LIVE STREAM ADS

Header Ads

Waziri Biteko azindua Zahanari iliyojengwa na Wanawake Wachimbaji Madini

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko amezindua Zahanati ya Kijiji cha Nyamishiga katika Halmashauri ya Msalala Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, iliyojengwa na kikundi cha wanawake wachimbaji madini cha TAWOMA Mshikamano.

Dkt. Biteko amezindua Zahanati hiyo Jumatatu Julai 03, 2023 na kukabidhi pia gari la wagonjwa (Ambulance) lililonunuliwa na kikundi hicho ambacho kimechangia jumla ya shilingi milioni 275 kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika Kijiji cha Nyamishiga.

Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi huo, Waziri Dkt. Biteko aliwapongeza wanawake wanaounda kikundi cha TAWOMA Mshikamano kwa ujenzi wa Zahanati hiyo pamoja na miradi mingine ikiwemo ujenzi wa nyumba ya mtumishi pamoja na kununua gari la wagonjwa.

“Ninawapongeza sana kwa kusimamia vizuri sekta ya madini, niwaahidi kusimamia maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwapa kipaumbele wanawake katika sekta ya madini” alisema Dkt. Biteko na kuongeza kuwa kikundi hicho kimeondoa dhana potofu kwamba wanawake hawawezi kusimamia mgodi hivyo Serikali iko tayari kuwapa leseni ya uchimbaji madini.

“Serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Dkt. Samia imetoa fursa kwa wote kushiriki uchumi wa madini, yale mashaka kwamba wanawake hawawezi kusimamia migodi yameondolewa na wanawake wa Nyamishiga, mnastahili kupata leseni ya uchimbaji” alisema Dkt. Biteko.

Mwenyekiti wa kikundi cha TAWOMA Mshikamano, Semeni Malale alisema Zahanati hiyo ilianza kujengwa mwaka 2018 kwa nguvu za wananchi ambapo mwaka 2022 kukindi hicho kilikabidhiwa boma kwa hatua ya umaliziaji.

“Tumeweza kumalizia jengo la Zahanati na ujenzi wa nyumba ya mtumishi kwa gharama ya shilingi 166,356,000, madwati 100 yenye thamani ya shilingi 7,000,000, samani za Zahanati shilingi 4,000,000, gari la wagonjwa shilingi 75,000,000” alisema Malale.

Naye Mkuu wa Mkoa Shinyanga, Christina Mdeme alisema Serikali itahakikisha inafikisha vifaa tiba, dawa na watumishi katika Zahanati hiyo ili kuwaondolea adha wananchi kutembea umbali wa kilomita zaidi ya 10 kufuata huduma za afya.

Mdeme pia alitumia fursa hiyo kuahidi kwamba Serikali itafikisha huduma ya umeme, maji, barabara na kujenga uzio katika Zahanati hiyo ili kuondoa adha wagonjwa wakiwemo wajawazito.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mbini Mhita alisema kikundi cha TAWOMA Mshikamano kimekuwa na ushirikiano mzuri na Kijiji cha Nyamishiga katika shughuli za maendeleo; “akina mama ni walezi na wakipata wanarudisha nyumbani kuhudumia familia, jamii na taifa kwa ujumla” alisema Mhita.

“Tunang’aa na kupongezwa kufanya vizuri kwa ukusanyaji wa mapato kutokana na uwepo wa sekta ya madini katika Halmashauri yetu hivyo tunashukuru kwa usimamizi mzuri wa sekta hii” alisema Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Msalala, Flora Sagasaga.

Awali Mtendaji wa Kijiji cha Nyamishiga, Teddy Jacob aliomba wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo wachimbaji wengine wa madini kuendelea kusaidia kutatua changamoto katika Zahanati hiyo ikiwemo ujenzi wa uzio na nyumba za watumishi ili kutoa huduma bora kwa wananchi zaidi ya elfu nne wa Kijiji hicho.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa jengo la Zahanati ya Kijiji cha Nyamishiga Kata ya Lunguya katika Halmashauri ya Msalala Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga iliyojengwa na kikundi cha wanawake wachimbaji madini cha TAWOMA Mshikamano.
Mkuu wa Mkoa Shinyanga, Christina Mdeme akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa jengo la Zahanati ya Kijiji cha Nyamishiga Kata ya Lunguya katika Halmashauri ya Msalala Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga iliyojengwa na kikundi cha wanawake wachimbaji madini cha TAWOMA Mshikamano.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama, Flora Sagasaga akizungumza kwenye hafla hiyo.
Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye hafla hiyo
Wananchi wakiwemo wachimbaji wadogo wa madini ya dhahamu katika Kijiji cha Nyamishiga wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa Zahanati ya Kijiji hicho.
Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko akikagua gari la wagonjwa (Ambulance) lililonunuliwa na wanawake wachimbaji madini ya dhahabu TAWOMA Mshikamano Group kwa ajili ya Zahanati ya Kijiji cha Nyamishiga.
Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko akifurahia baada ya kupokea gari la wagonjwa lililonunuliwa na kikundi cha wanawake wachimbaji madini cha TAWOMA Mshikamano kwa ajili ya Zahanati ya Kijiji cha Nyamishiga.
Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko (kulia) akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Msalala ufunguo wa gari la wagonjwa (Ambulance) lililonunuliwa na kikundi cha wanawake wachimbaji madini TAWOMA Mshikamano kwa ajili ya Zahanati ya Kijiji cha Nyamishiga.
Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko akizungumza wakati wa kukabidhi gari la wagonjwa lililonunuliwa na kikundi cha wanawake wachimbaji madini TAWOMA Mshikamano kwa ajili ya Zahanati ya Kijiji cha Nyamishiga Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama. Wanaoshuhudia ni pamoja na Mkuu wa Mkoa Shinyanga, Christina Mdeme na Mkuu wa Wilaya Kahama, Mboni Mhita.
Gari la wagonjwa (Ambulance) lililonunuliwa na kikundi cha wanawake wachimbaji madini TAWOMA Mshikamano kwa zaidi ya shilingi milioni 75.
Msanii wa nyimbo za asili, Elizabeth Maliganya akitumbuiza kwenye hafla hiyo.
Wanawake wanawake wachimbaji wa madini wakifurahia burudani wakati msanii Elizabeth Maliganya akitumbuiza.
Wanawake wanawake wachimbaji wa madini wakifurahia burudani wakati msanii Elizabeth Maliganya akitumbuiza kwenye hafla ya uzinduzi wa Zahanati ya Kijiji cha Nyamishiga iliyoambatana na kukabidhi gari la wagonjwa (Ambulance).
Tazama BMG TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.