LIVE STREAM ADS

Header Ads

Kituo Jumuishi cha Taasisi za Kisheria Mwanza kurahisisha utoaji huduma

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Viongozi mbalimbali wakiongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt.Damas Ndumbaro wakikagua jengo la ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Taasisi za Kisheria za Serikali Mkoa Mwanza katika eneo la Buswelu wilayani Ilemela.
***

Na Hellen Mtereko, Mwanza
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt.Damas Ndumbaro ameweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa jengo la Kituo Jumuishi cha Taasisi za Kisheria za Serikali mkoani Mwanza lililopo katika eneo la Buswelu wilayani Ilemela.

Akizungumza kwenye hafla hiyo ya uwekaji wa jiwe la msingi iliyofanyika Jumanne Novemba 29, 2022, Dkt.Ndumbaro amesema ujenzi wa Vituo vya aina hiyo nchini utasaidia kupunguza tabia ya watu kujichukulia Sheria kwa kufanya mambo wanavyotaka bila kufuata taratibu.

Waziri Dkt. Ndumbaro amesema kukamilika kwa mradi huo kutaboresha mazingira ya watumishi kutimiza majukumu yao na kurahisisha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.

Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Eliezer Feleshi amesema moja ya jukumu alilopewa Septemba 16, 2022 ikiwa ni siku ya tatu baada ya kuapishwa ni kuhakikisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia taasisi zake za kisheria zilizopo nchini zinatoa huduma bora kwa umma.

Amesema kwa kutambua changamoto inayozikabili taasisi za kisheria ikiwemo ya kutokuwa na miundombinu ya ofisi, Rais Samia Suluhu Hassan aliridhia wazo la kuwa na mpango wa kujenga majengo yatakayokuwa vituo jumuishi vitakavyotumiwa na taasisi za Serikali zinatoa huduma za kisheria ili kuondokana na adha ya upangaji pamoja na kuongeza ufanisi katika matumizi ya rasilimari fedha na watu.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa jengo la kituo hicho, Mkurugenzi wa Huduma za Ushauri kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Wencelaus Kizaba amesema jengo hilo litagharimu zaidi ya Sh Bilion 3.8 hadi kukamilika kwa ujenzi.

Amesema ujenzi wa jengo hilo ulianza Aprili 26, 2022 na unatarajia kukamilisha Oktoba 25, 2023 ambapo hivi sasa umefikia asilimia 35 ya ujenzi wa kazi zote za mkataba.

Kizaba amesema kuwa mradi huo umetengeneza ajira mbalimbali ikiwemo wataalamu pamoja na wafanyabiashara wadogo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima ameahidi kushirikiana na viongozi wa Wizara ya Katiba na Sheria ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt.Damas Ndumbaro (wapili kushoto) akiweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Taasisi za Kisheria za Serikali jijini Mwanza.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt.Damas Ndumbaro akizungumza kwenye hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi kwenye ujenzi wa jengo la Kituo Jumuishi cha Taasisi za Kisheria za Serikali mkoani Mwanza.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt.Eliezer Feleshi akizungumza kwenye hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi kwenye ujenzi wa jengo la Kituo Jumuishi cha Taasisi za Kisheria za Serikali.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Khatibu Kazungu.
Mkurugenzi wa huduma za ushauri kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) akitoa taarifa ya ujenzi wa jengo hilo kwenye hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima kwenye hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi kwenye Kituo Jumuishi cha Taasisi za Kisheria za Serikali mkoani Mwanza.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt.Damas Ndumbaro (wapili kushoto) akiweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa kituo Jumuishi cha Taasisi za Kisheria za Serikali mkoani Mwanza.
Viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Taasisi za Kisheria za Serikali mkoani Mwanza.
Wadau mbalimbali waliohudhuria hafla ya uwekaji wa jiwe la msingiujenzi wa Kituo Jumuishi cha Taasisi za Kisheria za Serikali mkoani Mwanza.

No comments:

Powered by Blogger.