LIVE STREAM ADS

Header Ads

TPA yawasilisha mapendekezo ya maboresho ya tozo za bandari

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imewasilisha mapendekezo ya maboresho ya tozo za bandari kwa wadau mbalimbali wa usafirishaji majini mkoani Mwanza ili kutoa fursa kwa wadau hao kuyaelewa mapendekezo hayo na kutoa maoni yao kabla ya kuanza kutumika.

Warsha ya uwasilishaji mapendekezo hayo imefanyika Juni 30, 2023 jijini Mwanza ikiratibiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Huduma za Meli Tanzania (TASAC) yenye mamlaka kisheria ya kuratibu na kupokea maoni ya wadau kuhusiana na mapendekezo yaliyowasilishwa na TPA kwa ajili ya hatua ya uchakataji kabla ya kuidhinishwa ili kuanza kutumika.

Akiwasilisha mapendekezo hayo, Afisa Mkuu Masoko TPA, Robert Soko amesema lengo ni kuwa na tozo shindani zitakazosaidia kuboresha ufanisi katika utendaji wa bandari, kuongeza wateja pamoja na shehena ya mizigo. 

Amesema mapendekezo ya tozo yanayofanyiwa marekebisho ni ya mwaka 2018 hivyo mamlaka hiyo imependekeza kuwepo kwa viwango vya tozo kulingana na mahitaji ya wateja, masoko, ushindani, teknolojia na kubwa zaidi kusaidia maboresho ya bandari nchini ili kuwa na ufanisi zaidi.

Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Nahson Sigalla amesema mamlaka hiyo imefungua milango kwa wadau kuendelea kutoa maoni kuhusiana na mapendekezo ya maboresho ya tozo za bandari yaliyowasilishwa na TPA hadi Julai 20, 2023 kwa njia ya barua pepe ya tariff@tasac.go.tz ama kufikisha maoni yao kwa njia ya maandishi ofisini.

"Mapendekezo haya yamegusa makundi matatu makubwa ambayo ni marekebisho ya mpangilio wa majedwali ya tozo ili kumrahisishia mtumiaji, marekebisho ya maneno yenye utata ikiwemo vifurushi pamoja na mabadiliko ya tozo" amesema Sigalla na kuongeza;

"Baada ya hatua ya kukusanya maoni, yatachambuliwa na baadae kwenda ngazi ya maamuzi kabla ya tarehe mpya ya kuanza kutumika kutangazwa ambapo kawaida zoezi hili halizidi miezi miwili baada ya kufunga muda wa kupokea maoni" amesema Sigalla.

Miongoni mwa mapendekezo yaliyoonekana kuvuta hisia za wadau wengi ni tozo ya mazao ya uvuvi kuanzia kilo 6.5 itakayokuwa inatozwa kwa kiwango cha shilingi 10 kwa kilo moja ambapo chini ya kilo sita hakutakuwa na tozo. 

Wadau wameshauri eneo hilo kurekebishwa na kiwango cha tozo kianzie kilo 20 ili kuondoa adha kwa wananchi watakaotumia mazao hayo kwa kitoweo kulazimika kulipia tozo ilihali wanaopaswa kulipa tozo hiyo ni wanaosafiriaha mazao hayo kibiashara.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Nahson Sigalla akizungumza kwenye warsha ya kuwasilisha mapendekezo ya maboresho ya tozo za bandari kwa wadau wa bandari/ usafirishaji majini mkoani Mwanza.
Afisa Mkuu Masoko Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Robert Soko akiwasilisha mapendekezo ya maboresho ya tozo za bandari kwa wadau wa usafirishaji majini mkoani Mwanza.
Kapteni Mande Mangapi kutoka kampuni ya usafirishaji majini ya Kamanga Ferry akiwasilisha maoni kuhusiana na mapendekezo ya maboresho ya tozo za bandari ambapo ameshauri mabadiliko ya maboresho ya tozo za bandari yaendane na uboreshaji wa bandari nchini.
Mkurugenzi wa kampuni ya Mkombozi Ferry, Ibrahim Chacha akiwasilisha maoni yake wakati wa hafla hiyo ambapo ameshauri tozo ya mafutwa kutozwa kwa lita badala ya tani kama TPA ilivyopendekeza.
Kepteni Mhoja Malima kutoka Chuo cha Uvuvi Nyegezi jijini Mwanza akiwasilisha maoni yake wakati wa warsha hiyo ambapo ameshauri maboresho ya tozo za bandari kuendana na Sheria ya Uvuvi ya mwaka 2023 na Kanuni zake za mwaka 2020 inayozuia wasafirishaji wa mazao ya uvuvi kutozwa tozo kwa mazao yaliyo chini ya kilo 30.
Wadau wa bahari jijini Mwanza wakiwa kwenye warsha ya kuwasilisha mapendekezo ya maboresho ya tozo za bandari na kushiriki utoaji maoni kuhusu mapendekezo hayo kabla ya kuanza kutumika.
Wadau wa bahari jijini Mwanza wakiwa kwenye warsha hiyo.
Wadau wa bahari jijini Mwanza wakiwa kwenye warsha hiyo.
Wadau wa bandari jijini Mwanza wakiwa kwenye warsha ya kupokea mapendekezo ya maboresho ya tozo za bandari na kutoa maoni yao kuhusiana na mapendekezo hayo kwa ajili ya kuchakatwa kabla ya kuanza kutumika.

No comments:

Powered by Blogger.