LIVE STREAM ADS

Header Ads

LATRA yaahidi kuboresha shughuli za usafirishaji

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.comMkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), CPA. Habib Suluo.



Na Dotto Mwaibale, Singida
Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), CPA. Habib Suluo ameihakikishia Kamati ya Bunge ya Miundombinu kuwa mamlaka hiyo itaendelea kutekeleza majukumu yake kikamilifu kwa kuboresha shughuli za usafirishaji nchini na kuwapima madereva ili waendeshe vyombo vya moto kwa usalama zaidi.

Suluo ameyasema hayo baada ya Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge, Miraji Mtaturu kuipongeza LATRA kwa kusimamia mfumo utoaji wa tiketi kwa mtandao ambao umeanza kupunguza kero kwa abiria.

''Tutaendelea kutekeleza majukumu yetu kwa ukamilifu na kuufanyia kazi ushauri uliotolewa na Kamati ya Bunge ya Miundombinu kwa lengo la kuboresha shughuli za usafirishaji ikiwemo kuendelea kuwatahini madereva ili kuhakikisha abiria wanasafiri kwa usalama'' amesema Suluo wakati akiwasilisha taarifa ya mamlaka hiyo kwa wabunge wa kamati hiyo Agosti 25, 2023.

LATRA katika kuhakikisha inadhibiti mawakala wa mabasi wanaokwepa kukata tiketi kwa mfumo wa mtandao, LATRA Mkoa wa Singida imetoza faini ya Shilingi 250,000 kwa kila basi kwa mabasi matano na kuvuna jumla ya Shilingi 1, 250,000.

Mabasi yaliyotozwa faini hizo ni ya kampuni ya Nyahunge mabasi manne na basi moja la kampuni ya Supafeo ambapo mabasi hayo yalikumbana na adhabu hiyo kutokana na kuwakatia abiria tiketi za zamani ambazo sio za kielektroniki zilizopigwa marufuku.

Afisa wa LATRA Mkoa wa Singida Kilua Mbezi baada ya kuyatoza faini mabasi hayo alitoa elimu kwa abiria kuhusu umuhimu na faida ya kupatiwa tiketi za mtandao na kuwa kabla ya kupanda gari nilazima wapatiwe tiketi hizo na kama watawakatalia na kuwapa za zamani ambazo zimepigwa marufuku watoe taarifa kwa kupiga namba ya bure 0800110020.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Miraji Mtaturu akizungumzia baadhi ya faida za mfumo wa ukataji wa tiketi kimtandao (Kielektroniki) alisema ni pamoja na kupunguza mianya ya uvujaji wa mapato kwani abiria ana uhuru wa kukata tiketi basi analolitaka na mmiliki wa basi anaona idadi ya siti zilizokatwa tofauti na zamani na kuwa faida hizo zipo kwa wahusika wote, abiria, wafanyakazi wa mabasi hayo mmiliki na Serikali.

“Tunawapongeza sana LATRA sababu kupitia mfumo wa tiketi mtandao abiria anaweza kukata tiketi akiwa popote bila kulanguliwa na mawakala , lakini pia mfumo huu umerahisisha ukusanyaji wa mapato kwa wamiliki na Serikali sababu unaweza kuona idadi za tiketi moja kwa moja kupitia mfumo,’’ alisema Mtaturu.

Mara baada ya mfumo wa Tiketi Mtandao kuanza kufanya kazi rasmi Julai 01, 2022, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ilifanya mkutano na wadau wa usafirishaji kutathmini utekelezaji wa mfumo huo na kujadili changamoto zinazojitokeza ili kuzifanyia kazi ikiwa ni pamoja na ukataji wa tiketi kimtandao.
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Miraji Mtaturu (kushoto) akizungumza wakati wa kikao hicho.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), CPA. Habib Suluo akizungumza katika kikao kazi na mmoja wa maafisa wa jeshi la polisi kuhusu masuala ya usafirishaji.
Afisa Mfawidhi wa LATRA Mkoa wa Singida, Layla Dafa akizungumza katika moja ya mikutano na wananchi.

No comments:

Powered by Blogger.