LIVE STREAM ADS

Header Ads

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji yakagua Mradi wa Maji Butimba

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imeridhishwa na utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa chanzo cha maji Butimba Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza.

Ni baada ya Januari 13, 2023 Kamati hiyo ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti Almas Maige kufanya ziara ya kutembelea na kukagua mradi huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na wakazi wa Jiji la Mwanza.

Akizungumza baada ya kukagua mradi huo, Maige alisema kazi inaendelea kufanyika kwa kiwango kizuri na fedha zinatumika kama ilivyokusudiwa katika ujenzi huo huku akitoa rai kwa mkandarasi kuhakikisha mradi huo unakamilika mapema.

"Mimi na Kamati yangu tumeridhika na ujenzi wa chanzo hiki cha maji, tuna imani kitakapokamilika kitasaidia kumaliza changamoto ya maji kwa wakazi wa Mwanza" alisema Maige.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maji, Maryprisca Mahundi alisema Wizara hiyo itaendelea kusimamia vyema mradi huo ili ukamilike haraka na kuanza kuoa huduma kwa wananchi.

Alisema mradi huo utakapokamilika changamoto ya uhaba wa maji jijini Mwanza itakuwa imepata mwarobani kutokana na chanzo hicho kutoa huduma ya uhakika.

Naye Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira jijini Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele alisema kwa kushirikiana na Wizara ya Maji, mamlaka hiyo itaendelea kusimamia ujenzi wa mradi huo ambao ukikamilika utakuhudumia wakazi 450,000.

Awali akizungumza kabla ya ziara ya Kamati hiyo kuanza, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima alisema Mkoa wa Mwanza una upungufu wa maji lita milioni 70 hivyo mradi utakapokamilika utakuwa ni suluhisho la changamoto ya maji katika Jiji la Mwanza hususani maeneo ya pembezoni.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Almasi Maige (katikati) akizungumza katika ofisi za Mkuu wa Mkoa Mwanza kabla ya Kamati hiyo kutembelea mradi wa maji Butimba. Kulia ni Mkuu wa Mkoa Mwanza, Adam Malima na kushoto ni Naibu Waziri wa Maji, Maryprisca Mahundi.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kabla ya kutembelea mradi wa maji Butimba. Kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Almasi Maige.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira jijini Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele (kulia) akitoa maelezo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusiana na utekelezaji wa mradi wa maji Butimba.
Meneja Usalama wa kampuni inayojenga mradi wa maji Butimba ya SOGEA SATOM, Hamenyaimana Ndeyeza (kushoto) akieleza hatua za kiusalama wakati Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ilipotembelea mradi huo.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakiwasili katika mradi wa chanzo cha maji Butimba jijini Mwanza.
Sehemu ya mwonekano wa eneo la kutibu maji katika chanzo cha maji Butimba.

No comments:

Powered by Blogger.