LIVE STREAM ADS

Header Ads

Waziri Mwigulu ahimiza matumizi sahihi ya takwimu

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Mwigulu Nchemba, akihutubia wakati akifungua mafunzo ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwa viongozi na watendaji wa Mkoa wa Singida yaliyofanyika Shule ya Sekondari ya Kizaga wilayani Iramba Julai 1, 2023.

Na Dotto Mwaibale, Singida
Wazriri wa Fedha na Mipango Dk. Mwigulu Nchemba amewataka watendaji wa serikali kuzingatia matumizi sahihi ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi katika Mipango ya Maendeleo.

Nchemba ameyasema hayo mkoani Singida jana wakati akifungua mafunzo ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwa viongozi na watendaji wa Mkoa wa Singida yaliyofanyika Shule ya Sekondari ya Kizaga wilayani Iramba.

Alisema mipango mingi inashindwa kutoa huduma kwa wananchi kutokana na kutokutumia Takwimu zilizopo katika kupanga mipango hiyo kwenye shughuli mbalimbali.

“Tuzingatie Takwimu sahihi zilizopo, matokeo ya Takwimu na maoteo itatusaidia sana uko mbele tuendako kwani zamani sensa ililenga zaidi kujua idadi ya watu,” alisema Mwigulu.

Akitoa mfano mdogo wa kutofanya mambo yetu kwa Takwimu alisema inakuweje inatokea tuna walimu wengi wa baadhi ya masomo hawana hata nafasi, lakini kwenye nchi hiyo hiyo kuna walimu wengi ambao akili zinalingana na hawana masomo.

Dk. Mwigulu alisema kutozingatia Takwimu tumekuwa na dharura nyingi ambazo zimekuwa zikiipa nchi changamoto kubwa akitolea mfano wa Serikali ilipolazimika kujenga shule za sekondari za kata nchi nzima kufuatia kuwepo na wanafunzi wengi waliotakiwa kuanza kidato cha kwanza kushindwa kupelekwa shuleni kwa kukosa mahali pa kusoma.

Alisema mambo hayo ya dharura na kutozingatia takwimu yamekuwa yakimpa Rais wakati mgumu akitoa mfano kuwa leo anapelekewa idadi ya ujenzi wa madarasa pengine 100, anayajenga na baada ya siku chache anaambiwa tena idadi ile haikuwa sawasawa hivyo madarasa hayo hayatoshi.

Awali kabla ya kufungua mafunzo hayo Dk.Mwigulu aliwaomba watanzania kuendelea kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na kazi kubwa anayoifanya ya kuwaletea maendeleo wananchi ambapo kwa muda mfupi aliokaa madarakani ameweza kufanya mambo makubwa ambayo yamemgusa kila mtanzania.

Akitaja baadhi ya mambo hayo ni ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ambao ujenzi wake umebakia asilimia 15 ukamilike, ujenzi wa zahanati na vituo vya afya nchi nzima, kuongeza bajeti ya ujenzi wa barabara za vijijini (TARURA) kutoka Sh.Bilioni 200 hadi kufikia Sh. Trioni 1, kuongeza bajeti ya kilimo kutoka Sh.Bilioni 200 hadi kufikia Trioni moja na Bilioni 200 bajeti ambayo haijawa kufikiwa na awamu zote za Serikali zilizopita.

Alitaja mambo mengine kuwa ni kuongeza mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka Bilioni 400 hadi kufikia Bilioni 750 na kuviingiza kwenye mikopo vyuo vya kati vya afya , elimu na vya ufundi zaidi ya 50 sanjari na kutoa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha sita.

Dk.Mwigulu alitumia nafasi hiyo kuipongeza Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) chini ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk.Albina Chuwa kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kukusanya takwimu sahihi kwa ajili ya kukamilisha mipango ya maendeleo nchini.

Aidha, alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhamasisha wananchi katika shughuli za maendeleo na kuifuatilia kwa karibu.

“Hii ni faida kubwa ya kuwa na mkuu wa mkoa ambaye aliwahi kuwa mbunge mwenye uwezo wa kujua mahitaji ya wananchi na kuyafanyia kazi anatusaidia hata sisi wabunge wa mkoa huu katika maeneo mbalimbali endeleeni kumpatia ushirikiano,” alisema Mwigulu.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba alisema Mipango na programu zote za maendeleo za mkoa huo zinapangwa kwa kuzingatia matokeo ya Sensa hiyo ya Watu na Makazi, Majengo na Sensa ya Anuani za Makazi ya mwaka 2020/ 2022.

Alisema katika mipango na programu za mwaka wa fedha 2023/2024 zimezingatia matokeo ya Sensa na takwimu nyingine zinazozalishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu na kuwa ili wananchi wa mkoa wa Singida waweze kupata huduma Bora, mipango ya mkoa huo itazingatia matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.

Mtakwimu Mwandamizi, Ofisi ya Taifa ya Takwimu- (NBS), Mdoka Omary alisema madhumini ya mafunzo hayo ni kusambaza matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2020/ 2022 na kuwajengea uwezo wadau wote na viongozi namna ya kutumia matokeo hayo katika kutekeleza majukumu yao ya uongozi na utendaji katika Serikali kuu na mamlaka ya Serikali za mitaa.

Alisema kufanya hivyo kutasaidia kuongeza uwezo na kupanua wigo wa matumizi ya sensa ya watu na makazi kwa Serikali.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akitoa salamu za Mkoa wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Mtakwimu Mwandamizi, Ofisi ya Taifa ya Takwimu- (NBS), Mdoka Omary, akizungumzia madhumuni ya mafunzo hayo.
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Moses Machali, akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Mbunge wa Singida Mjini Musa Sima akizungumza kwa niaba ya wabunge wenzakewakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akiteta jambo na Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Mwigulu Nchemba kabla ya ufunguzi wa mafunzo hayo.
Wenyeviti wa Halmashauri za Wilaya za Singida wakiwa kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo. Kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, Hussein Simba, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Innocent Msengi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, James Mkwega, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Jumanne Mlagaza na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida, Yagi Kiaratu.
Washiriki wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Katibu Tawala mpya wa Wilaya ya Iramba, Warda Abdallah Obathany akitambulisha viongozi mbalimbali wa wilaya hiyo waliokuwepo kwenye mafunzo hayo. kabla ya kufanya utambulisho huo naye alitambulishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk.Mwigulu Nchemba.
Mtaalam wa Habari na Mawasiliano wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Said Ameir akiwatambulisha maofisa wa NBS kutoka makao makuu waliokuwepo kwenye mafunzo hayo.
Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida katika mafunzo hayo, ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Utawala na Rasilimali Watu, Stephen Pankras akitoa utambulisho wa viongozi mbalimbali waliohudhuria mafunzo hayo.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Lucy Boniface akitoa salamu za chama wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Mafunzo yakitolewa.
Mafunzo yakiendelea.
Wakuu wa Wilaya wakiwa kwenye mafunzo hayo. Kutoka kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson, Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Mragili na kulia ni Katibu Tawala Wilaya ya Iramba, Warda Abdallah Obathany.
Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Singida, wakitoa heshima mbele ya viongozi waliokuwepo meza kuu wakati wakitambulishwa.
Taswira ya mafunzo hayo.

No comments:

Powered by Blogger.