaji wa Elimu kuhusu umuhimu wa bima mbalimbali ikiwemo afya, maisha, majengo ya biashara, masoko ya umma vyombo vya usafiri na bidhaa zinazosafirishwa nje ya nchi.

"Ili kufanikisha malengo haya, nguvu ya pamoja ni muhimu sana hivyo Kanda ya Ziwa mjipange ili mpige hatua kuongeza wateja wapya, muwatumie maafisa wauza bima ili kuwafikia watu wengi zaidi ambapo pia mtakuwa mmeongeza wigo wa ajira kwa vijana" alisema na kuongeza kuwa;

"Changamoto zilizopo zilizopo tutaenda kuzijadili na kuzifanyia maboresho, tunatambua asilimia zaidi ya 80 hapa ni mawakala hivyo tunathamini mchango wenu na niyatake makampuni ya bima kulipa kamisheni za mawakala kwa wakati" alisisitiza Ndwata.

Naye Kaimu Meneja wa TIRA Kanda ya Ziwa, Richard Toyota alisema Kanda hiyo ina jumla ya watoa huduma wa bima 150 na mkakati uliopo ni kuongeza idadi yao hadi kufikia zaidi ya 200 ifikapo Disemba mwaka 2023. 

Pia Toyota aliongeza kuwa TIRA imeweka mikakati mbalimbali ikiwemo kuunda kikosi kazi chenye jukumu la kuelimisha jamii kupitia maeneo yenye mikusanyiko kama masomo na mashuleni ili kuongeza hamasa kwa wananchi kujiunga na huduma za bima hususani zisizo za lazima ikiwemo bima ya maisha ambapo utekelezaji unaanza na watoa huduma wenyewe kuhakikisha wanajiunga na bima hizo.

Toyota aliongeza kuwa TIRA Kanda ya Ziwa inaendelea na ukaguzi wa huduma mbalimbali ikiwemo vituo vya mafuta ili kuhakikisha wana bima za majanga ambapo kati ya vituo 121 vilivyokaguliwa hadi sasa, vituo 12 vimekutwa havina bima.

"Kwenye majanga vituo 10 ni vituo vingi, tutaandaa taarifa na kuipeleka EWURA kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria, sisi hatutoi adhabu, EWURA ambao ni wasimamizi watachukua hatua kulingana na sheria" alisema Toyota.

Kwa upande wake Makamu mwenyekiti Chama cha Mawakala wa Bima Kanda ya Ziwa, aliomba TIRA kuwasaidia mawakala kupata kamisheni zao kwa wakati kutoka kwa makampuni ya bima ili kurahisisha utendaji kazi wao pamoja na kushughulikia changamoto ya baadhi ya makampuni kuchelewa kulipa fidia kwa wateja waliokata bima kwa mawakala.

Katika hatua nyingine Meneja wa kampuni ya Bima Zanzibar (ZIC), Dotto Kanyoro akitoa salamu kwa niaba ya makampuni ya bima alishauri elimu ya bima kuanza kutolewa kuanzia ngazi ya Shule za Msingi na Sekondari hatua itakayorahisisha jamii kutambua umuhimu wa bima.

Mada mbalimbali zimewasilishwa kwenye mkutano huo ikiwemo umuhimu wa miongozo mipya ya bima, hali ya soko la bima Afrika Mashariki na fursa za bima katika shughuli za kiuchumi ukiwa na kaulimbiu isemayo "Huduma Bora ni Chachu ya Usatawi wa Sekta ya Bima"
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG 
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Masoko Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Abubakar Ndwata akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa Bima Kanda ya Ziwa kwa niaba ya Kamishna wa Bima Tanzania. Mkutano huo umefanyika Oktoba 24, 2022 jijini Mwanza ukiandaliwa na TIRA Kanda ya Ziwa.
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Masoko Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Abubakar Ndwata (kulia) akifungua mkutano wa wadau wa Bima Kanda ya Ziwa kwa niaba ya Kamishna wa Bima Tanzania.
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Masoko Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Abubakar Ndwata (kulia) akifungua mkutano wa wadau wa Bima Kanda ya Ziwa.
Kaimu Meneja TIRA Kanda ya Ziwa, Richard Toyota akizungumza kwenye mkutano huo na kuhimiza wadau wa bima kushirikiana ili kuhakikisha elimu ya ima inawaikia wananchi.
Wadau wa Bima Kanda ya Ziwa wakifuatilia mkutano huo wakati Kaimu Meneja wa TIRA Kanda ya Ziwa akizungumza.
Meneja wa Shirika la Bima Zanzibar (ZIC), Dotto Kanyoro akitoa salamu kwenye mkutano wa wadau wa bima Kanda ya Ziwa kwa niaba ya makampuni ya bima.
Meneja wa Shirika la Bima Zanzibar (ZIC), Dotto Kanyoro (kulia) akitoa salamu kwenye mkutano wa wadau wa bima Kanda ya Ziwa.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Nyamagana, Fredrick Mpolo akitoa salamu kwa niaba ya Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa Mwanza.
Wadau wa bima Kanda ya Ziwa wakifuatilia mkutano huo.
Wadau wakifuatilia mkutano wa bima Kanda ya Ziwa ulioandaliwa na TIRA.
Wadau mbalimbali wa bima Kanda ya Ziwa.
Viongozi wa TIRA wakiwa kwenye mkutano huo.
Mkutano wa wadau wa bima Kanda ya Ziwa.
Picha ya pamoja.

No comments:

Powered by Blogger.