Waziri Mwigulu achangisha Milioni 443 ujenzi wa Shule za KKKT Dayosisi ya Kati
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com

Waziri wa Fedha na Mipango,Dk. Mwigulu Nchemba, akiwa amebeba kikapu chenye fedha wakati alipokuwa akiongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa shule mbili za sekondari zitakazomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kati katika changizo lililofanyika Kanisa la Emmauel Msalaba Mrefu Mjini Singida leo Juni 4, 2023. Wa pili kushoto ni Katibu Mkuu wa Kanisa hilo, Robert Kitundu.
Na Dotto Mwaibale, Singida
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, ameongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa shule mbili za sekondari zitakazomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kati ambapo jumla ya Sh. 443,063,800 zilipatikana na lengo lilikuwa ni kukusanya Sh.Milioni 500.
Katika fedha hizo zilizopatikana, taslimu zilikuwa ni Sh. 400,103, 800 na ahadi ikiwa ni Sh. 42,960,000. Dk.Mwigulu wakati wa harambee hiyo aliambatana na Mbunge wa Singida Mjini, Mussa Sima,Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu,Mbunge wa Makete, Festo Sanga, Mbunge wa Handeni Mjini, Reuben Kwagilwa na Mbunge wa Nsimbo, Anna Lupembe na viongozi mbalimbali wa kanisa hilo akiwamo Baba Askofu Dk.Alex Malasusa na Katibu Mkuu wa kanisa hilo, Robert Kitundu.
Akizungumza katika harambee hiyo iliyofanyika Kanisa la KKKT Usharika wa Emmanuel Msalaba Mrefu Mjini Singida, Dk.Nchemba ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi alisema Serikali inatambua mchango mkubwa unaofanywa na taasisi za dini hasa katika eneo la sekta ya elimu na afya kwani shule nyingi kongwe hapa nchini zilikuwa zimeanzishwa na taasisi hizo likiwamo kanisa la KKKT.
“Kanisa la KKKT hapa nchini ni taasisi iliyochangia sana katika maendeleo ya Mtanzania na lipo katika historia ya nchi yetu na haitafutika kwani ukiondoa hizi shule za sekondari zilizopewa jina katika kila kata kabla ya hapo shule zote zilizokuwa zikitumika kwa kiwango kikubwa zilikuwa ni za kanisa,” alisema Dk. Mwigulu.
Dk.Mwigulu alisema hata katika sekta ya afya hospitali nyingi zilizokuwa zikitoa huduma zilikuwa ni za kanisa na kwamba lengo la harambee hiyo lipo kwenye malengo yaleyale ya kuhudumia jamii.
Aidha, Mwigulu alisema moja ya muundo ambao anapenda kuhusisitiza katika utekelezaji wa shughuli za miradi ya maendeleo baina ya Serikali na sekta binafsi ni ile iliyofanywa na kanisa na kuwa viongozi wengi bila ya kujali dini zao wamepitia kwenye mikono ya kanisa na kusoma katika shule za taasisi hiyo.
Askofu wa kanisa hilo Dayosisi ya Kati, Dk.Syprian Hilinti akizungumza kwenye harambee hiyo alisema Halmashauri Kuu ya kanisa hilo imeweka mpango mkakati wa miaka mitano ya kujenga shule mbili za Sekondari Kiomboi na Kititimo kuanzia mwaka 2022/ 2027 kama mradi wa kitega uchumi cha kanisa.
“Miradi hii hailengi kuuwa historia za Missioni au biblia Kiomboi balikupanua kuendana na hali halisi na mahitaji ya wakati bila kuacha au kupoteza kusudi la injili bali kulitoa kwa ubora wa kukidhi changamoto za sasa.
Alisema kuwa hawawezi kuendesha gari la kisasa kwa kutumia gia za mwaka 1926 na kuwa halmashauri hiyo imeweka mipango ya muda mrefu kujenga kitega uchumi maeneo ya nyuma ya ofisi Kuu ya Dayosisi hiyo mara baada ya kumaliza mpango wa ujenzi wa shule.
Aliongeza kuwa sambamba na mpango huo Dayosisi imeweka sera ya kuendelea kuimarisha ukarabati, maongozi, usimamizi na utendaji kwenye vituo, miradi na taasisi zake zilizopo tayari.
Alisema katika awamu ya kwanza zilikuwa zikihitajika Sh.Milioni 500 na ndio lengo la kufanya harambee hiyo.
Katika hatua nyingine Dk. Hilinti alimuomba Dk.Mwigulu kuwasilisha ombi la kanisa hilo kwa Rais Samia Suluhu Hassan la kutaka warejeshewe Shule ya Sekondari ya Luluma iliyopo wilayani Iramba Kiomboi.
Askofu wa kanisa hilo Dayosisi ya Kati, Dk.Syprian Hilinti, akiendesha harambee hiyo.

No comments: