LIVE STREAM ADS

Header Ads

Takukuru Pwani yabaini madudu mchakato wa manunuzi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani Christopher Myava akizungumza katika mkutano na na waandishi wa habari hawapo pichani uliofanyika Agosti 16, 2023 Ofisini kwake Kibaha.



Na Mwandishi Wetu, Kibaha
Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani Christopher Myava amesema kuwa wamegundua kuwa baadhi ya wazabuni wamepewa kazi na Afisa Manunuzi wa Halmashauri pasipo kuomba kazi hizo kwa kupitia mfumo wa manunuzi ya umma yaani TANEPs.

"Hatua hii imesababisha wazabuni kupata kazi bila kufuata taratibu za manunuzi ya umma mfano mzabuni aliyechaguliwa kuleta vifaa vya ujenzi katika shule mpya ya Sekondari ya Kata ya Shungubweni iliyoko Wilaya ya Mkuranga hakuomba kazi hiyo kwenye mfumo wa wa TANEPs na badala yake amepatiwa zabuni na Afisa Manunuzi wa Halmashauri kinyume cha utaratibu" amesema Myava.

"TAKUKURU Mkoa wa Pwani tumegundua uwepo wa Kamati hewa kwa baadhi ya miradi inayosimamiwa na Halmashauri jambo limesababisha uwepo wa mianya ya rushwa katika malipo yanayofanyika, jamii kutokuwa na umiliki wa miradi hiyo kutokana na kutokusbirikishwa katika utekelezaji wake, mfano ujenzi wa Kituo cha Afya Kisiju hamii haikushirikishwa kabisa katika yaimamizi na utekelezaji wa mradi huu" amesema Myava.

Aidha TAKUKURU wamebaini mianya ya ukosefu wa uaminifu katika kukusanya ushuru na usimamizi uendeshaji wa soko la Mnarani Halmashauri ya Mji Kibaha imebainika kuwa wakusanyaji wa ushuru kutotoa risiti za mashine ya POS baada ya wafanyabiashara kufanya malipo kwa kisingizio cha cha ubovu wa mashine au mashine kutokuwa na 'Charge' jambo ambalo limesababisha wakusanyaji kutumia fedha hizo kwa matumizi yao binafsi na kusababisha kukosekana kumbukumbu za wafanyabiashara waliofanya malipo yao" amesema Kamanda Myava.

"Upotevu wa mapato ya maegesho unasababishwa na utendaji mdogo wa wakusanya mapato ambapo baadhi ya wakusanyaji hutoza viwango tofauti vya ushuru wa malori yanayoegesha sokoni tofauti na viwango vilivyowekwa kwenye sheria ndogo" amesema Kamanda Myava.

Kamanda Myava amesema tayari wamekaa kikao na wadau wa soko la Mnarani na kuweka maazimio moja wapo likiwa kukusanya mashine zote ambazo zinadaiwa kuwa mbovu ili kudhibiti huo mwanya, wafanyabiashara wamepewa elimu ili kuhakikisha wanadai risiti baada ya kufanya malipo ya ada na ushuru na kutakiwa kutoa taarifa pindi wanapoelezwa na wakusanya ushuru kuwa mashine za POS ni mbovu ili kudhibiti upotevu wa mapato yanayokusanywa.

Pia wamekubaliana kutengeneza vibao vitakavyo onesha bei za tozo za maegesho ili kuepusha kutoza viwango tofauti hususani kwa kila lori linapoegeshwa sokoni kwa ajili ya kushusha bidhaa.

Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani Myava amesema hayo leo Agosti 16 alipozungumza na Waandishi wa Habari kwenye Mkutano uliofanyika ofisini kwake Kibaha " Kipindi cha robo ya Aprili hadi Juni 2023,Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Pwani tumeendelea na majukumu yetu katika maeneo ya uzuiaji rushwa, uchunguzi pamoja na uelimishaji" amesema.

Amesema kuwa uchunguzi umefanyika wa tuhuma mbalimbali huku tayari kesi imefunguliwa Mahakamani dhidi ya Afisa Manunuzi wa Halmashauri ya Mkuranga .

Amesema kuwa katika eneo la uzuiaji rushwa wamefanya ufuatiliaji miradi 11 ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi.Bilioni mbili milioni mia tatu na mbili na laki tano hamsini na mia nne ishirini na sita (2,302, 550,426/-) katika sekta za elimu, afya, maji barabara , masoko na amendeleo ya jamii, katika ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi hiyo hakukuwa na mapungufu yaliyobainika katika miradi hiyo iliyofanyiwa ufuatiliaji.

Ili kudhibiti mianya ya rushwa katika Idara za serikali na sekta binafsi tumefanya mikutano ya hadhara 36, semina nane kwa watumishi wa serikali na sekta binafsi imefanyika, maonesho nane yamefanyika, klabu za wapinga rushwa 96 zimeimarishwa kwenye shule za msingi na sekondari na elimu dhidi ya rushwq imetolewa kupitia vipindi bitatu vya redio.

Amesema kuwa idadi ya malalamiko yaliyopokelewa ni 87,malalamiko yanayohusu rushwa 62, yasiyohusu rushwa 25, malalamiko yaliyohamishiwa Idara nyingine 04, yaliyoshauriwa 18 na yaliyofungwa hakuna.

TAKUKURU Mkoa wa Pwani imeweka mikakati yake katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2023 kuwa ni kiendeleza programu ya TAKUKURU Rafiki, kuendelea kufanya ufuatiliaji na chambuzi za mifumo kwa lengo la kuziba mianya ya rushwa itakayobainika kuendelea kukagua utekelezaji wa miradi yote ya maendeleo ndani ya Mkoa wa Pwani.

Kuendelea kuelimisha umma wa watanzania juu ya madhara ya rushwa ili wafahamu nafasi yao katika mapambano dhidi ya rushwa kwa makundi yote katika jamii kuendelea nauchunguzi wa vitendo vya rushwa na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wale watakaobainika kutenda makosa ya rushwa.

Kamanda wa TAKUKURU Pwani Myava ametoa wito na kuwahamasisha wananchi na wadau wote katika Taasisi za serikali na sekta binafsi kuendelea kuunga mkono juhudi za mapambano dhidi ya rushwa kwa kukataa kujihusisha na vitendo vya rushwa, kufuatilia miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao ili thamani ya fedha ya Serikali ionekane.

 Kwa kufanya hivyo miradi ya maendeleo itatekelezwa kwa kiwango kilichokusudiwa na hivyo kuleta maendeleo na huduma bora kwa wananchi, pia wananchi wanaombwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa endapo utavishuhudia au kusikia ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria 'Kuzuia rushwa ni jukumu lako na langu, tutimize wajibu wetu'

No comments:

Powered by Blogger.