LIVE STREAM ADS

Header Ads

Prof. Kitila Mkumbo na Dkt. Mwigulu Nchemba wamaliza tofauti zao

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mbunge wa Jimbo la Ubungo mkoani Dar es Salaam, Prof. Kitila Mkumbo ambaye pia ni Waziri wa Mipango na Uwekezaji pamoja na Mbunge wa Iramba Magharibi, Dkt. Mwigulu Nchemba ambaye pia ni Waziri wa Fedha wakiwa wameshikana mikono baada ya kutangaza kumaliza tofauti zao katika hafla ya kumkabidhi Mkandarasi Henan Highway Engineering Group Ltd ya nchini China kazi ya ujenzi wa barabara ya Singida-Sepuka- Ndago, Kiziga iliyofanyika katika eneo la Misigiri Wilaya ya Iramba mkoani Singida.


Na Dotto Mwaibale, Iramba
Wakati kukiwa kumebakiza miaka miwili kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa 2025, Mbunge wa Ubungo jijini Dar es Salaam, Prof. Kitila Mkumbo ambaye ni Waziri wa Mipango na Uwekezaji ametangaza rasmi kumaliza tofauti za kisiasa na Mbunge wa Iramba Magharibi ambaye ni Waziri wa Fedha, Dkt.Mwigulu Nchemba.

Prof. Mkumbo na Dk.Mwigulu ambao wote ni wazaliwa wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida walivutana kugombea ubunge katika jimbo la Iramba Magharibi kabla ya suala hilo kuingiliwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa enzi hizo hayati Dk. John Magufuli ambaye aliamuru Prof. Mkumbo akagombee ubunge Ubungo ili kumuachia Dkt. Mwigulu Iramba Magharibi.

Viongozi hao wamemaliza tofauti zao wakati wa hafla ya kumkabidhi Mkandarasi Henan Highway Engineering Group Ltd ya nchini China kuanza kazi ya ujenzi wa barabara ya Singida-Sepuka- Ndago, Kizaga.

Akizungumza katika hafla hiyo Prof. Mkumbo amesema yeye na Dkt. Mwigulu walishamaliza tofauti zao za kisiasa zilizojitokeza wakati wa uchaguzi mkuu wa 2015.

"Nawaletea tangazo langu kwamba mimi na Mwigulu tulishayamaliza, hatununiani, hatukasilikiani, tunakaa pamoja na tunakula nyama pamoja, sasa nyie wengine msidhani bado hatuelewani mtakuwa vichaa, kwahiyo, hilo limeisha" amesema Prof. Mkumbo huku akishangiliwa na wananchi waliohudhuria hafla hiyo.

Amesema baada ya mvutano wao kisiasa kufikia tamati kilichobaki ni wananchi wa jimbo la Iramba Magharibi kuendelea kumuunga mkono Dkt. Mwigulu kwa ajili ya kuleta maendeleo ya Wilaya ya Iramba.

"Mnafahamu kutoka mwaka 2013 hadi 2020 mimi na mdogo wangu (Dkt. Mwigulu) tulipambana kisiasa lakini tunamshukru Mungu wote tumekuwa wabunge na mawaziri" amesema Prof. Mkumbo na kuongeza kuwa;

"Mimi Mbunge wa Ubungo, jijini Dar es Salaam, kule kwetu kwenye jimbo langu ukija wazaramo watakuimbia kwamba muacheni Kitila abaki alipo na mimi nawaambia leo muacheni Mwigulu abaki pale alipo."

Prof. Mkumbo ametumia hafla hiyo kumshukru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaamini watoto wa Iramba (Dk. Mwigulu na Prof. Mkumbo) kwa kuwateua kuwa mawaziri.

"Mama (Rais Samia Suluhu Hassan) ametuamini watoto wenu wawili katukabidhi wizara nyeti za uchumi wa nchi, kanikabidhi mimi nipange mipango nikimaliza kupanga mipango nimkabidhi Mwigulu Nchemba atoe fedha, mnataka nini?" amehoji Prof. Mkumbo.

Akizungumza baada ya Profesa Mkumbo kutoa maneneo hayo, Dkt. Mwigulu amemshukuru na kueleza kuwa walikwisha maliza tofauti zao siku nyingi kilichobakia ilikuwa ni Mkumbo kuzungumza mbele ya kadamnasi.

"Mimi na huyu ndugu yangu tofauti zetu tulikwisha zimaliza siku nyingi na tumekuwa tukishirikiana kwa mambo mengi na hata hii Shahada ya Udaktari (PhD) niliyonayo ni yeye aliyenishauri niende nikasome" amesema Dkt. Mwigulu huku wananchi wakimshangilia kwa furaha.

Alipopata nafasi ya kuzungumza Mgeni rasmi wa hafla hiyo Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amepongeza hatua hiyo walioichukua viongozi hao na akawataka kufanyakazi kwa bidii kwa maslahi mapana ya wana Iramba na Taifa zima kwa ujumla baada ya kupewa nafasi za juu Serikalini na Rais Samia Suluhu Hassan.
Profesa Kitila Mkumbo akizungumza wakati akitangaza kumaliza tofauti kati yake na Dk. Mwigulu Nchemba.
Mawaziri hao wawili wakikumbatiana na kuonesha furaha baada ya kutangaza kumaliza na kuzika tofauti zao rasmi.
Viongozi wa dini wakiwa wamewainua mikono mawaziri hao baada ya kutangaza kumaliza tofauti zao.

No comments:

Powered by Blogger.