Wazazi, walezi watakiwa kutumia Vituo vya Malezi ya Watoto
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Wazazi na walezi wamehimizwa kutumia Vituo vya kulelea watoto vilivyopo kwenye vyuo vya Maendeleo ya Wananchi katika mikoa mbalimbali hapa nchini ili kuwalea watoto katika malezi bora na salama.
Wito huo ulitolewa na Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya Sengerema mkoani Mwanza, Consolata Magaka wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wakufunzi wa Vituo vya kulelea watoto kutoka Vyuo 54 vya Maendeleo ya Wananchi.
Magaka alisema kuna faida kubwa ya watoto wenye umri wa miaka miwili hadi mitano kulelewa na walimu waliopo kwenye vituo vya kulelea watoto kuliko dada wa kazi kwa kuwa walimu hao wamepewa mafunzo maalumu ya kumlea mtoto kimwili na kiakili.
“Dada wa kazi hawezi kumlea mtoto vizuri na wengine wanawafanyia ukatili watoto kwa kuwa hawana elimu ya malezi kwa maana hiyo jamii inatakiwa sasa kutumia hivi vituo vinawasaidia watoto kukua kimwili na kiakili na vituo hivi vinamuandaa vizuri mtoto kwa masomo yake ya darasa la awali” alisema Magaka (kulia).
Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo ya siku 14 kwa wakufunzi wa vituo vya kulelea watoto, Henry Adriano kutoka Wizara ya Elimu Idara ya Ufundi alisema lengo la mafunzo hayo yamelenga kuwakumbusha walimu mbinu mbalimbali za malezi na makuzi ya mtoto ili kuendana na wakati uliopo.
“Na sisi kwa hivi sasa tunapambana na utandawazi na tunashirikiana na wadau wengine lengo likiwa bado pale pale kuhakikisha walimu wetu wanakuwa na elimu ya kutosha katika eneo hili la makuzi na tukifanikiwa hapa tutakuwa na taifa bora na wenye wasomi wa kutosha” alisema Adriano.
Kwa upande wake Beatrice Chaula ambaye ni Mkufunzi kutoka Chuo cha Maendeleo Bariadi alilishukuru shirika la Karibu Tanzania kwa kuwapatia mafunzo hayo kwa kuwa yatawasaidia kuwalea vizuri watoto walionao katika vituo vyao na kutoa wito kuendelea kutoa mafunzo ya namna kila mara ili kuendelea kuwaongezea ujuzi na kuendana na mabadiliko yanayoendelea kujitokeza katika jamii hasa upande wa malezi.
Naye Majid Mjengwa ambaye ni Mkurugenzi Shirika lisilo la kiserikali la Karibu Tanzania alisema kwa hivi sasa wamekuwa wakitoa elimu ya malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kwa Vyuo vya Serikali vya Mendeleo ya Jamii vyenye Vituo vya kulelea watoto wadogo.
Majid alisema kuna pengo linafanywa na baadhi ya walimu kwa kushindwa kumuandaa mtoto ili aweze kuanza elimu ya awali vizuri kwa kuanza kumfundisha kwa njia ya michezo na kuanza kumjengea mazingira ya kuichangamsha akili yake tayari kwa kupokea vitu vikubwa.
“Tumegundua pia kuna uhaba wa vituo vya kulelea watoto hasa maeneo ya pembezoni hivyo kuna kila haja ya kuendelea kushawishi serikali na wadau wa elimu kuwekeza kwenye vituo hivi ili wazazi waweze kuendelea na shughuli zao na mtoto pia awe salama chini ya malezi ya walimu wenye ujuzi” alisema Majid.
Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa cha Mwaka 2020 kinaeleza kuwa mwaka 2020, Serikali ilisajili vituo 134 vya kulelea watoto wadogo mchana ikilinganishwa na vituo 373 mwaka 2019 na kufanya jumla ya vituo vilivyosajiliwa kufikia 1,677. Katika kipindi hicho, jumla ya watoto 163,394 (wavulana 85,175 na wasichana 78,219) waliandikishwa ikilinganishwa na watoto 159,479 (wavulana 82,539 na wasichana 76,940) mwaka 2019, sawa na ongezeko la asilimia 2.5.
Hili ilitokana na kuongezeka kwa mwamko wa wazazi kuandikisha watoto wadogo kulelewa katika vituo. Aidha idadi ya walezi wa watoto katika vituo vya kulelea watoto wadogo mchana iliongezeka na kufikia walezi 2,878 mwaka 2020 kutoka walezi 2,563 mwaka 2019.
Na Tonny Alphonce, Mwanza
No comments: