LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wakaguzi wa migodi watakiwa kusimamia Kanuni

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adolf Ndunguru amewataka wakaguzi wa migodi na baruti nchini kuhakikisha wanasimamia kanuni na miongozo mbalimbali iliyowekwa na Serikali kwenye utendaji kazi wao ili kumaliza changamoto ya ajali kwenye shughuli za uchimbaji wa madini.
 
Ndunguru ameyasema hayo Desemba 20, 2022 mjini Morogoro  wakati akifunga mkutano wa siku mbili wa wakaguzi wa migodi na baruti nchini wenye lengo la kupeana uzoefu kwenye ukaguzi na usimamizi wa masuala ya afya, mazingira kwenye shughuli za uchimbaji wa madini kama moja ya mikakati ya kupunguza ajali na kuwa na uchimbaji endelevu usioathiri mazingira.
 
Amesema kuwa, pamoja na mikakati iliyowekwa na Serikali kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini, bado kumekuwepo na changamoto ya ajali kwenye shughuli za uchimbaji wa madini hususan maeneo yanayomilikiwa na wachimbaji wadogo wa madini na kusisitiza kuwa chanzo kikuu kikiwa ni pamoja na mashimo kubomoka, ukosefu wa oksijeni na matumizi mabaya ya baruti.
 
Katika hatua nyingine, amewataka wakaguzi wa migodi na baruti nchini kuhakikisha kuwa wanafanya kaguzi za mara kwa mara kwenye shughuli za uchimbaji wa madini pamoja na kutoa elimu.
 
“Kwa kufuata kanuni na miongozo iliyowekwa na Serikali, bado mna wajibu mkubwa wa kuhakikisha kaguzi zinafanyika mara kwa mara, hasa katika maeneo ya wachimbaji wadogo ambapo ajali nyingi hutokea, ikilinganishwa na maeneo ya wachimbaji wa kati na wakubwa,” amesema Ndunguru.
Ameongeza kuwa wachimbaji wadogo walio wengi bado wanahitaji elimu ya kutosha kuhusu njia salama za uchimbaji wa madini na matumizi sahihi ya baruti.
 
Nduguru amewataka wachimbaji wa kati na wakubwa kuhakikisha wanatenga kiasi cha fedha kwa ajili ya usimamizi na utunzaji wa mazingira pamoja na kurekebisha mazingira yaliyoharibiwa.
 
Katika hatua nyingine, amewataka wachimbaji wakubwa wa madini kuhakikisha  sambamba na kutenga fedha za kutosha, wanaweka hati fungani (rehabilitation bond) kama Sheria ya Madini inavyotaka.
Akieleza hali  ya ukaguzi kwenye shughuli za uchimbaji wa madini nchini, Ndunguru amesema kuwa katika kipindi  cha nusu ya kwanza ya  mwaka wa fedha 2022-2023 (Julai hadi Novemba) jumla ya kaguzi 177 kwenye migodi mikubwa na midogo ya madini ziliweza kufanyika na kuwezesha Sekta ya Madini kuendelea kuimarika na kuongeza mchango wake kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi
 
Wakati huohuo, Ndunguru amemtaka Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba kuleta mapendekezo ya usimamizi wa mazingira kwa wachimbaji wadogo wa madini ili kuhakikisha mazingira yanatunzwa inavyotakiwa hata baada ya kumalizika kwa shughuli za uchimbaji wa madini.

No comments:

Powered by Blogger.