LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wizara ya Madini yatakiwa kushughulikia tozo na kodi kandamizi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa akizungumza kwenye kongamano la wachimbaji wadogo wa madini jijini Mwanza.
***

Wachimbaji wadogo wa madini wameshauriwa kulitumia Kongamano la wachimbaji wadogo wa Madini kama fursa ya kujiongezea tija na kujipatia kipato cha mtu mmoja mmoja kupitia mafunzo waliyopata.

Hayo yalibainishwa Mei 09, 2023 na Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa kwenye kilele cha Wiki ya Maonesho ya Madini wakati akifungua Kongamano la Wachimbaji Wadogo wa Madini na Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA) uliofanyika katika ukumbi wa Rock City Mall Jijini Mwanza.

Aidha Majaliwa alisema kuwa sekta ya madini ni sekta tegemewa inayotarajiwa kuleta matokeo chanya katika ukuaji wa uchumi wa nchi na kwa Mtanzania mmoja mmoja, Serikali itaendelea kutekeleza adhima yake ya kusimamia na kuwaendeleza wachimbaji wadogo nchini.

"Serikali yetu inathamini sana uchimbaji mdogo kwa kuwa wachimbaji wadogo wanachangia moja kwa moja katika uchumi wetu hivyo Kongamano hili ni muhimu kwa muktadha wa maendeleo ya Sekta ambapo itawaleta karibu wadau wote wa madini na kupata fursa ya kujadiliana ili kupata majibu ya changamoto mbalimbali" alisema Majaliwa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa alilipongeza shirikiko la vyama vya wachimbaji madini Tanzania (FEMATA) kwa maandalizi ya Kongamano hilo ambapo alisema mchango wa Sekta ya Madini tangu mwaka 2015 umekuwa ukiimarika mwaka hadi mwaka kutokana na usimamizi thabiti unaotokana na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wanayoyatoa kwenye sekta hiyo.

Pamoja na mambo mengine Dkt. Kiruswa alisema lengo la Wizara la kuchangia asilimia 10 kwenye Pato la Taifa ifikapo 2025 litafikiwa na ikiwezekana litachangia zaidi ambapo Wizara kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) linaendelea kuwaunganisha wachimbaji wadogo na Taasisi za fedha.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kiruswa alifafanua kuwa mchango wa wachimbaji wadogo wa madini umezidi kuimarika kutoka asilimia mbili mwaka 2015 mpaka kufikia asilimia 40 ya makusanyo ya serikali yanayotokana na mrabaha na ada ya ukaguzi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima alisema Mkoa huo umedhamiria kuwapa leseni wachimbaji wadogo wa madini ambapo wachimbaji wadogo wanawake wamepewa kipaumbele katika kupatiwa maeneo ya uchimbaji madini.

Pia Malima alimshukuru Waziri Mkuu kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika kilele cha kongamano hilo ambapo amesema Mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa umeongezeka mpaka kufikia asilimia 9.7 ambapo Mkoa wa Mwanza ni mmoja ya wachangiaji katika ongezeko hilo na kutoa wito kwa washiriki kutembelea vivutio mbalimbali vilivyomo mkoa wa Mwanza ikiwemo visiwa vya Ukerewe na Saa Nane.

Kwa upande wa Rais wa FEMATA, John Bina alisema mchango wa masoko ya madini umeongezeka kutoka asilimia 2.2 mwaka 2019 mpaka kufikia asilimia 28 mwaka 2023.

"Hakika tunaiona nguvu ya Mama, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika kuilea Sekta ya Madini kwa sasa sekta yetu ya uchimbaji mdogo inazidi kusonga mbele japo kuna changamoto kadhaa ambazo bado tunazifanyia kazi, hakika alipo Mama, wachimbaji tupo," alisema Bina.

Aidha Bina alisema FEMATA imedhamiria kwenda pamoja na wanawake ambapo mpaka sasa takwimu zinaonesha kwamba zaidi ya wanawake 2000 wamejiunga katika shughuli za madini ikiwemo uchimbaji, uchenjuaji na uongezaji thamani madini.

Awali akitoa utambulisho wa viongozi wa Serikali, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo alisema Kongamano hilo limehudhuriwa na zaidi ya wadau wa madini 1400 ambao wameshiriki katika kutoa elimu mbalimbali kuhusiana na Sekta ya Madini.
Tito Mselem, Mwanahamisi Msangi na Godwin Masabala, Mwanza
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa akizungumza kwenye kongamano hilo.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo akizungumza kwenye kongamano hilo.
Rais wa FEMATA, John Bina akizungumza wakati wa kongamano hilo
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dkt. Venance Mwasse (kulia) akitoa ufafanuzi kwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa (kushoto) alipotembelea banda la shirika hilo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiangalia aina mbalimbali za madini yanayochimbwa na kuongezewa thamani hapa nchini wakati akikagua mabanda kwenye maonesho ya madini yanayofanyika viunga vya Rock City Mall. Kulia anayetoa ufafanuzi ni Kamishna wa Madini, Dkt. Abdulrahman Mwanga.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea zawadi ya picha wakati akikagua mabanda mbalimbali kwenye maonesho ya madini yanayofanyika katika viunga vya Rock City jijini Mwanza.
Washiriki wakiwa kwenye kongamano la wachimbaji wadogo wa madini.
Washiriki wakifuatilia kongamano hilo.
Tazama BMG TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.