LIVE STREAM ADS

Header Ads

Hospitali ya Bugando yapokea vifaa tiba kutoka shirika la Americares

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com 
Hospitali ya Rufaa Kanda Bugando jijini Mwanza imepokea vifaa tiba vya upasuaji wa ugonjwa wa fistula ya uzazi kutoka shirika la Americares, vyenye thamani ya shilingi milioni 234.2 vitakavyosaidia utoaji huduma ya matibabu ya ugonjwa huo.

Akizungumza Juni 01, 2023 kwenye hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi amesema vitasaidia kutoa huduma ya matibabu kwa akina mama wanaougua fistula ya uzazi na hivyo kuzuia vifo vitokanavyo na ugonjwa huo.

Makilagi ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa Mwanza, Amos Makalla amesema suala la kuboresha huduma za afya ni kipaumbele cha Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan lakini pia ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/25.

“Nitoe rai kwa uongozi wa Hospitali ya Bugando kuhakikisha vifaa hivi vinatunzwa vyema na kufanya kazi iliyokusudiwa ya kuokoa maisha ya mama na mtoto” amesema Makilagi.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Kanda Bugando, Dkt. Fabias Massaga amesema zaidi ya wanawake 300 wanaougua fistula kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, wamekuwa wakitibiwa katika hospitali hiyo ambapo kwa mwaka 2022 waliopata tiba walikuwa wanawake 373 na kati yao, 207 walifanyiwa upasuaji huku 166 wakipata tiba ya viungo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi Shirika la Americares, Nguke Mwakatunde amesema takribani wanawake elfu tatu huugua fistula kila mwaka hapa nchini ambapo wanaofika katika matibabu ni takribani wanawake elfu mbili huku wanawake elfu moja wakikosa huduma kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa elimu ya kufika katika vituo vya kutolea huduma za afya.

“Vifaa hivi vitasaidia kuboresha huduma za upasuaji wa fistula ya uzazi hapa Bugando, lakini pia shirika la Americares kwa kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Afya litaendelea kushiriki juhudi mbalimbali za kutokomeza fistula hadi kufikia mwaka 2030” amesema Mwakatunde huku akishauri Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kusogeza huduma za fistula karibu na wananchi hadi ngazi za hospitali za rufaa za mikoa.

Nao baadhi ya mashujaa wa fistula wanaopata matibabu katika hospitali ya Bugando akiwemo Pendo Dodo kutoka mkoani Mara na Christina kutoka mkoani Mwanza wamelishukuru shirika la Americares kwa msaada wa vifaa hivyo na kueleza kuwa vitasaidia kuboresha huduma kwa wanawake wanaougua ugonjwa huo.

Wamesema ugonjwa huo unaosababishwa na uchungungu pingamizi wakati wa kujifungua unasababisha changamoto mbalimbali kwa wanawake ikiwemo unyanyapaa na hivyo kutumia fursa hiyo kuwasihi wanajamii kuacha tabia hiyo na badala yake kuwasaidia wagonjwa kufika mapema kwenye matibabu kwani fistula inatibika.

Kwa Kanda ya Ziwa, mikoa ya Shinyanga na Geita imetajwa kuwa na wagonjwa wengi wa fistula ambapo wataalamu kutoka hospitali ya Kanda Bugando kupitia huduma ya tiba mkoba (Outrich Program) wamekuwa wakifika katika mikoa hiyo ili kuwajengea uwezo watoa huduma za afya ili kuwasaidia akina mama wakati wa kujifungua na kuwaepusha na hatari ya kupata ugonjwa huo.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi (katikati) akikata upete kuashiria uzinduzi na makabidhiano ya vifaa tiba vya upasuaji wa fistula ya uzazi katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Bugando jijini Mwanza ambapo vimetolewa na shirika la Americares.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo.
Mkurugenzi Mkuu Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Dkt. Fabian Massaga akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mkurugenzi Mkazi Shirika la Americares akieleza namna shirika hilo limekuwa likishirikiana na hospitali ya Bugando kuboresha huduma mbalimbali ikiwemo za fistula.
Shujaa wa fistula anayepata matibabu hospitali ya Bugando, Pendo Dodo (kushoto) kutoka mkoani Mara akizungumza na waandishi wa habari ambapo amewahimiza akina mama wajawazito kuwahi katika vituo vya afya wakati wa kujifungua ili kupata msaada wa haraka wanapokumbwa na uchungu pingazi hatua itakayosaidia kukabiliana na ugonjwa wa fistula.
Wadau wa afya wakiwa kwenye hafla hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi ya Hospitali ya Bugando na shirika la Americares.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi (katikati) waliokaa akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa hospitali ya Bugando na shirika la Americares.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi (katikati) waliokaa akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa hospitali ya Bugando na shirika la Americares.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi (katikati) waliokaa akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa hospitali ya Bugando.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi (katikati) waliokaa akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Bugando, Americares na mashujaa wa fistula.
SOMA PIA>>> Habari zaidi hapa

No comments:

Powered by Blogger.