LIVE STREAM ADS

Header Ads

Imani potofu zasababisha watoto kutoanza Shule Kwimba

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mkurugenzi wa Shirika la kusaidia watu wenye ulemavu (TADDI), Piason Bwenda akizungumza wakati wa utoaji msaada katika shule ya msingi Budushi wilayani Kwimba.
***

Na Tonny Alphonce, Kwimba
Imeelezwa kuwa umbali mrefu na imani potofu za kishirikina ni miongoni mwa sababu zinazosababisha watoto wenye ulemavu wa viungo na changamoto ya ngozi kushindwa kupelekwa shule kwa ajili ya kuanza elimu ya awali katika Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.

Wakizungumza wakati wa kupokea msaada kutoka Shirika la Tanzania Alliance for Disability Development Initiatives, baadhi ya wakazi wa Kata ya Mantale kutoka Vijiji vya Mwanekeyi na Mwampulu wilayani Kwimba mkoani Mwanza wamesema Shule ya Msingi Budushi yenye miundo mbinu ya watoto wenye mahitaji maalumu inapatikana umbali wa kilometa 10 na hivyo kuwawia vigumu wazazi kuwapeleka watoto wao katika Shule hiyo.
Joyce Josephat ambaye ni mzazi wa mtoto mwenye ulemavu ameitaka Serikali kuungana na wadau wa maendeleo ili kuwajengea bweni kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalumu hali ambayo itawawezesha wazazi wa watoto wenye changamoto waweze kuwapeleka shule na kupata elimu.

“Wanakijiji wengi hapa wapo mbali na shule hivyo tunapata tabu sana kuwapeleka shule hawa watoto wenye ulemavu kwa kuwa wanahitaji mtu wa kuwapeleka shule na kuwarudisha, na watoto wengine wana ulemavu wa ngozi hivyo huwezi kuwaacha peke yao waende shule maana wanawindwa hivyo vema tuwe na bweni lao” alisema Joyce.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la kusaidia watu wenye ulemavu (TADDI), Piason Bwenda amesema wameguswa kuwasaidia wakazi wa Kata ya Mantale baada ya kupata taarifa ya watoto wengi kushindwa kuripoti shuleni mwaka huu kutokana na sababu za umbali pamoja na imani potofu.

Bwenda amesema wameamua kuitembelea Shule ya msingi Budushi kwa kuwa inahudumia vijiji zaidi ya sita hivyo inauhitaji mkubwa wa vitu mbalimbali hasa upande wa watoto wenye mahitaji maalumu wanaosoma katika shule hiyo.

“Shirika letu limegushwa na kwa kuanza tumetoa misaada midogo midogo kama vile nguo, dawa za meno, sabuni, miswaki na vyakula mbalimbali lakini kwa namna tulivyoona hali ilivyo awamu ijayo itabidi tuangalie namna ya kutatua changamoto ya miundombinu” alisema Bwenda.
Naye Mkuu wa Shule ya Msingi, Budushi Mathew Magigi amesema kwa hivi sasa Shule hiyo ina watoto wenye mahitaji maalumu 53 kati hao 28 wavulana na 25 wasichana na changamoto kubwa wanazokumbananazo ni kufichwa kwa watoto wenye ulemavu wa ngozi na kuwalazimu walimu kuwafuata watoto hao majumbani kwa ajili ya kuwapatia elimu.

Akielezea juu ya mikakati ya Serikali ya kutatua changamoto ya ukosefu wa miundombinu ya kujifunzia kwa wanafunzi hao, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, Hole Mashauri amesema kwa kushirikiana na Serikali wataangalia namna ya kufanikisha ujenzi wa bweni kwa ajili ya watoto hao wenye mahitaji maalumu.

Kwa mjibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, inakadiria kuwa kuna asilimia 9.3 ya watu wenye ulemavuni kuanzia miaka saba na kuendelea ambapo kila watu 1000, watu 93 wana ulemavu, hata hivyo kuna uwezekano kuwa takwimu hizi ni kadirio la chini ukizingatia vijana wadogo na watoto wenye ulemavu wanafichwa na kutojumuishwa kwenye takwimu hizo ambapo huenda hilo likabainika wazi baada ya matokeo rasmi ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kwimba, Hole Mashauri akitoa ufafanuzi juu ya imani potofu ikiwa ni moja ya sababu za watoto wilayani Kwima kutoanza Shule wakati wa zoezi la kupokea msaada kutoka shirika la TADDI.

No comments:

Powered by Blogger.