LIVE STREAM ADS

Header Ads

Mradi wa maji Butimba jijini Mwanza kuanza majaribio

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi amesema utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa maji Butimba unakwenda vizuri na kasi inaridhisha.

Amesema hayo Septemba 12, 2023 wakati wa ziara ya Kamati ya Usalama Wilaya Nyamagana iliyolenga kukagua mradi wa maji Butimba akiwa ameambatana na Menejimenti ya MWAUWASA ikiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Neli Msuya.

Ziara hiyo imelenga kujionea maendeleo ya mradi kuelekea siku ya majaribio ya awali ya mradi huo Septemba 15, 2023.

"Niwapongeze MWAUWASA kwa kazi nzuri na kasi hii ya utekelezaji mnayoendelea nayo, niipongeze pia timu iliyoundwa na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kwa ushirikiano huu mnaoutoa kwa MWAUWASA, tuna imani tutapata matokeo chanya" amesema Makilagi.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na usafi wa Mazingira jijini Mwanza (MWAUWASA), Neli Msuya amesema utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 96 na kuongeza kuwa majaribio ya mradi yanatarajiwa kufanyika Septemba 15, 2023 ikiwa ni hatua ya awali kuelekea katika hatua ya ukamilishaji wake.

"Tunakwenda kwa awamu, majaribio haya yatatupa matokeo chanya katika upatikanaji wa huduma ya Maji kwa awamu. Wananchi wataanza kuona mabadiliko kadri siku zinavyokwenda" amesema Msuya.

Mradi wa Maji Butimba unatekelezwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 69 na unaotarajiwa kuzalisha kiasi cha lita milioni 48 kwa siku ukihudumia zaidi ya wakazi 450,000 hatua inayotajwa kuondoa adha ya maji jijini Mwanza.

No comments:

Powered by Blogger.