LIVE STREAM ADS

Header Ads

MSD yapiga hatua juhudi za usambazaji dawa

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Wafanyakazi wa Bohari ya Dawa (MSD) wakitumia mtumbwi unaotumia injini ya mafuta kusafirishia dawa na vifaa tiba kwenda kwenye vijiji vinazungukwa na Ziwa Nyasa katika Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya.

Na Mwandishi Wetu, Kyela
Bohari ya Dawa (MSD) imeeleza kwamba kwa sasa imefikia asilimia 95 ya usambazaji wa dawa na vifaa tiba katika Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya.

Hatua hiyo imefikiwa mbali ya changamoto zilizopo ikiwemo katika kijiji cha Ikombe ambacho kinazungukwa na Ziwa Nyassa hivyo kukosa barabara na ziwa linapochafuka dawa na watumishi kuwa hatarini.

Akizungumza wilayani humo Mfamasia wa Wilaya ya Kyela Emanuel Chacha amesema hali ya upatikanaji wa bidhaa za afya wilayani Kyela mkoani Mbeya ni asilimia 95 na wamefikia hali hiyo licha changamoto zilizopo katika kijiji cha Ikombe kilichopo kisiwani mwa Ziwa Nyasa.

“Tuna vituo 37 vinavyopata dawa na vifaa tiba kwa mfumo wa kielektroniki wa ELMIS kati ya vituo hivyo vyote vinafikika kasoro kimoja ambacho kipo kisiwani katika kijiji cha Ikombe kilichozungukwa na Ziwa Nyasa.

“Kutokana na juhudi za Serikali kituo hicho pia kinapokea vifaa vya afya kwa asilimia 90 kutoka MSD,”amesema na kutumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kipaumbele kwa sekta ya afya nchini.

Amesisitiza hatua hiyo ni matokeo ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba vyenye ubora na kwa wakati na kuboresha huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Ikombe Dk.Joshua Katabazi, amesema ufikishaji wa dawa katika zahanati hiyo umekuwa na changamoto kutokana na kukosekana kwa barabara na kijiji kuzungukwa na Ziwa Nyasa.

Ameongeza kituo hicho kinatumia njia ya majini na kinapokea dawa na vifaa tiba kila mwezi kutoka MSD hivyo upatikanaji wa vifaa vya afya kuwa wa asilimia 90.

“Kunachangamoto ya usafirishaji wa dawa kutoka Matema hadi hapa lakini Serikali yetu inahakikisha maboresho sekta ya afya wanakijiji wa Ikombe wanakuwa wanufaika na sisi watoa huduma tunajivunia wananchi kupata dawa, vipimo na matibabu yote wanapofika kituoni,”amesema.

Wakati huo huo akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Ikombe Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji Ezekiel Mwamgunda, amesema wanaishukuru Serikali mbali ya kuwapo kwa changamoto ya kupitisha dawa katika maji zimekuwa zikifika kwa wakati.

Kuna muda Ziwa linachafuka hivyo kuwa na hatari ya dawa na watumishi wa MSD kuzama ombi langu kwa Serikali kuona haja ya kujenga barabara, mazingira haya ni hatarishi na hali inapokuwa mbaya zaidi inabidi wananchi wajitolee kupita pori kwa pori kufuata dawa kule ng’ambo eneo la Matema,”amesema.
Vijana wakisaidia kubeba dawa kuzipeleka katika Zahanati baada ya kushushwa katika mtumbwi.
Dawa na vifaa tiba zikishushwa kwenye gari tayari kwa kusafirishwa kwa njia ya mitumbwi kupelekwa kwenye Zahanati na Vituo vya Afya wilayani Kyela mkoani Mbeya.
Mitumbwi ikitumika kuwapeleka wananchi katika Zahanati na Vituo vya Afya wilayani humo.
Muonekano wa moja ya Zahanati inayopokea dawa na vifaa tiba kutoka MSD kwa kusafirishwa kwa mitumbwi wilayani humo.

No comments:

Powered by Blogger.