LIVE STREAM ADS

Header Ads

Mkuu wa Mkoa Singida ataka miradi ikamilike kwa wakati

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akifungua bomba la maji kuashiria uzinduzi wa mradi wa maji wa Kijiji cha Iglansoni katika hafla iliyofanyika Juni 5, 2023 wilayani Ikungi. Kulia ni Mkuu wa wilaya hiyo, Thomas Apson.

Na Dotto Mwaibale, Ikungi
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba amewaagiza maafisa manunuzi katika halmashauri za wilaya mkoani hapa kuweka mafundi wengi kwenye miradi inayotekelezwa kwa 'force acount' badala ya kutoa zabuni kwa mkandarasi mmoja ambapo imebainika wanachelewa kuikamilisha.

Serukamba alitoa agizo hilo Juni 5, 2023 alipokuwa Wilaya ya Ikungi katika mfululizo wa ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo na kuhimiza kukamilika kabla ya mwisho wa mwezi huu.

"Niwaombe maafisa manunuzi muache kutoa zabuni za ujenzi wa miradi kwa mkandarasi mmoja pale mradi husika unapofanywa kwa njia ya force acount kwani tunaongeza gharama pasipo sababu yoyote na wengi wa wakandarasi hao wakekuwa wakichelewesha ukamilikaji wake kutokana na kuwa na kazi nyingi," alisema Serukamba.

Alisema utekelezaji wa miradi kwa njia ya 'force acount' baada ya kuunda zile kamati tatu wanaitwa mafundi zaidi ya 10 na kushindanishwa kwa bei kulingana na ujenzi unaofanyika na yule atakayeonekana kuwa na bei ya chini ndio anayepewa kazi ya papo kwa papo kama kupiga ripu na kazi ya msimamizi wa mradi huo ni kuandika taarifa ya kazi iliyofanyika na gharama yake.

Alisema inapohitajika kujenga ukuta au kupaua mafundi hao wanaitwa tena na kushindanishwa na yule atakaye kuwa na bei nzuri atapewa kazi hiyo na kuwa utaratibu huo utakuwa ukiendelea hadi ujenzi utakapo kamilika na kuwa wakati huo vifaa vyote vinakuwa vimenunuliwa.

" Hii habari ya kumtafuta fundi mmoja mkubwa apewe kazi yote yeye na kulipwa fedha zote alafu aanze kutafuta mafundi mara nyingi kazi hiyo inakuwa haikamiliki kwa wakati na haraka kutokana na kuwa na kazi nyingi," alisema Serukamba.

Alisema ukamilishaji wa miradi kwa njia ya force acount ni miradi kufanyika kwa haraka na kupunguza gharama ya ujenzi na faida nyingine watakuwepo wananchi ambao watajitolea na kuwa kazi kubwa ya madiwani ni kuwahamasisha wananchi kujitokeza kujitolea.

Aidha, Serukamba aliwaomba wahandisi kwenda kutembelea na kukagua inapotekelezwa miradi hiyo kwani uzoefu unaonesha huwa hawaendi inapofanywa kwa njia ya 'force acount' wakiamini kazi hiyo haiwahusu bali inafanywa na kamati zilizoundwa.

Serukamba alisema Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo ambapo aliomba ikamilishwe kwa viwango vinavyotakiwa na kwa thamani halisi na si vinginevyo.

Katika hatua nyingine Serukamba alizindua miradi ya maji miwili ya Kijiji cha Iglansoni na Ihanja ambayo imetekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Ikungi ambayo inakwenda kuondoa changamoto ya muda mrefu waliokuwa wakiipata wananchi wa maeneo ilipo miradi hiyo ya kukosa maji.

Serukamba alitumia nafasi hiyo kuipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi na Mbunge wa Jimbo la Singida, Magharibi Elibariki Kingu kwa utekelezaji mzuri wa miradi yote aliyoitembelea na akawahimiza kuhakikisha wanaongeza kasi ya kuikamilisha kabla ya Juni 20,2023 ili ianze kufanya kazi ifikapo Julai 1, mwaka huu.

Miradi aliyoitembelea na kuridhishwa nayo ni mradi wa maji katika Kijiji cha Ihanja ambao pia utatoa huduma katika Kijiji cha Iseke, mradi wa maji wa Kijiji cha Iglansoni, ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi Malolo iliyopo Kijiji cha Iglansoni, ujenzi wa barabara za Ihanja, Nduru, Nduru Makilawa na Ikhakhamo- Mayaha-Ighombwe na ujenzi wa madarasa katika Shule ya Sekondari ya Puma.

Mradi mwingine alioukagua ni ujenzi wa Kituo cha Afya Iglansoni ambao ujenzi wake umekamilika kwa sehemu kubwa na kuwa tayari Serikali imekwisha peleka baadhi ya vifaa tiba ambapo aliagiza hadi ifikapo Julai 1, 2023 kituo hicho kianze kutoa huduma za afya kwani hakuna sababu itakayo sababisha kisianze kufanya kazi.
Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Ikungi, Mhandisi Hopeness Liundi (mwenye miwani) akimuelekeza jambo Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba wakati akizindua rasmi mradi wa maji wa Kijiji cha Iglansoni.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akikagua daraja linalojengwa Kijiji cha Nduru ambalo ni muhimu sana kwa kuinua uchumi wa wananchi wa eneo hilo na wilaya ya Ikungi kwa ujumla.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson akitoa maelezo ya ujenzi wa mradi wa maji wa Kijiji cha Iglansoni kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba (katikati aliyevaa kaunda suti)
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mradi wa maji wa Kijiji cha Iglansoni.
Diwani wa Kata ya Iglansoni (katikati) akimkabidhi zawadi ya karanga na boga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba.
Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Iglansoni, Musa Benard (kulia) akitoa taarifa ya ujenzi wa kituo hicho mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba.
Muonekano wa baadhi ya majengo ya kituo hicho cha afya Iglansoni.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba (katikati) akitoka kukagua kituo hicho cha afya.
Ukaguzi wa ujenzi wa madarasa ya Shule ya Msingi Malolo, ukifanyika.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ally Mwanga akijitambulisha na kuwasalimiawananchi wa Kijiji cha Nduru katika ziara hiyo.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ikungi, Stamili Dendego, akijitambulisha.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi akijitambulisha na kuwasalimia wananchi wa Kijiji cha Nduru..
Safari ya kwenda kukagua ujenzi wa daraja la Nduru ikifanyika.
Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA), Wilaya ya Ikungi, Mhandisi Ally Mimbi (kulia) akielezea kuhusu ujenzi wa daraja la Kijiji cha Nduru mbele ya mkuu wa mkoa.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akikabidhiwa zawadi ya mbuzi baada ya kukagua daraja hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mradi wa maji wa Kijiji cha Ihanja ambao pia utakuwa ukihudumia na Kijiji cha Iseke.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akimtwisha ndoo ya maji Mwajuma Athumani baada ya kuzindua mradi huo wa maji.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akimtwisha ndoo yenye maji, Agnes Bakari baada ya kuzindua mradi huo wa maji wa Kijiji cha Ihanja.

No comments:

Powered by Blogger.