LIVE STREAM ADS

Header Ads

RC Mwanza ataka changamoto ya maji ishughulikiwe

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Mkoa Mwanza, Adam Malima ameiagiza mamlaka ya maji safi na Usafi wa Mazingira jijini Mwanza (MWAUWASA) kuhakikisha inashughulikIa changamoto ya upungufu wa maji uliopo ili kuondoa adha kwa wananchi.

Malima ametoa agizo hilo Oktoba 25, 2022 wakati akizungumza kwenye kikao cha pili cha maendeleo ya sekta ya maji mkoani Mwanza kilicholenga kujadili taarifa na mikakati ya pamoja ya kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa majisafi na salama mkoani Mwanza.

Malima alisema kikao hicho ambacho ni sehemu kushughulikia kero zilizoibuliwa na wananchi wakati wa ziara ya Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango pamoja na Makamu Mwenyekiti CCM Bara, Abdulrahman Kinana walipofanya ziara hivi karibuni mkoani Mwanza.

Alisema katika Jiji la Mwanza (Nyamagana na Ilemela) uhitaji wa maji ni lita milioni 160 kwa siku lakini maji yanayozalishwa kwa sasa katika chanzo cha Capripoint ni lita milioni 90 ambazo hata hivyo zote haziwafikii wananchi kutokana na upotevu ambao ni zaidi ya asilimia 30 ambapo ameiagiza pia MWAUWASA kushughulikia changamoto hiyo na ile ya wizi wa maji.

Pia Malima aliiagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira jijini Mwanza (MWAUWASA) kuhakikisha mradi mkubwa wa chanzo cha maji Butimba wenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 48 za maji kwa siku unakamilika kwa wakati ili kukabiliana na upungufu wa maji uliopo sasa.

"Nataka pia ufanyike utafiti wa kina ili kubaini hali ya upatikanaji wa maji ukoje ili huduma ya maji itolewe kwa usawa maana haipendezi eneo flani wanapata maji muda wote huku eneo jingine wiki mbili hakuna maji" alisisitiza Malima.

Katika hatua nyingine Malima aliiagiza MWAUWASA kushughulikia kwa haraka matengenezo ya mtambo wa kusukuma maji katika eneo la Mabatini ili kuongeza kasi ya upatikanaji wa maji hususani maeneo yenye miiniko.

Akijibu.hoja katika kikao hicho, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji MWAUWASA, Mhandisi Salim Lossindilo alisema kumekuwa na uchakavu wa pampu za kusukuma maji hali inayosababisha wananchi kukosa maji na kwamba jitihada za kuzibadili zinaendelea ambapo kiasi cha shilingi bilioni tatu zinahitajika ili kutatua changamoto hiyo.

Kikao hicho kimejumuisha taasisi za maji ambazo ni MWAUWASA, RUWASA na SEUWASA. Kando na Nyamagana na Ilemela, hali ya upatikanaji wa majisafi Kwimba ni lita milioni 12 ambapo uzalishaji ni lita nane kwa siku. Magu uhitaji ni lita milioni saba na uzalishaji ni lita milioni tano.

Misungwi uhitaji wa maji ni lita milioni tisa na uzalishaji ni lita milioni sita, Sengerema uhitaji ni lita milioni 15 na uzalishaji ni lita milioni tisa na Ukerewe uhitaji ni lita milioni nane ambapo uzalishaji ni lita milioni nne.

Katika kikao hicho, RC Malima amezitaka taasisi za sekta ya maji ikiwemo MWAUWASA na RUWASA kujitathmini na kushughulikia changamoto za maji ili kuondoa kero kwa wananchi.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Mkuu wa Mkoa Mwanza, Adam Malima akizungumza kwenye kikao cha sekta ya maji.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji MWAUWASA, Mhandisi Salim Lossindilo akijibu hoja mbalimbali kwenye kikao hicho.
Hali ya upatikanaji wa maji katika Wilaya tano mkoani Mwanza zinazohudumiwa na RUWASA.
Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mwanza.

No comments:

Powered by Blogger.