LIVE STREAM ADS

Header Ads

Naibu Waziri Mkuu atoa maagizo kwa Wizara ya Ardhi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko (kushoto) akikabidhiwa moja ya vifaa vitakavyotumika katika shughuli za upimaji ardhi nchini, anayemkabidhi ni Balozi wa Korea Kusini nchini, Kim Su Pyo.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko (kulia) akimkabidhi moja ya vifaa vitakavyotumika katika shughuli za upimaji ardhi nchini, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko (kulia) akimkabidhi cheti mmoja wa wakufunzi Kumi waliopata mafunzo ya kurusha ndege zisizo na rubani zitakazotumika katika shughuli za upimaji ardhi nchini.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko akizungumza wakati wa hafla ya kuzindua kituo cha Taifa cha Ubunifu na Mafunzo ya taarifa za kijiografia kwa niaba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
***


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko ameiagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kufanyia kwa ufanisi majukumu yake ya msingi ambayo ni kupanga, kupima na kumilikisha ardhi ili kuondoa migogoro ya ardhi inayotokea nchini na kuifanya Wizara husika kuishughulikia mara kwa mara.

Ameyasema hayo tarehe 09 Septemba, 2023 jijini Dodoma wakati wa hafla ya kuzindua kituo cha Taifa cha Ubunifu na Mafunzo ya taarifa za kijiografia kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mhe.Kassim Majaliwa.

“Kazi za Wizara hii ni tatu, ambazo ni kupanga, kupima na kumilikisha ardhi, sasa tujipime na tujitathmini kama katika sekta yetu ya ardhi kazi hizi tunazifanya kwa ukamilifu wake, lipo wimbi la kuweka tension ya Wizara kutoka kwenye Sheria yake au Ilani ya uchaguzi na kugeuka kuwa Wizara ya utatuzi wa migogoro ya ardhi; kuanzia sasa tuwafanye watanzania wazungumze mipango miji, maendeleo ya makazi na matumizi bora ya ardhi” amesisitiza Dkt. Biteko.

Ameitaka Wizara hiyo pia kushirikiana na Halmashauri zote nchini ili kazi zifanyike kwa ufanano na hivyo kwa pamoja waweze kuondoa urasimu na kuondoa migogoro ya ardhi na hivyo ana imani kuwa Wizara hiyo itamaliza changamoto zilizopo na kuweza kupanga miji ipasavyo na kuimarisha makazi ya watu ili kujenga Tanzania iliyo bora zaidi.

“Wizara hii ni moyo wa shughuli za uchumi hapa nchini, kwani watu wanaofanya shughuli za ujenzi, kilimo, wanaojenga miradi mbalimbali ikiwemo ya gesi asilia, wanategemea Sekta ya Ardhi, pamoja na kazi kubwa iliyofanyika ya kuimarisha sekta hii bado kuna kazi kubwa mbele ya kujiimarisha” amesema Dkt. Biteko

Kuhusu kituo hicho alichokizindua, Dkt. Biteko amesema ni muendelezo wa hatua zinazochukuliwa na Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kuchochea matumizi ya teknolojia katika kuleta maendeleo endelevu na ubunifu hapa nchini.

Amesema kuwa kituo hicho ni muhimu kwani kitaboresha shughuli za upimaji ardhi, uandaaji wa ramani za msingi, ujenzi wa miundombinu, kupanga matumizi bora ardhi pamoja na masuala mengine yanayohusiana na Sekta ya Ardhi. Ametoa wito kwa Wizara na Taasisi zake kupeleka watumishi kwenye kituo hicho ili wapate mafunzo ya ukusanyaji, uchakataji na utumiaji wa taarifa za kijiografia katika kutekeleza majukumu ya taasisi zao.

Ametoa pongezi kwa Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kutoa eneo na jengo kwa ajili ya kuanzisha kituo hicho, pia ameishukuru Serikali ya Korea Kusini kwa kugharamia uanzishaji wa kituo hicho.

Aidha, amewataka wahitimu kutoka Kituo hicho wakafundishe watumishi wengine na wakawe chachu ya mabadiliko ya kiutendaji katika Sekta na kuongeza matumizi ya taarifa za kijiografia nchini.

Hafla hiyo ya uzinduzi wa kituo cha Taifa cha Ubunifu na Mafunzo ya taarifa za kijiografia ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali.

No comments:

Powered by Blogger.