LIVE STREAM ADS

Header Ads

Profesa Mbarawa aombwa kuruhusu Latra kutoa motisha kwa abiria wanaotoa taarifa za mabasi yanayokwepa kodi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa.


Na Dotto Mwaibale, Singida
Abiria wenye uzalendo na nchi wanaosafiri kwenye mabasi ndani na nje ya nchi wamemuomba Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kuiruhusu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), kutoa motisha kwa wananchi wanaotoa taarifa za mabasi yanayokwepa kukata tiketi za mtandao kwa lengo la kuikosesha Serikali kupata mapato.

Motisha wanayoiomba abiria hao ni ile inayotokana na LATRA baada ya kuyatoza faini mabasi wanayotoa taarifa za kukwepa kulipa kodi kwa njia ya tiketi za kimtandao.

Ombi la abiria hao limekuja ikiwa zimepita siku chache tangu Kamati ya Bunge ya Miundombinu kuipongeza LATRA kwa ufanisi wa kazi ambapo Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, CP Habib Suluo, aliihakikishia kamati hiyo kuwa mamlaka hiyo itaendelea kutekeleza majukumu yake kikamilifu kwa kuboresha shughuli za usafirishaji nchini.

Suluo alitoa ahadi hiyo baada ya Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo ya Bunge, Miraji Mtaturu, kuipongeza LATRA kwa kusimamia mfumo wa utoaji tiketi kwa njia ya mtandao ambao umeanza kupunguza kero kwa abiria.

''Tutaendelea kutekeleza majukumu yetu kwa ukamilifu na kuufanyia kazi ushauri uliotolewa na Kamati ya Bunge ya Miundombinu kwa lengo la kuboresha shughuli za usafirishaji ikiwemo kuendelea kuwatahini madereva ili kuhakikisha abiria wanasafiri kwa usalama'' alisema Suluo wakati akiwasilisha taarifa ya mamlaka hiyo kwa wabunge wa kamati hiyo Agosti 25, 2023.

Mmoja wa abiria hao aliyekuwa amesafiri na basi la Kampuni ya Nyahunge akitokea Dodoma kwenda Singida aliyetoa taarifa kwa Mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo na Afisa Mfawidhi wa LATRA Mkoa wa Singida Layla Dafa baada ya kushuhudia abiria wakikatiwa tiketi zisizo za kielektroniki zilizopigwa marufuku kwa lengo la kuinyima Serikali mapato alisikitishwa na kitendo cha Afisa Habari wa Mamlaka hiyo Salum Pazzy kushindwa kuwasiliana na abiria huyo licha ya CP Suluo kumpa namba ya Mhasibu Mkuu wa LATRA, Samwel Kaenja ili amuunganishe abiria huyo na Afisa Habari huyo kufuatia mabasi manne ya kampuni hiyo kupigwa faini ya Sh. Milioni 1,250,000/- likiwepo basi moja la Kampuni ya Supafeo.

''Nimempa namba yako Afisa Habari wetu Mkuu Salum Pazzy kama ulivyoagizwa na mkurugenzi atakupigia sasa hivi'' alisema Kaenja.

Abiria huyo alisema pamoja na kumpigia simu mara kadhaa na kwa siku tofauti na kumtumia 'link' kwenye namba yake ya WhatSapp zinazoonesha taarifa hiyo ilivyoandikwa kwenye mitandao ya kijamii simu ya afisa habari huyo ilikuwa ikiita wakati wote bila ya kupokelewa jambo ambalo linaonesha haendi na kasi ya utendaji wa kazi wa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbawar na Mkurugenzi wake CP Suluo na kuomba ikiwezekana aondolewa kwenye nafasi hiyo na kuwekwa mtu mwingine kwani anafifisha utendaji kazi wa mamlaka hiyo licha ya mkuu wake kutoa ahadi kwa Bunge ya kuboresha ufanisi wa kazi.

Alisema utendaji kazi wa aina ya Afisa Habari huyo unaweza kuwakatisha tamaa wananchi ya kutoa taarifa za namna hiyo jambo ambalo litaisababishia Serikali kukosa mapato yanayosaidia kutekeleza miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kulipa mishahara ya watumishi akiwemo na afisa huyo.

''Kitengo cha habari na masoko ndio kiunganishi kati ya wananchi na mamlaka hiyo sasa inapofikia hatua ya wahusika kupigiwa simu kwa zaidi ya siku mbili na kwa nyakati tofauti lakini hakuna mapokeo yoyote kinakuwa hakina maana ya kuwepo na hiyo inaonesha kutokuwepo kwa umakini na kufanya kazi kimazoea'' alisema abiria huyo kwa niaba ya wenzake.

Aidha abiria hao wamempongeza Mkurugenzi Mkuu wa LATRA kwa kazi nzuri anayoifanya ndani ya mamlaka hiyo pamoja na Afisa Mfawidhi wa LATRA Mkoa wa Singida, Layla Dafa kwa hatua aliyoichukua ya kutuma Afisa wake Kilua Mbezi kuyafutilia mabasi hayo Stendi Kuu ya Mabasi Mkoa wa Singida Misuna na kubaini kosa hilo na kuyatoza faini ambapo alitumia nafasi hiyo kutoa elimu kwa abiria kuhusu umuhimu na faida ya kupatiwa tiketi za mtandao na kuwa kabla ya kupanda gari nilazima wapatiwe tiketi hizo na kama watapewa za zamani ambazo zimepigwa marufuku watoe taarifa kwa kupiga namba ya bure 0800110020.

Aidha, Mbezi aliwakumbusha wafanyakazi wa mabasi hayo kuendelea kufuata sheria za usafirishaji ili kuepuka adhabu mara watakapobainika kutenda makosa na kuwa jambo hilo lipo ndani ya uwezo wao na kuwa wataendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuwabaini wanaokiuka sheria na kutoa elimu hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), CPA Habib Suluo, akisaini kitabu wakati akiwa katika moja ya matukio yake ya kikazi.

No comments:

Powered by Blogger.