LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wananchi watakiwa kuripoti matukio ya ukatili wa watoto

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa ameitaka jamii kuendelea kufichua vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto vinavyofanyika majumbani.

Kamanda Mutafungwa amesema kupitia madawati ya jinsia na watoto yaliyopo kwenye vituo vya polisi,wananchi wanaweza kutoa taarifa za matukio yote ya kikatili kwa watoto na watu wengine ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Kamanda Mutafungwa ametoa kauli hiyo wakati akitoa taarifa ya mwanaume mmoja aitwaye Godbless Mushi mwenye umri wa miaka 39 mfanyabiashara wa kuuza vifaa vya magari mkazi wa shibula wilayani Ilemela mkoani Mwanza ambaye anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kujaribu kumbaka mtoto wake wa kike.

Mtoto huyo ambaye jina lake limehifadhiwa kutokana na taratibu za kimaadili,mwenye umri wa miaka mitano mwanafunzi wa chekechea.
Kamanda alieleza kuwa jeshi la polisi linaendelea kumhoji mtuhumiwa huyo ambaye alitenda kosa hilo April 02, 2023 majira ya saa nne usiku mtoto huyo akiwa amelala ndipo mwanaume huyo alipata nafasi ya kujaribu kumfanyia mtoto wake vitendo vya udhalilishaji wa kingono.

April 03, 2023 majira ya saa tatu na dakika 40 asubuhi tukio hilo la kikatili liliripotiwa kituo cha polisi Kirumba ambapo mtuhumiwa alikamatwa na kufikishwa kituo cha polisi Kirumba ambapo anaendelea kuhojiwa na mtoto huyo anaendelea kufanyiwa uchunguzi wa kitaalamu

“Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia na Watoto linaendelea kushughulikia tukio hili kwa kushirikiana na Ofisi ya Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mwanza na upelelezi utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani” ameeleza Kamanda Mutafungwa.
Akielezea matukio hayo ya ulinzi na usalama kwa watoto, Mkurugenzi wa Shirika la Uzao Wetu, Yusuph Mtobela ameiomba jamii kuwatumia wataalamu wa saikolojia pale wanapokumbwa na msongo wa mawazo ili waweze kusaidiwa kiushauri mapema kabla ya kuchanganyikiwa na kuanza kufanya vitendo vya ajabu katika jamii inayowazunguka.

Mtobela amesema kitendo cha mzazi kumdhalilisha kingono mtoto wa kuzaa mwenyewe sio cha kawaida na kiashilia tatizo la afya ya akili ambalo linawakabili watu wengi kwa hivi sasa.

Takwimu za hali ya matukio ya ukatili kwa watoto katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2021 iliyotolewa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, jumla ya matukio yaliyoripotiwa na jeshi la polisi ni 11,499 huku mkoa wa Mwanza ukitajwa kuwa miongoni mwa mikoa inayoongoza ikiwa na matukio 500 ya ukatili kwa watoto.
Na Tonny Alphonce, Mwanza

No comments:

Powered by Blogger.