LIVE STREAM ADS

Header Ads

Kamati ya PAC yatua Singida

   

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC),  Japhet Hasunga  akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati kamati hiyo ilipotembelea na kukagua ujenzi wa mradi wa umeme wa Backbone Transmission Investment Project (BTIP), mkoani Singida Novemba 13, 2023 unaosimamiwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)

.................................................

 

Na Dotto Mwaibale, Singida

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti Japhet Hasunga imeridhishwa na hatua iliyochuliwa na Seriakali ya kutumia fedha zake za ndani kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kupokea, kupoza na kusafirisha umeme mkubwa cha Shinyanga kupitia mradi wa Backbone Transmission Investment Project (BTIP), unaosimamiwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)

Hasunga alitoa pongezi hizo wakati kamati hiyo ilipotembelea na kukagua mradi huo mkoani Singida  Novemba 12, 2023 ambao ulisimama utekelezaji wake kutokana na changamoto kadhaa.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Hasunga alisema kamati hiyo imefanya ziara hiyo ili kujiridhisha na utekelezaji wa mradi huo  ambao unahusisha kuviongezea uwezo vituo vya kupokea na kupoza umeme mkubwa katika mikoa ya Iringa, Singida, Dodoma na Shinyanga kutoka umeme mkubwa wa Kilovoti 220 kwenda umeme mkubwa wa kilovoti 400.

Alisema lengo la mradi huo ni kuunganisha nchi ya Tanzania na nchi ya Kenya ambao utaenda hadi Ethiopia na pia kuunganisha nchi ya Tanzania na Zambia yaani nchi za Kusini mwa Afrika.

"Mwaka jana tulikuja hapa lakini tulipata maelezo kiundani tuliona kulikuwa na changamoto katika utekelezaji wa huu mradi na changamoto kubwa zilikuwa mbili ya kwanza ni kujitoa kwa baadhi ya wafadhili ambao walikuwa wameahidi kutoa fedha hivyo kuathiri mradi huo na kushindwa kukamilika," alisema Hasunga.

Hasunga aliongeza kuwa wakati wafadhili hao wakijitoa tayari Serikali ilikuwa imekwisha tumia dola za Kimarekani zaidi ya Milioni 400 kujenga miundombinu mbalimbali hadi nchini Kenya.

Alisema hiyo ilikuwa ni changamoto ya kwanza lakini changamoto ya pili ilikuwa kituo cha kupozea umeme cha Shinyanga kisingeweza kujengwa baada ya wafadhili hao kujitoa pamoja na kituo cha Iringa ambacho kingeunganisha hadi Tunduma mkoani Mbeya.

Hasunga alisema kutokana na jambo hilo kamati hiyo iliona zile fedha zilizotolewa mara ya kwanza na kujenga miundombinu hiyo ya Shinyanga, Iringa na ile ya Tunduma kama isingekamilika zingeonekana hazina thamani kwa sababu ya kutofiKIwa kwa malengo yaliyokusudiwa.

  " Leo tumekuja kujiridhisha kuona maendeleo ya  utekelezaji wa mradi huu na wote tumeshuhudia na kuelezwa kuwa Serikali imeamua kujenga kituo cha Shinyanga kwa fedha za ndani ili kuhakikisha mikoa ya Kanda ya Ziwa inaunganishwa katika suala hili la nishati iliyotimilifu jambo ambalo tumelifurahia," alisema Hasunga.

Alisema jambo la pili ni mradi wa TAZA kutoka Iringa hadi Zambia nao upo katika hatua za manunuzi ya kumpata mkandarasi ambapo ukikamilika utaunganisha mikoa ya Kusini Magharibi ambayo ni Songwe, Rukwa, Katavi , Kigoma na kuunganisha Nyakanazi hatua ambazo kamati hiyo ilitaka ipate maelezo ya kina namna gani Serikali imejipanga kutekeleza jambo hilo na wao wameziona jitihada zilizochuliwa hivyo wanaipongeza.

Hasunga alisema watafuatilia kwa karibu kuona mradi huo una kamilika kwa muda uliopangwa ili watanzania waweze kuona manufaa ya miradi hiyo.

Kamati hiyo imetoa ushauri kwa Serikali kukamilisha miradi hiyo kwa wakati kwani imejifunza miradi mingi inachukua muda mrefu tofauti na ile iliyokubalika mara ya kwanza na hivyo kusababisha ongezeko la gharama kubwa.

Akitoa taarifa mbele ya kamati hiyo Mratibu wa mradi huo wa BTIP, Mhandisi Peter Kigadye alisema mradi huo ulianzishwa mwaka 2014 baada ya marais wa Kenya, Tanzania na Zambia kukaa pamoja na kuzungumza masuala mbalimbali na mahusiano ya  nishati hiyo na namna ya kuuziana umeme kutokana na kila nchi kuwa na gharama na vyanzo tofauti katika nchi za Afrika Mashariki.

Mhandisi Kigadye alisema katika kikao hicho Kenya na Zambia wakawa wameungana katika jambo hilo na kila nchi ilitakiwa ijenge miundombinu kwa gharama zake ambapo wakenya walitengeneza miundombinu na kuiunganisha na Ethiopia na Tanzania kuunganisha na nchi zote za Kaskazini.

Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo, Mhandisi Dkt. Cosmas Masawe akizungumza kwa niaba ya mwenyekiti huyo , aliishukuru kamati hiyo kwa kutembelea na kuona utekelezaji wa mradi huo.

Aidha, aliomba kamati hiyo wanapotekeleza miradi mbalimbali Taasisi nyingine za Serikali kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ziwe zinawaondolea kodi na ushuru mbalimbali wakati wa kusafirisha vifaa vyao na kuwa  mara nyingi mchakato wake umekuwa ukichukua muda mwingi na kujikuta wakitekeleza kazi zao nje ya muda na kwa hasara wakati kazi inayofanywa ni ya serikali.

Mhandisi Masawe alitolea mfano nchi ya Kenya taasisi nyingine ya Serikali inapotekeleza mradi umetengenezwa utaratibu wakutozitoza ushuru kwa kuzingatia kuwa mradi husika upo chini ya Serikali.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Japhet Hasunga alipokea ombi hilo na kuahidi kulifanyia kazi kwa kushirikisha wahusika na taasisi zingine ilikuona namna bora ya kulizungumzia kwani miradi hiyo inayotekelezwa ni ya Serikali kwa ajili ya wananchi hivyo kuna kila sababu ya kuviondoa vikwazo hivyo kwa maslahi ya nchi na kuwa taasisi hizo zinapaswa kufanya kazi kama timu.. 

Mratibu wa mradi huo wa BTIP, Mhandisi Peter Kigadye , akitoa taarifa mbele ya kamati hiyo ya PAC.
Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco, Mhandisi Dkt. Cosmas Masawe, akizungumzia mradi huo.
Mjumbe wa kamati hiyo Joseph Kakunda, akizungumza.
Mjumbe wa kamati hiyo, Geoffrye Mwambe, akisisitiza jambo wakati kamati hiyo ilipotembea mradi huo.
Mjumbe wa Kamati hiyo, Ester Matiku akizungumza kwenye kikao hicho.


Mjumbe wa kamati hiyo, Mhandisi  Isack Kamwelwe akisisitiza jambo katika ziara hiyo.
Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Japhet Hasunga (wa pili kushoto) akiwa na wajumbe wa kamati hiyo wakati wa ukaguzi wa mradi huo. 
Aliyekuwa Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida Mhandisi Florence Mwakasege akijitambulisha mbele ya kamati hiyo. Mwagasege amehamishiwa Tanesco Mkoa wa Kinondoni.
Meneja mpya wa Tanesco Mkoa wa Singida,  Mhandisi Mwamvita Ally akijitambulisha mbele ya kamati hiyo
Wajumbe wa kamati ya PAC wakipokea taarifa ya mradi huo.
Baadhi ya wafanyakazi wa Tanesco Mkoa wa Singida wakiwa kwenye kikao cha utoaji taarifa ya mradi huo.
Muonekano wa kituo cha kupozea na usambaji umeme kilichopo Mkoa wa Singida.
Meneja Miradi vituo vya kupoza umeme kwa miradi ya Zambia, Tanzania na Kenya (ZTK), Timothy Mgaya,  akitoa maelezo ya mradi huo.

No comments:

Powered by Blogger.