Taasisi ya DSIK Tanzania yatoa mafunzo kwa vijana wajasiriamali Mwanza
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Katika kuadhimisha Wiki ya Akiba Duniani, taasisi ya DSIK Tanzania imetoa bure mafunzo ya elimu ya fedha kwa wajasiriamali vijana 50 jijini Mwanza ili kuwajengea uwezo wa kuendesha biashara zao kwa tija zaidi.
Mafunzo hayo ya siku mbili yalianza Jumatatu Oktoba 24, 2022 katika ofisi za taasisi hiyo zilizopo Bwiru jijini Mwanza ambapo pia mafunzo ya aina hiyo tayari yametolewa kwa wanachama wa vyama vya akiba na mikopo (SACCOS) zaidi ya 350 pamoja na wanafunzi zaidi ya 7,000 katika shule za msingi na sekondari katika kipindi cha mwaka 2021/22.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkufunzi wa Elimu ya Fedha taasisi ya DSIK Tanzania, Rukia Amin alisema hatua hiyo imetokana na wajasiriamali wengi hususani vijana kutokuwa na uelewa mpana kuhusu elimu ya fedha ikiwemo umuhimu wa kuweka akiba kwa manufaa ya baadae na hivyo kusababisha biashara zao kuzorota.
“Tuna imani kwamba vijana hawa watakuwa na uwezo wa kuboresha na kuendesha biashara zao pamoja kujiwekea akiba huku pia wakitunza kumbukumbu kulingana na mapato na matumizi” alisema Amin.
Nao washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Dorcas Kessy kutoka Kata ya Nyakato pamoja na Samson Majengela kutoka Kata ya Kiseke walisema awali hawakuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha wala kutambua umuhimu wa kuweka akiba hivyo elimu waliopata itawasaidia kukuza shughuli zao.
“Hata matumizi yetu ya fedha hayakuwa rafiki, tumejifunza kwamba tunaweza kutengeneza mfumo wa matumizi sahihi, kiasi gani nimepata, kiasi gani nimetumia na kiasi gani nimeweka kama akiba. Vijana tunapaswa kuwekeza tungali wadogo kwa manufaa ya baadae” alisema Mashaka Mulya kutoka Kata ya Kayenze.
Taasisi ya DSIK Tanzania inayotekeleza mradi wa elimu ya fedha jijini Mwanza kila mwaka imekuwa ikiadhimisha Wiki ya Akiba Duniani ambayo huadhimishwa katika wiki ya mwisho ya mwezi Oktoba.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Mkuu wa Idara ya Elimu ya Fedha taasisi ya DSIK Tanzania, Immaculate Mwaungulu akiwasilisha mada kwenye mafunzo hayo.
Wajasiriamali vijana jijini Mwanza wakifuatilia mafunzo ya elimu ya fedha kutoka taasisi ya DSIK Tanzania.
Mkufunzi wa Elimu ya Fedha kutoka taasisi ya DSIK Tanzania, Rukia Amin akiwasilisha mada kwenye mafunzo hayo.
Wajasirimali vijana wa kike na kiume jijini Mwanza wakifuatilia mafunzo hayo.
Wajasiriamali vijana jijini Mwanza wakifuatilia mafunzo ya elimu ya fedha yaliyoandaliwa na taasisi ya DSIK Tanzania ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Akiba Duniani.
Wajasiriamali vijana jijini Mwanza wakifuatilia mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na taasisi ya DSIK Tanzania.
Washiriki wa mafunzo hayo wakichangia mada.
Washiriki wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Mshiriki wa mafunzo hayo, Dorcas Kessy kutoka Kaya ya Nyakato akieleza umuhimu wa mafunzo hayo.
Mshiriki Samson Manjelenga kutoka Kata ya Kiseke alisema mafunzo hayo yatamsaidia kuchanganua matumizi ya fedha za biashara yake.
Mshiriki Alodia Gattege kutoka Kata ya Sangabuye alisema mafunzo hayo yatawasaidia wajasiriamali kukabiliana na changamoto ya matumizi makubwa ya fedha kuzidi mapato.
Mshiriki Mashaka Mulya kutoka Kata ya Kayenze alisema aliishukuru taasisi ya DSIK Tanzania kwa kuwapatia vijana elimu ya masuala ya fedha kwani itawasaidia kukabiliana na changamoto zilizokuwa zinawakabili ikiwemo kuandaa mfumo wa kumbukumbu katika mapato na matumizi ya biashara zao.
Tazama BMG TV hapa chini
SOMA>>> Habari zaidi hapa
No comments: