LIVE STREAM ADS

Header Ads

Shuhudia Mahafali ya Chuo cha Afya MWACHAS, Serikali yaahidi kukifanyia upanuzi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com 
Serikali imeahidi kusaidia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya upanuzi wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Mwanza (MWACHAS) ili kuongeza uwezo wa chuo hicho kudahili wanafunzi wengi zaidi.

Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Elikana Balandya ametoa ahadi hiyo Agosti 12, 2023 wakati akizungumza kwenye mahafali ya wahitimu wa chuo hicho ngazi ya Stashahada yaliyofanyika katika eneo la Bailor Bugando jijini Mwanza. 

"Kuhusu ujenzi kwenye eneo la chuo lililopo Matale wilayani Magu, nalo nimelichukua na naahidi tutashirikiana na Wizara ya Afya na wadau wengine ili kuhakikisha fedha za ujenzi zinapatikana ili tukipanue chuo chetu" amesema Balandya na kuongeza;

"Mahitaji ya wanafunzi kujiunga na chuo hiki ni makubwa lakini uwezo wa kudahili ni mdogo hivyo kukipanua kwa kujenga majengo mapya itasaidia kudahili wanafunzi wengi zaidi" amesisita Balandya.

Pia Balandya amewahimiza wahitimu wa chuo hicho kwenda kuwahudumia wananchi kwa upendo na ufanisi mkubwa huku wakizingatia maadili ya sekta ya Afya ikiwemo kulinda siri za wagonjwa.

Awali Mkuu wa chuo hicho, Dkt. Hyasinta Jaka amesema kina uhaba wa vyumba vya madarasa na mabweni hatua inayosababisha adha kwa wanafunzi hususani wakati wa mitihani ambapo hulazimika kutumia vyumba vya madarasa ya chuo jirani cha CUHAS Bugando.

"Kupitia mapato ya ndani tumenunua viwanja viwili vyenye ukubwa wa ekari 139 kwa thamani ya shilingi milioni 170 katika eneo la Matale Magu kwa ajili ya kupanua chuo hiki" amesema Dkt. Jaka.

Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu, Hamida Soko ameomba changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa, mabweni na usafiri kutafutiwa ufumbuzi ili kuondoa adha kwa wanafunzi.

"Tumepata ujuzi wa kutosha uliojumuisha mafunzo ya nadharia na vitendo na hivyo kuwa wahitimu bora tunaoweza kujiajiri na kuajiriwa. Sisi ni bidhaa bora inayoweza kutumika katika sekta ya afya kwani hakuna maendeleo bila afya" amesema Soko.

Katika mahafali hayo, wahitimu mbalimbali wametunukiwa vyeti ngazi ya Stashahada katika kozi za afya ikiwemo uuguzi na ukunga, ufamasia, tiba ya viungo na Sayansi ya Taarifa za Afya.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Mgeni rasmi Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Elikana Balandya (kushoto) akimkabidhi cheti mmoja wa wahitimu.
Mgeni rasmi Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Elikana Balandya (kushoto) akimkabidhi cheti mmoja wa wanafunzi wa MWACHAS kwa kufanya vizuri kwenye masomo.
Mgeni rasmi Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Elikana Balandya (kushoto) akionyesha picha ya Mkuu wa Mkoa Mwanza, Amos Makalla ambayo imechorwa na mmoja wa wanafunzi wa MWACHAS.
Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Elikana Balandya akizungumza kwenye mahafali hayo.
Baadhi ya watumishi na wahitimu wa MWACHAS.
Mmoja wa wahitimu, Hamida Iddy Soko akisoma risala kwa niaba ya wahitimu.
Mkuu wa Chuo MWACHAS, Dkt. Hyasinta Jaka akizungumza kwenye mahafali hayo.
Baadhi ya wahitimu wakifurahia wakati wa mahafali hayo.
Uongozi wa Chuo cha MWACHAS ukimuonyesha mgeni rasmi ramani ya eneo la chuo hicho lililopo Matale wilayani Magu.

No comments:

Powered by Blogger.