LIVE STREAM ADS

Header Ads

Waislam Singida wasaka bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa msikiti

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro akizungumza na Waislam wa Kata ya Mtinko wakati wa harambee ya ujenzi wa msikiti iliyofanyika Septemba 03, 2023.


Na Dotto Mwaibale, Singida
Wadau mbalimbali wameombwa kuchangia ujenzi wa Msikiti wa Jaamigh uliopo Kata ya Mtinko Wilaya ya Singida, mkoani Singida ambapo jumla ya Sh. Bilioni 1.8 zinahitajika kwa ajili ya ujenzi wa msikiti huo.

Katibu wa kamati ya ujenzi wa msikiti huo, Abdallah Rajab akizungumza wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa msikiti huo mbele ya Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro amesema hadi kukamilika kwa ujenzi huo Sh.Bilioni 1.8 zinahitajika.

Rajab amesema msikiti wa awali ambao ulijulikana kama Msikiti wa Ijumaa Mtinko ulijengwa mwaka 1949 ukiwa na uwezo wa kuhudumia waumini 100 kwa wakati mmoja.

Amesema kutokana na ongezeko la waumini msikiti huo ulipanuliwa mwaka 1990 na kuwa na uwezo wa kuwahudumia waumini 300 na unatumika hadi hivi leo.

Rajab amesema kutokana na ongezeko la waumini na kuanza kuswalia nje mwaka 2018 ndipo walipopata wazo la kuanzisha ujenzi wa msikiti wa sasa wa ghorofa ambao ujenzi wake ulianza mwaka 2019.

''Ujenzi upo hatua ya kusuka bimu kwenye msingi na ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuhudumia waumini 1000 kwa wakati mmoja,'' alisema Rajab.

Amesema msikiti huo utakuwa na huduma za ofisi ya utawala, madrasa, vibanda vya biashara na huduma ya vyoo.

Amesema mahitaji makubwa ya hivi sasa ya ujenzi huo ni mchanga, saruji na nondo na kuwa katika hatua hiyo waliyoifikia ya ujenzi zimetumika Sh.Milioni 28,059,300 fedha zilizotokana na sadaka za waumini na wadau wengine mbalimbali na kuwa kwenye akaunti yao wana Shilingi Milioni tatu.

Baada ya kutolewa kwa taarifa hiyo iliyoandaliwa na uongozi wa msikiti wakishirikiana na kamati ya bodi ya msikiti, Jumuiya ya Wanawake wa Wakiislam (JUWAKITA), wa kata hiyo na kamati ya ujenzi ilifanyika harambee ambapo zilipatikana zaidi ya Sh.Milioni 3.7.

Katika kuongeza nguvu ya kupatikana kwa fedha za ujenzi wa msikiti huo Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro anatarajia kufanya harambee nyingine hivi karibuni katika tarehe itakayo pangwa ambayo itawashirikisha wadau na viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya Mkoa wa Singida.

Kamati ya ujenzi wa msikiti huo inawaomba wadau mbalimbali kusaidia ujenzi huo na kwa mtu yeyote, wafanyabiashara, taasisi watakaokuwa tayari kuchangia chochote walichonacho iwe saruji, kokoto, mchanga na vifaa vingine vya ujenzi na kama ni fedha wanaweza kuweka katika akaunti namba 0152737109500 Benki ya CRDB Mtinko Masjid au wanaweza kuwasiliana na Mtunza fedha wa msikiti huo Said Salim Mdimi kwa namba ya simu 0788778591 kwani kutoa ni moyo na si utajiri.
Katibu wa Baraza la Masheikh Mkoa wa Singida, Said Ally Mang'ola akizungumza kwenye harambee hiyo.
Sheikh wa Kata ya Mtingo, Jumanne Ramadhan akichangia jambo wakati wa harambee hiyo.
Mwalimu wa Dini, Sheikh Isihaka Hassan akizungumza kwenye harambee hiyo.
Kikongwe Hadija Mandi akiwahamasisha Waislam kuchangia ujenzi wa msikiti huo.
Wazee wakiwa kwenye harambee hiyo.
Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro (katikati) akizungumza wakati akikagua ujenzi wa msikiti huo.
Muonekano wa ujenzi wa msikiti huo.
Kiongozi wa Kamati ya Wanawake wa Kiislam wa kata hiyo, Hawa Ayubu, akiongoza uhamasishaji wa kuchangia ujenzi huo.
Wakina mama wakiwa kwenye harambee hiyo.
Harambee hiyo ikiendelea.
Wakina mama wakichangia katika harambee hiyo.

No comments:

Powered by Blogger.