LIVE STREAM ADS

Header Ads

Benki ya NMB yakabidhi vifaa vya usafi wilayani Kongwa

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Benki ya NMB Tawi la Kongwa Mjini Dodoma limetoa vifaa vya kuhifadhia takataka kwa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kongwa , ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji na soko la Wilayani humo kwa lengo la kuunga juhudi za Serikali Katika kuweka Mazingira safi.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo kwa Mwenyekiti wa Mji wa Kongwa, Meneja wa Benki ya NMB Kongwa Bi. Beatrice John Nghwasa alisema Benki yao inatambua na kuthamini juhudi za Serikali Katika kuboresha usafi na utunzaji wa Mazingira hivyo vifaa hivyo vitakuwa chachu ya utunzaji wa Mazingira kwa kuondoa utupwaji wa taka hovyo hivyo kwani zitakuwa zinatupwa kwenye vifaa maalumu.

Alisema Kwa miaka kadhaa wamekuwa wakiadhimisha wiki la huduma kwa wateja kwa kuhalika wateja ofisini na kuzungumza nao, lakini kwa mwaka huu wameamua kufanya tofauti kidogo kwa kutoa sehemu ya fungu kununua vifaa hivyo na kuvigawa.

Alisema Benki hiyo imefikia uamuzi huo lli kuunga mkono jitihada za serikali katika utunzaji na uhifadhi wa Mazingira.

"Vifaa hivi vitatumika kuwekea taka taka na kwa kufanya hivyo na sisi kwa namna moja au nyingine tutakuwa tumeshiriki Katika kusafisha Mazingira yetu"Alisema Meneja Beatrice

Kwa upande wake Mwenyekiti wa mamlaka ya Mji wa Kongwa Ndg. Onesmo Semundi aliwashukuru Benki ya NMB kuja na kutoa vifaa hivyo.

"Tunawashukuru sana NMB kwa jambo hili ambalo mmelifanya na kwetu sisi ni jambo kubwa na la muhimu kwani ni muda mrefu tulikuwa tukitafuta namna ya kupata mapipa ya kuwekea taka hivyo kwa msaada huu kwetu ni jambo kubwa sana"Alisema Ndg. Semundi

Mbali na pongezi hizo Mwenyekiti huyo alitoa wito kwa wafanyabiashara na Wananchi kuhakikisha mapipa hayo yanatumika kwa kazi iliyokusudiwa itakuwa haina maana kama bado taka zitaendelea kuzagaa hovyo wakati Kuna vifaa vimetolewa kwa ajili ya kuwekea takataka.

Naye Mwenyekiti wa Soko la Kongwa Bi. Helena Mbogo alipongeza Benki ya NMB kwa msaada huo huku akiwahakikishia kwamba watayatunza na yatatumika kwa kazi iliyokusudiwa.

Jumla ya mapipa manne (4) ya kukusanyia takataka yametolewa na NMB na ikumbukwe kwamba Wiki la huduma kwa wateja huadhimishwa ifikapo juma la kwanza la mwezi Oktoba ya kila Mwaka.
Na Maganga Gwensaga, Dodoma
Mwenyekiti wa Mji wa Kongwa Mhe. Onesmo Semundi (kushoto aliyevaa kofia)akipokea vifaa vya kuwekea taka kutoka Banki ya NMB.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema(Mwenye suti nyeusi kushoto) akipokea kifaa cha kuwekea taka kutoka Benki ya NMB.

No comments:

Powered by Blogger.