LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wafanyakazi NMB Kanda ya Ziwa wahitimisha kwa kishindo Wiki ya Huduma kwa Wateja

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Katika kuhitimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja Duniani, Benki ya NMB Kanda ya Ziwa imezikutanisha timu za volleyball, kuvuta kamba, netiball na mpira wa miguu kutoka mikoa ya Mwanza na Mara ili kuimarisha afya za wafanyakazi na kuendelea kutoa huduma zilizo bora zaidi.

Mitanange hiyo imepigwa katika viwanja vya Chuo cha Ualimu Bunda mkoani Mara ambapo Mkoa wa Mwanza umeibuka mabingwa katika michezo mitatu ambayo ni kuvuta kamba, netball na volleyball huku Mkoa wa Mara ukiibuka kifua mbele kwenye mpira wa miguu.

Timu ya NMB Mkoa wa Mwanza ya kuvuta kamba imeibuka mabingwa baada ya kuishinda timu ya Mkoa wa Mara mara kwa ushindi wa mbili mtawalia, nayo ya volleyball ikiibugiza ya Mkoa wa Mara kwa seti 3:0, huku NMB ya netball Mkoa wa Mwanza ikiifunga timu ya NMB netball Mara kwa magoli 16:13.

Katika kipute cha mpira wa miguu timu ya NMB Mwanza ikaondoka kichwa chini dhidi ya ile ya Mara kwa kubugizwa goli 2:1.

Akizungumza katika michuano hiyo, Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa- Dickson Richard amesema lengo ni kuimarisha umoja, mahusiano na ukaribu miongoni mwa wafanyakazi huku wakiongeza utoaji huduma bora kwa wateja.

"Tumekutana ili kubadilishana mawazo na kufurahi huku tukiziweka afya zetu imara ili tutakaporudi kutoa huduma tuweze kuwa vizuri, tukumbuke michezo inaimarisha afya zetu na kujenga umoja baina yetu" amesema Richard.

Wiki ya Huduma kwa Wateja huadhimishwa kila mwaka wiki ya kwanza ya mwezi Oktoba na kuwaleta pamoja watoa huduma pamoja na wateja, kuimarisha mahusiano na kutambua mchango wa pande zote mbili.
Tazama picha mbalimbali hapa chini.

No comments:

Powered by Blogger.