Walimu mna nafasi kubwa ya kupambana na ushoga- RAS Singida
Na Dotto Mwaibale,Singida
KATIBU Tawala Mkoa wa Singida, Dk. Fatuma Mganga, amesema walimu wana
nafasi nzuri ya kuweza kupambana na tatizo la mapenzi ya jinsia moja (ushoga)
na usagaji mashuleni kwa kuwa wao ni walezi wa wanafunzi kuanzia ngazi ya
chekechea hadi elimu ya juu.
Akizungumza Machi 30, 2023, wakati akifungua kikao cha Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA) Mkoa wa Singida, alisema sasa hivi kumekuwa na
tatizo kubwa la ushoga hivyo inatakiwa jitihada za dhati katika kunusuru
wanafunzi wasiweze kujiingiza kwenye vitendo hivyo ambavyo ni kinyume na
utamaduni wa kitanzania.
Alisema walimu wanaweza kuzuia watoto wasijiingize katika vitendo hivyo kwa
kuwa jirani na watoto hao na kufuatilia mienendo yao kwa kushirikiana na wazazi
wao.
"Wote tuliona Dk.Harrison Mwakyembe wakati akizungumzia suala la
ushoga ambalo walengwa zaidi wanaotafutwa kujiingiza katika vitendo hivyo ni
vijana wadogo hivyo walimu chukueni hatua kuwanusuru wanafunzi na janga
hilo," alisema.
Akizungumzia taaluma alisema walimu wakiamua wanafunzi wote watafaulu na
kuondoa kabisa alama ziro na akawaomba walimu kujenga ushirikiano na wazazi na
walezi ili kujua changamoto za watoto wakiwa shuleni na nyumbani jambo litakalosaidia kuwaweka sawa.
Mganga alisema changamoto za watoto darasani haziwezi kuwa za wazazi, mila au desturi bali ni za walimu na akahoji inakuweje watoto asilimia 90 darasani
wote wapate alama F.
"Walimu wa enzi zetu wanafunzi walipokuwa wakifanya vibaya katika
mitihani yao walikuwa wakiumia sana na ninyi ebu igine hilo kwa ajili ya
kuwasaidia watoto" alisema Mganga.
Mganga aliwaomba walimu hao waende wakakomae na hawatashindwa na kupitia
wao hakuna litakaloshindikana kwani Serikali inawategemea.
Aliwataka walimu waende kutoa faraja katika familia, waende kutengeneza
wasomi, wakafanye kazi kwa uzalendo kwa kuwainua watoto hao kitaaluma na kuwa
watapata baraka kutoka kwa wazazi na Mungu.
Mganga alisema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya kujenga
miundombinu ya madarasa ili wanafunzi wapate maeneo mazuri ya kusomea ambapo kwa
Mkoa wa Singida madarasa 620 yenye thamani ya Sh.Bilioni 12.4 yamejengwa hivyo njia pekee
ya kumuheshimisha ni kufaulisha wanafunzi wote na asiwepo wa kupata daraja la
tatu wala ziro bali wapate daraja la kwanza na la pili.
Aidha, Mganga aliwataka walimu hao kuwashirikisha wazazi kukarabati samani
za shule zinazo haribika ambazo zimekuwa zikiwekwa katika moja ya madarasa yao
badala ya kusubiri Serikali ifanye kazi hiyo.
Akizungumzia suala la chakula kwa wanafunzi aliwataka walimu hao kila shule
kuwa na mashamba kwa ajili ya kulima mahindi na mazao mengine na akahimiza suala zima
la utunzaji wa mazingira ya shule kwa kupanda miti na maua na wanafunzi wawe na
vidumu vya maji kwa ajili ya kumwagilia.
"Kuanzia mwaka ujao tutaanza kufanya mashindano ya utunzaji wa
mazingira na shule itakayo shinda tutaipatia zawadi" alisema Mganga.
Mganga pia aliwataka walimu hao kwenda kuanzisha elimu ya kujitegemea
katika shule zao kwa kufuga, mbuzi, ng'ombe, kuku na kufungua miradi midogo
midogo ambayo itawapatia kipato na kuwajengea uwezo wanafunzi wa kujua mbinu za
kujitegemea kuanzia wakiwa shuleni.
Mganga aliwahimiza walimu hao kufanya kazi kwa bidii na kujituma na kuwa
adui yake mkubwa ni mtumishi yeyote ambaye atashindwa kufanya hivyo na kuwa hata mvumilia hata kidogo.
Afisa Elimu Mkoa wa Singida, DK. Elpidius Baganda alisema kazi kubwa
wanayotarajia kuifanya ni kupita mashuleni kwa siku sita kila wiki kwa ajili
ya kuangalia kama tathmini za mitihani ya kidato cha nne na tatu zilizochukuliwa.
Alisema jambo lingine watakalolitilia kipaumbele ni suala zima la
upatikanaji wa chakula mashuleni sambamba na kuangalia miradi mbalimbali ambayo
Serikali imetoa fedha nyingi kama imekamilika kwa asilimia 100.
Mwenyekiti wa TAHOSSA, Paskal Kichambati alisema changamoto zao nyingi huwa
zinatatuliwa kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa hadi taifa na kuwa TAHOSSA kazi yake
kubwa ni kuleta utulivu.
Akizungumzia suala la miradi inayofanyika mashuleni chini ya usimamizi wa
walimu hao alisema licha ya kuwa ni walimu wamekuwa wahandisi wabobezi kwa
kuweza kuisimamia na kukamilika kwa ubora na kwa kiwango cha hali ya juu na kwa
thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali.
Alisema baadhi ya walimu kwenye akaunti zao za shule wamekuwa na fedha kuanzia Sh. milioni 30 hadi 80 kwa ajili ya kumalizia miradi hiyo na wamekuwa wazalendo na waaminifu katika matumizi ya fedha hizo.
No comments: