LIVE STREAM ADS

Header Ads

Watoto wamjeruhi baba yao mkoani Lindi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkazi wa Kijiji cha Makangaga, Kata ya Kiranjeranje,Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, Salehe Lihanzi (47) akiwa na majeraha baada ya kushambuliwa na watoto wake wa kufikia.


Na Said Hamdani, Lindi
Mkazi wa Kijiji cha Makangaga Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, Salehe Lihanzi (47) amelazwa Hosptalini akiuguza majeraha aliyoyapata baada ya kukatwa mapanga maeneo mbalimbali ya mwili wake na watoto wa kufikia/ watoto wa mkewe.

Tukio hilo linaelezwa kutekelezwa na vijana hao August 31, 2023 akiwa shambani akilinda mazao yake yasishambuliwe na wanyama waharibifu.

Lihanzi amelazwa katika Hosptali ya Sokoine mkoani Lindi na amewataja watoto hao kuwa ni Ally Halfani na Hassani Mbulula.

Amesema siku hiyo akiwa shambani akilinda mazao yasiliwe na wanyama waharibifu alifuatwa na vijana hao wakiwa na mapanga na fimbo mikononi mwao.

Lihanzi amesema baada ya kufika mahali aliposimama alikatwa panga mguu na mkono wa kulia na mtoto mkubwa Ally Halfani huku mdogo wake Hasani akimpiga na fimbo kichwani.

Ametaja sababu ya yote hayo ni kuwataka watoto hao kurejesha vitu walivyochukuwa kikiwemo kitanda cha mbao chenye ukubwa wa futi 5 kwa 6.

Amesema licha ya kuwaeleza kurejesha vitu hiyo, suala hilo alilifikisha kwa mama wa watoto hao Ashura Mbunda ambaye ni mke wake na kwa bibi yao Zaria Omari ambapo walikubali kuvirudisha.

Amesema ndipo August 30, 2023 saa 7:00 mchana akiwa shambani vijana hao walimfuata na kuanza kumshambuli na kumsababishia maumivu makali.

Mkulima huyo amesema baada ya watoto hao kumfanyia ukatili huo waliondoka kuelekea Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji na kueleza kule walicho mfanyia.

"Nilipowaona wanakuja sikuwa na hofu nao wala kudhani wanakuja kundhuru"amesema Lihanzi.

Lihanzi amesema mtu wa kwanza kufika eneo la tukio ni mama mkwe wake Zaria Omari na kumuomba aende kijijini kuwapa taarifa ndugu zake kwa kile kilichomkuta.

Mkulima huyo amesema baada ya ndugu kufika eneo hilo walimchukua na kumpeleka Zahanati ya Kiranjeranje, lakini kutokana na uzito wa tatizo wakalazimika kumpeleka Hosptali ya Mkoa Sokoine iliyopo mjini Lindi.

Amesema tayari askari polisi wamefika Hosptali kuchukuwa maelezo yake kwa ajili ya ya kuyafanyia kazi.

Mganga Mfawidhi Hosptali ya Sokoine mkoani Lindi, Alexander Makalla amethibitisha kumpokea mgonjwa huyo August 30, 2023 saa 2:00 usiku.

Makalla amesema mgonjwa huyo ameshambuliwa na kitu chenye ncha kali mguuni na mkono wa kulia na kichwani na hali yake inaendelea vizuri kutokana na huduma za matibabu anayoyapata

"Mteja wetu amejeruhiwa mguu na mkono wa kulia na kichwsni" amesema Makalla.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Pili Mande amekiri kuwa na taàrifa hiyo na kueleza wanaendelea kuifanyia kazi.

No comments:

Powered by Blogger.