LIVE STREAM ADS

Header Ads

Watakiwa kujitokeza kufanya uchunguzi wa awali wa Saratani

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Watanzania wametakiwa kujitokeza kwa wingi kufanya uchunguzi wa awali wa saratani, ili wakigundulika kuwa saratani wapatiwe tiba hospitali na kamwe watambue kuwa aina zote za ugonjwa wa saratani hutibiwa hospitalini peke yake na sio kwa waganga wa kienyeji.

Kauli hiyo imetolewa jana jijini hapa na Meneja wa Ubora na Ubunifu wa Mradi Mtambuka wa Saratani(TCCP) Edina Selestiniwakati alipokuwa akizungumza na mashujaa wa saratani, wakazi wa jiji la Mwanza na wadau mbalimbali wakati wa maadhimisho ya siku ya saratani duniani.

“ Kule kwa waganga wa kienyeji na tiba za asili, kwakweli wengi wanapoteza tu muda na kukomaza ugonjwa”, alisema na kuitaka jamii kuiepukana na vitu vinavyosababisha saratani kama vile kuepuka unywaji wa pombe na uvutaji wa sigara na tumbaku uliokithiri na visababishi vingine.

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Claudia Kaluri alisema saratani bado ni miongoni mwa magonjwa yanayoongoza duniani kwa kusababisha vifo kwa watu wengi bila kujali umri wala kipato cha mtu.

Alisema takwimu zinaonyesha kuwa katika kila watu 100,000 kuna wagonjwa 76 wapya wa saratani huku vifo vinavyosababishwa na ugonjwa huo vikifikia 68 kwa kila wagonjwa 100.

“ Vifo hivi vinatokana na wagonjwa wengi kufika hospitalini kwa kuchelewa”, alisema.

Mwenyekiti wa Upendo Cancer Foundation Claris Mhimba licha ya kuwashukuru ndugu, jamaa na marafiki walioungana nao kwenye maadhimisho hayo kwa kuwatia faraja wagonjwa na mashujaa wa saratani walioko jijini Mwanza aliitaka jamii kujitokeza mapema ili kushiriki kwenye upimaji wa awali wa saratani ili kuweza kuzitambua afya zao na kwamba baada ya kujitambua kwa watakaobainika kuwa na saratani itakuwa ni rahisi kutibiwa.

“Sisi tuliosimama hapa leo, tunalinga kusherehekea siku hii ya mashujaa ni kwa sababu tuliwahi kufanyiwa uchunguzi na kutibiwa”, alisema.

Alisema kwa mujibu wa takwimu zilizopo, kati ya wagonjwa 100 wa saratani watu 68 hufariki kwa ugonjwa huo na kwamba wao mashujaa wa saratani ni wale 32 waliobaki kati ya 68 waliofariki dunia kwa ugonjwa wa saratani.

Aliwashukuru wadau mbalimbali kwa kuendelea kuwasaidia ukiwepo Mradi Mtambuka wa kudhibiti saratani(TCCP) ambao uliwapatia mafunzo namna ya kukabiliana na ugonjwa wa saratani na kuwawezesha wao kama mashujaa wa saratani kuungana pamoja .

Aliwataka wadau mbalimbali katika jamii kuendelea kuihamasisha jamii kutogoopa kwenda kufanyiwa uchunguzi wa awali wa saratani kwa madai kuwa bado wapo wanaendelea kuamini ushirikina.

“Hebu tuwasaidie kuelewa hili kwa sababu sisi tumepita pale tumeona hali halisi ilivyo, pamoja na kwamba matibabu ni magumu lakini ndio taratibu zake tumepitia hapo na hatimaye leo tumeweza kusimama mbele ya umma tukishangilia kwamba tumepona”, alisema

Kwa upande wake, Mtalaam wa Mionzi Tiba kwa wagonjwa wa saratani kutoka Idara ya Saratani Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, Kidaya Bashari alisema changamoto kubwa iliyoko Kanda ya ziwa ni watu kuchelewa kufika hospitalini, ambapo asilimia 70-80 ya wagonjwa wa saratani huenda bugando kutibiwa wakiwa wamechelewa.

Maadhimisho hayo yalianza kwa mashujaa wa saratani kupitia Cancer Foundation kufanya maandamano kwa kushirikiana na wadau na marafiki ambapo waliwatembelea wagonjwa wa saratani waliolazwa katika wodi ya saratani katika hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando na wazazi wanaowauguza watoto walio katika Kituo cha Iccare na kuwapa zawadi mbalimbali kwa ajili ya kuwatia moyo na kuwasaidia wakati wakiendelea na matibabu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo cha Kulea Watoto wenye saratani kilichoko Bugarika wilayani Nyamagana cha Iccare Tanzania Hillary Sued aliwashukuru Upendo Cancer Foundation kwa kuwatembelea wazazi wanaowauguza watoto wenye saratani katika kituo chake kwa kutoa msaada wa bidhaa, vyakula na vitu mbalimbali kwa ajili ya watoto hao.

Katibu wa Upendo Cancer Foundation Rose Sawika alisema kitendo cha mtu yeyote katika jamii kupima afya yake kwenye uchunguzi wa awali wa saratani na kupokea majibu yake huyo ni shujaa tayari wa saratani.

Sawika aliwataka Watanzania kuendelea kujitokeza kjufanya uchunguzi wa awali wa saratani kwa madai kuwa ugonjwa wa saratani ukijulikana mapema unatibika.

Rais wa Lion Club - Mwanza City Mahesh Choudhary ambaye alitoa bidhaa na zawadi kwa watoto wenye saratani, aliitaka jamii kujengautamaduni wa kupima afya zao.

Kwa upande wao baadhi ya wazazi wanaouguza watoto saratani katika Kituo hicho Cha Iccare wameushukuru uongozi wa hospitali ya Bugando Kwa kupatiwa matibabu na watoto hao wanaendelea vyema.

Mmoja wa wazazi anayeuguza mtoto wake Kituoni hapo Daines Kalori ambaye ni mkazi wa Ukerewe mkoani Mwanza anaushukuru uongozi wa Kituo hicho na ule wa hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa kutoa matibabu kwa mwanawe anayeugua saratani ya figo na kwa sasa anaendelea vizuri.

Naye Phares Naftari mkazi wa Kibondo mkoani Kigoma anaushukuru uongozi wa hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa kumtibia mwanawe saratani ya tezi na kwa sasa anaendelea vizuri na matibabu.
Na Nashon Kennedy, Mwanza
Mashujaa wa saratani katika picha ya pamoja wakiwa na zawadi zao walizowanunulia watoto wenye saratani katika Kituo Cha watoto wanaougua saratani cha Iccare Tanzania.
Mkurugenzi wa Katua Decorations, Juliet Katua( aliyevaa gauni la batiki kushoto) akikabidhi mahitaji mbalimbali katika Kituo cha kulelea watoto wanaougua saratani jijini Mwanza.
Mkurugenzi wa Kituo cha watoto wanaougua Saratani cha Iccare Hillary Sued (kushoto) akizungumza na mashujaa wa saratani.
Daines Kalori mkazi wa Ukerewe mkoani Mwanza akitoa ushuhuda namna huduma za Saratani zimeboreshwa ambapo mwanae anapata matibabu katika Hospitali ya Bugando.

No comments:

Powered by Blogger.