LIVE STREAM ADS

Header Ads

Usalama wa mtoto unaanzia nyumbani

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Wazazi na walezi wa watoto wametakiwa kuhakikisha wanaweka mazingira mazuri nyumbani kwa mtoto kuishi kwa kuwa malezi bora ya mtoto yanaanzia nyumbani ukiwemo usalama wake.

Akizungumza katika kikao kazi cha ulinzi na usalama wa mtoto kilichoandaliwa na shirikika la uchumi wa nyumbani (TAHEA) na kuwashirikisha maafisa wa jeshi la polisi kitengo cha dawati la jinsia pamoja na waandishi wa habari mratibu wa program ya malezi na makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto wa shirika hilo Damas Joachim amesema wazazi na walezi ndio askari wa kwanza kuhakikisha mtoto yupo salama katika mazingira yote yanayomzunguka.

Damas amesema kama kunachangamoto nyumbani mtoto huwa mtu wa kwanza kuathirika hivyo wazazi wanatakiwa kutenga muda wao wa kuwasikiliza watoto kama wanachangamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi mapema kabla hazijaleta madhara kwa mtoto lakini kwa watoto wenye umri wa mwaka 0-5 ni vema kuwasikiliza na kuwakagua ili kujua kama viungo vyao hasa vya siri kama vipo salama.

“Sio kama wazazi hawaoni hatari za kiusalama wanazoweza kupata watoto wao hasa hawa wenye umri wa kuanzia mwaka 0-5 wanajua na ndio maana wengi wao hutafuta wafanyakazi wa ndani kwaajili ya kuwalinda na wakati mwingine kuwapeleka shule za bweni hii haitoshi lazima tu wazazi watimize wajibu wao wa kuishi na watoto wao ili waweze kuwasaidia katika safari yao yote ya makuzi”.alisema Dismas

Damasi amesema ili kuwasaidia wazazi katika suala zima la malezi TAHEA wameanzisha jarida la Mbeleko ambalo litawasaidia wazazi kujua majukumu yao katika suala zima la malezi na makuzi ya mtoto.

Kwa upande wake Peter Matyoko msimamizi wa miradi ya elimu kutoka TAHEA amesema miradi mingi inayoanzishwa na shirika hilo ni ile inayoanzishwa na jamii ukiwemo mradi wa malezi na makuzi ukiwa na lengo la kuhakikisha mtoto anapata mahitaji yake ya msingi kuanzia anapokuwa tumboni hadi anapozaliwa na kuwa mtu mzima.

Peter amesema TAHEA imefanikiwa kujenga vituo vya jamii vya kulelea watoto mchana maeneo ya pembezoni kutokana na huduma hiyo kukosekana katika maeneo hayo kwa lengo la kuwasaidia watoto kupata msingi mzuri wa elimu pamoja na kuwahakikishia usalama watoto.

“Mfano eneo la Igombe ni hatarishi sana kwa watoto maana wakazi wa maeneo hayo wanajihusisha sana na shughuli za uvuvi na wazazi mara nyingi wanawaacha nyumbani peke yao kwa kuliona hilo tumeshirikiana na jamii na kujenga kituo kizuri cha watoto na watoto tunaowachukua ni wale wa miaka miwili na nusu mpaka mine”.alisema Peter.

Akizungumzia hali ya vitendo vya kikatili kwa watoto mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Mwanza, Faraja Mkinga amesema watoto wamekuwa katika hatari ya kufanyiwa matukio ya ukatili ikiwemo ubakaji na ulawiti kutokana na wahusika kuwa watu wa karibu na familia na kuwataka wazazi na walezi kuwa mstari wa mbele katika kuwalinda watoto.

Faraja amesema hali ya kiuchumi kuyumba ni sababu nyingine iyonasababisha watoto wengi wanaofanyiwa ukatili kupoteza haki zao kutokana na wazazi kuogopa kuripoti matukio hayo Polisi kwa hofu kuwa ndugu akichukuliwa hatua familia itashindwa kujikimu kimaisha.

“Siku hizi wazazi hasa wakiume wamekuwa wakiwafanyia vitendo vya ukatili watoto wao kama ubakaji na ulawiti lakini mama au walezi waliopo nyumbani huogopa kumchukulia hatua hasa pale baba anapokuwa tegemezi hapo nyumbani”.alisema Faraja

Kwa upande wake Askari mpelelezi Sajent Leah kutoka kituo cha One Stop Centre amesema wao kupitia kituo chao wamekuwa wakiwasaidia watoto waliobakwa dawa za kuzuia maambukizi zinazofanyakazi ndani ya saa 72 na mzazi hupewa mwongozo wa namna ya kuzitumia dawa hizo.

Akizungumzia Jarida la Mbeleko mara baada ya kulisoma Laurencia Maguzu mzazi mwenye watoto wawili mkazi wa Mkolani jijini Mwanza amepongeza hatua ya shirika la TAHEA kuanzisha jarida hilo la Mbeleko kwaajili ya kuwakumbusha wazazi wajibu wao katika malezi.

“Jarida ni zuri lina vitu ambavyo tunakutananavyo kila siku lakini ukisoma ndio unashituka kujua kumbe hiki kinatakiwa kufanywa kwa mtindo mwingine lakini kuna kurasa zinawahusu watoto pia hivyo ni jarida la familia”.alisema Laurencia.

Kwa mujibu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, mwaka 2022 kulikuwa na matukio 12,163 ya ukatili dhidi ya watoto ambapo kati ya hayo, matukio 9,962 walikuwa watoto wa kike na 2,201 walikuwa watoto wa kiume.
Na Tonny Alphonce, Mwanza
Mratibu wa Miradi ya Watoto (Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali Watoto) kutoka Shirika la Uchumi wa Nyumbani (Tanzania Home Economics Organization- TAHEA) Mwanza, Damas Joachim akizungumza kwenye kikao cha ulinzi na usalama wa mtoto jijini Mwanza.
Mratibu wa Miradi ya Elimu kutoka Shirika la TAHEA Mwanza, Peter Matyoko akizungumza kwenye kikao cha ulinzi na usalama wa mtoto jijini Mwanza.
Wadau wa ulinzi na usalama wa mtoto wakiwa kwenye kikao kazi jijini Mwanza.

Wadau wa ulinzi na usalama wa mtoto jijini Mwanza wakiwa kwenye picha ya pamoja.

No comments:

Powered by Blogger.