LIVE STREAM ADS

Header Ads

Serikali kuboresha zaidi Vituo vya kunenepesha mifugo

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Serikali imesema itaongeza nguvu kwenye vituo atamizi vya kunenepesha mifugo ili viweze kuzalisha kwa tija na kuleta mabadiliko katika sekta ya mifugo.

Akizungumza Aprili 11, 2023 baada ya kutembelea mradi wa vijana wa kunenepesha ng'ombe katika kituo cha Mabuki Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesema hiyo ni hatua nzuri ambayo italifanya taifa liweze kuuza nyama na mifugo kwenye mataifa ya nje.

Amesema ni aibu kwa taifa ambalo ni la tatu barani Afrika kwa ufugaji lakini mifugo yake haina tija.

"Kuanzishwa kwa vituo hivi atamizi ni ukombozi kwa taifa, ni hatua ya kupongezwa na kusifiwa ambapo sio tu kwamba taifa litafanikiwa kuuza nyama bora na mifugo nje ya nchi lakini pia vijana wanaohitimu elimu watajipatia ajira"amesema Dkt. Mpango.

Amesema inastajabisha kuona maprofesa wanafundisha kilimo na ufagaji lakini wao hawaishi kwenye huo ufugaji hivyo kuanzishwa kwa vituo hivi inatoa picha kile kinachofundishwa vyuoni kinakuja kufanyiwa kazi kwenye jamii.

Makamu wa Rais ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuja na wazo hilo na kwamba changamoto zilizowasilishwa ikiwemo ukosefu wa umeme, mashine za kuchanganyia chakula na roli la kubebea mifugo kwenda mnadani zitafanyiwa kazi ili kuwasaidia vijana hao kufanya kazi kwenye mazingira mazuri.
"Nimeona kwa macho kazi nzuri inayofanyika hapa kwakweli nawapongeza sana hata hiyo bajeti mliyoomba hapa naweza nikaenda kwa Rais hata kwa kumpigia magoti ili aweze kutatua changamoto hizo" amesema Dk Mpango

Hata hivyo amesema vijana wanaofanya kazi hiyo ni mifano ya kuhakikisha wanabadilisha mifugo mingi iliyopo nchini ili wafugaji waanze kufuga kisasa.

Awali Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdalah Ulega amesema jumla ya vituo atamizi vinane vimeanzishwa nchini ili kuwasaidia vijana kujipatia ajira na kuongeza kipato chao.

Amesema jumla ya ng'ombe 2,150 zimenunuliwa hivyo ambapo vijana 240 wamejiajiri kwenye vituo hivyo.
Mariam John, Mwanza

No comments:

Powered by Blogger.