LIVE STREAM ADS

Header Ads

Waajiri watakiwa kuzingatia kima cha mishahara kwa wafanyakazi wa nyumbani

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Waajiri nchini wamekumbushwa kuzingatia tangazo la Serikali No. 687 lililotolewa Novemba 25, 2022 na kuanza kufanya kazi Januari 01, 2023 kuhusu mishahara kwa wafanyakazi wa nyumbani ambapo kima cha chini kwa mfanyakazi anayeishi kwa mwajiri wake ni shilini elfu 60 kwa mwezi.

Tangazo hilo pia linataka mfanyakazi wa nyumbani asiyeishi kwa mwajiri kulipwa shilingi 120,000, anayefanya kazi kwa viongozi mashuhuli wakiwemo wabunge kulipwa shilingi 200,000 na anayefanya kazi kwa wafanyabiashara wakubwa ama viongozi wa kidiplomasia wakiwemo mabalozi kulipwa shilingi 250,000 kila mwezi.

Rai hiyo imetolewa wakati wa mafunzo kwa wanachama wanaounda Mtandao wa Wafanyakazi wa Nyumbani Tanzania (TDWN) kutoka mikoa ya Mwanza, Mara, Morogoro, Pwani na Dar es salaam yaliyofanyika kuanzia Agosti 25- 29, 2023 jijini Mwanza.

"Tunapaza sauti zetu kwa Serikali, jamii na waajiri kuzingatia kima chini cha mshahara kwa wafanyakazi wa nyumbani kwani bado kuna baadhi ya waajiri wanawalipa wafanyakazi wa nyumbani chini ya kima cha chini cha mshahara kilichotangazwa" amesema mshiriki wa mafunzo hayo, Debora Mwageni.

Naye mshiriki mwingine wa mafunzo hayo, Beatrice Johnson amesema ni vyema waajiri wakazingatia kima cha mishahara kilichotangazwa na Serikali ili kuwawezesha wafanyakazi wa nyumbani kujikimu kimaisha.

"Sisi kama mtandao wa wafanyakazi wa nyumbani Tanzania baada ya mafunzo haya tutakwenda kushirikiana na viongozi mbalimbali wakiwemo wa Serikali ili kuwafikia waajiri na kuwaelimisha umuhimu wa kuwalipa wafanyakazi wao wa nyumbani kwa viwango vinavyostahili" amesema Beatrice.

Kwa upande wake Demitila Faustine kutoka shirika la kutetea haki za wafanyakazi wa nyumbani WoteSawa amesema bado kuna changamoto kwa waajiri wengi kuzingatia viwango stahiki kwa wafanyakazi wa nyumbani.

"Tunakwenda kushawishi jamii ibadilike na kuanza kuwalipa wafanyakazi wa nyumbani kwa kuzingatia kima cha chini cha mshahara, pia tutaendelea kuhamasisha waajiri kuingia mikataba ya maandishi na wafanyakazi wa nyumbani" amesema Demitila.

Katika hatua nyingine Demitila ameishukuru Serikali kwa mwitikio mzuri wa kuelekea kuridhia mkataba wa kimataifa No. 189 unaohamasisha kazi za staha kwa wafanyakazi wa nyumbani akisema mkataba huo ukiridhiwa utakuwa mwarobaini wa changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi wa nyumbani.

Washiriki wa mafunzo hayo wamejifunza mada mbalimbali ikiwemo usimamizi wa fedha, uongozi, ufuatiliaji na usimamizi wa miradi, teknolojia, uchechemuzi na sheria zinazowalinda wafanyakazi wa nyumbani pamoja na afya ya uzazi.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Demitila Faustine ambaye ni Msimamizi wa miradi wa miwili kutoka shirika la WoteSawa ambayo ni mradi wa Sauti Yetu, Nguzo ya Mabadiliko unaofadhiliwa na shirika la Women Fund Tanzania na mradi wa kuhamasisha kazi za staha kwa wafanyakazi wa nyumbani unaofadhiliwa na shirika la Voice Global akizungumza wakati wa mafunzo kwa wanachama wa Mtandao wa Wafanyakazi wa Nyumbani Tanzania yaliyofanyika jijini Mwanza kuanzia Agosti 25-29, 2023.
Afisa Mawasiliano kutoka shirika la WoteSawa, Jackline Nyambere akiwasilisha mada kuhusu teknolojia ya mawasiliano wakati wa mafunzo kwa wananchama wa Mtandao wa Wafanyakazi wa Nyumbani Tanzania yaliyofanyika jijini Mwanza.
Washiriki kutoka mikoa ya Mwanza, Mara, Morogoro, Pwani na Dar es salaa ambao wanaunda Mtandao wa Wafanyakazi wa Nyumbani Tanzania wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo ili kuwa na sauti ya pamoja katika kutetea haki za wafanyakazi wa nyumbani. Mafunzo hayo yameandaliwa na shirika la WoteSawa linalosimamia mtandao huo.
SOMA PIA>>> HABARI ZAIDI HAPA

No comments:

Powered by Blogger.