LIVE STREAM ADS

Header Ads

MWANZA: Wavuvi waanza kunufaika na mradi wa nishati ya jua

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Teknolojia mpya ya ukaushaji dagaa kwa kutumia mitambo ya nishati ya umeme wa jua imetajwa kuwa mwarobaini wa kukabiliana na changamoto ya upotevu wa dagaa na hivyo kuongeza tija kwa wavuvi na wachuuzi mkoani Mwanza.

Teknolojia hiyo imebuniwa na kampuni ya Millenium Engineers ya jijini Mwanza inayotekeleza mradi wa ukaushaji na uchakataji dagaa kwa kutumia nishati ya jua katika mwalo wa Kayenze Ndogo wilayani Ilemela na kisiwa cha Kasalazi wilayani Sengerema.

Pia mradi huo unelenga kuzalisha na kusambaza taa za sola zenye mwanga wa kutosha kwa shughuli za uvuvi na hivyo wavuvi kuondokana na taa za karabai na betrii za asidi ambazo si rafiki kwa mazingira na viumbe hai.

Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Millenium Engineers, Mhandisi Diana Mbogo amesema; “tumeleta mitambo ya kwanza Afrika Mashariki kwa ajili ya kukaushia dagaa kwa kutumia nishati jadidifu. Hii itasaidia kupunguza upotevu wa dagaa zinazooza hususani nyakati za mvua kutokana na ukaushaji wa kutumia chanja”.

Akikagua utekelezaji wa mradi huo katika mwalo wa Kayenze Ndogo wilayani Ilemeka, Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu REA, Mhandisi Advera Mwijage amesema Serikali imechangia asilimia 30 (milioni 560) ya utekelezaji wa wa mradi huo ili kuhimiza matumizi ya nishati safi na salama katika kuinua uchumi wa wananchi na taifa.

“REA tunampongeza mwekezaji wa mradi huu na tunawakaribisha wawekezaji wengine maana uvuvi uko maeneo mbalimbali ikiwemo Mara na Kagera. Mitambo hii ina uwezo wa kukausha dagaa wengi kwa muda mfupi na hivyo kuleta tija kwa wananchi” amesema Mhandisi Mwijage.

Baadhi ya wachuuzi katika mwalo wa Kayenze Ndogo akiwemo Agness Selestine na Latifa Buchoji wamesema ukaushaji dagaa kwa kutumia nishati ya jua umewaondolea adha hasa wakati wa mvua na sasa dagaa zinakauka kwa ubora zaidi.

Kwa upande wake Frank Faustine ambaye ni mvuvi wa dagaa katika mwalo huo kwa zaidi ya miaka 15 amewahimiza wavuvi wenzake kuachana na uvuvi wa kutumia taa za karabai na kugeukia matumizi ya taa za sola kwani zina mwanga wa kutosha unaochochea mavuno zaidi ya dalai.

Mradi wa taa na ukaushaji dagaa kwa kutumia nishaji jua unatekelezwa na kampuni ya Millenium Engineers ya jijini Mwanza kwa thamani ya shilingi bilioni 1.2 ukifadhili wa wakala wa nishati vijijini REA, taasisi ya EEP Africa na STICHTING DOEN.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Millenium Engineers, Mhandisi Diana Mbogo akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mradi wa ukaushaji dagaa kwa kutumia nishaji ya umeme jua katika mwalo wa Kayenze Ndogo wilayani Ilemela.
Wanahabari wakifanya mahojiano na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Millenium Engineers, Mhandisi Diana Mbogo.
Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu REA, Mhandisi Advera Mwijage akizungumzia umuhimu wa mradi huo katika kuinua uchumi wa wananchi na taifa.
Wanahabari wakifanya mahijiano na Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu REA, Mhandisi Advera Mwijage (kulia).
Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu REA, Mhandisi Advera Mwijage akijionea taa za sola zinazokubalika kwa matumizi ya uvuvi zikiwa zinachajiwa.
Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Millenium Engineers, Mhandisi Diana Mbogo akishuhudia taa za sola zikiwa zinachajiwa kwa ajili ya matumizi ya uvuvi.
Mkurugenzi wa Fedha kampauni ya Millenium Engineers, Victoria Japhet akijionea taa za sola zikichajiwa kwa ajili ya matumizi ya uvuvi.
Mmoja wa wavuvi katika mwalo wa Kayenze Ndogo, Frank Faustine akieleza umuhimu wa taa za sola katika shughuli za uvuvi.
Wavuvi katika mwalo wa Kayenze Ndogo wilayani Ilemela wakiwa kwenye maandalizi ya kuelekea kwenye shughuli za uvuvi katika Ziwa Victoria.
Mchuuzi wa dagaaa, Agnes Selestine akikausha dagaa kwenye mitambo ya ukaushaji dagaa inayotumia nishaji ya jua.
Mchuuzi wa dagaa katika mwalo wa Kayenze Ndogo, Latifa Buchoji akianika dagaa kwenye ndani ya mtambo wa ukaushaji kwa kutumia nishaji ya jua.
Mwonekano wa mitambo ya kukaushia dagaa kwa kutumia nishati ya jua katika mwalo wa Kayenze Ndogo wilayani Ilemela.
Tazama BMG TV hapa chini
PIA SOMA>>> HABARI ZAIDI HAPA

No comments:

Powered by Blogger.