LIVE STREAM ADS

Header Ads

Maafisa Tarafa, Watendaji Kata watakiwa kufanya kazi kwa ushirikiano

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Muragili ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa Peter Serukamba, akifungua mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo Watendaji wa Kata na Maafisa Tarafa wa Mkoa wa Singida yaliyoandaliwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mtaa (TAMISEMI) yaliyoanza Novemba 23, 2023.


Na Dotto Mwaibale, Singida
Watendaji wa Kata na Maafisa Tarafa wa Mkoa wa Singida wametakiwa kufanya kazi kama timu ili kuondoa misuguano isiyo ya lazima wakati wa utendaji wa kazi za kuwahudumia wananchi kwenye maeneo yao.

Ombi hilo limetolewa na Mhadhiri kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo kilichopo Dodoma, Paul Faty wakati akitoa mada kwenye mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo maafisa hao yaliyoandaliwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mtaa (TAMISEMI) yaliyoanza leo Novemba 23, 2023.

Faty alisema mara nyingi kumekuwa kukitokea muingiliano katika utendaji wa kazi kwa maafisa hao na kusababisha kushindwa kufanya kazi ipasavyo za kuwahudumia wananchi kutokana na sababu mbalimbali.

“Kufanya kazi kama timu na kushirikishana kutawafanya muweze kuwahudumia wananchi vizuri katika maeneo yenu kwa kusimamia utekelezaji wa sera, sheria kanuni na miongozo ya Serikali” alisema Faty.

Aidha Fati alisema kuwa moja ya majukumu wanayopaswa kuyafanya ni kuwasikiliza wananchi na kutatua kero zao kwani wao ndio waliopewa dhamana ya kuonana nao moja ka moja na ni kiunganishi kati yao na Serikali.

Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Muragili ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa Peter Serukamba kufungua mafunzo hayo alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwaongezea ujuzi na maarifa wakati wa kutekeleza majukumu yao ili kupunguza kama siyo kuziondoa kabisa changamoto wanapo wahudumia wananchi na kuimarisha mahusiano baina yao na Serikali.

Mragili aliwakumbusha baadhi ya majukumu yao maafisa Tarafa na watendaji hao wa kata kuwa ni pamoja na kumwakilisha na kumsaidia mkuu wa wilaya katika utekelezaji wa shughuli za Serikali kuu na Taifa, kuhamasisha wananchi kushiriki shughuli za maendeleo kwenye Tarafa zao na kuwa kiungo cha wananchi na kata husika.

Mambo mengine aliyowakumbusha ni kushughulikia malalamiko ya wananchi katika Tarafa, kufuatilia na kuhimiza utekelezaji wa Sera za Serikali katika maeneo yao na kuhakikisha zinatekelezwa ipasavyo, kushiriki katika kupanga miradi ya maendeleo katika kata na kuwa mtendaji mkuu wa kata ni kiungo wa idara zote katika kata.

Alitaja mambo mengine aliyowakumbusha maafisa hao kuwa ni kuandaa mpango kazi wa maendeleo katika kata na kuhuwasilisha kwa mkurugenzi na Afisa Tarafa, kutafsiri na kusimamia utekelezaji wa sera, sheria kanuni na miongozo ya Serikali katika kata, mratibu wa upangaji wa mipango shirikishi ya maendeleo katika kata na kupokea na kutatua malalamiko na matatizo ya wananchi katika kata.

Naye Naibu Mkuu wa chuo hicho Dkt. Michael Msendekwa akizungumza kwa niaba ya mkuu wa chuo hicho, alisema chuo hicho kilianzishwa kwa sheria namba 26 sura 396 lengo kubwa likiwa ni kuziwezesha mamlaka za Serikali za Mitaa ziweze kutekeleza majukumu yake.

Alisema chuo hicho kimekuwa kikitoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu yenye programu sita kuanzia ngazi ya cheti na sasa wanatoa shahada ya kwanza na kueleza kuwa kimejipanga kuiwezesha Serikali za Mitaa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Idara ya TAMISEMI, Hamisi Mkanga alisema mafunzo hayo yalianzishwa kwa ajili ya kuwajengea uwezo maafisa Tarafa na watendaji kuanzia ngazi ya chini kabisa ndipo walipo omba chuo hicho kiwatafutie mada ambazo zitaendana na maafisa hao kwa kukumbushana mambo mbalimbali.

Alisema mafunzo hayo ya siku mbili yatawashirikisha walengwa hao katika mada mbalimbali ambazo wataweza kuzifanyia kazi.

Alisema mada ambazo watafundishwa ni takribani 13 na kuwa mafunzo hayo kwa awamu ya kwanza yalifanyika mikoa ya Katavi, Rukwa, Njombe pamoja na Songwe na kwa awamu hii ya pili kuna mikoa ya Singida, Shinyanga, Tabora, Pwani, Dar es Salaam, Lindi pamoja na Mtwara na kuwa wataendelea kutoa mafunzo hayo kwenye mikoa mingine kulingana na jinsi watakavyokuwa wanapata fedha.

Mkanga alitumia nafasi hiyo kuwasihi washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia mada wanazofundishwa kwani ni za muhimu sana.

Baadhi ya mada zilizofundishwa kwa siku ya kwanza ni Uongozi na Utawala, Sera na Sheria zinazosimamia Tawala za Mikoa na MSM, Maadili ya Utumishi wa Umma, Majukumu ya Watendaji wa Kata na Maafisa Tarafa, Muundo, mfumo wa uwajibikaji na mawasiliano Serikalini na mafunzo ya awali ya MUKI.

Mada zitakazo fundishwa siku ya pili ni Upangaji mipango na Bajeti, Usimamizi na Udhibiti wa Fedha, Usimamizi na Ununuzi wa Umma,, Usimamizi wa Miradi, Ushughulikiaji Malalamiko (kero za wananchi), Kuhabarisha Wananchi Mafanikio ya Serikali, Mfumo wa Kujifunza Kielektroniki (MUKI) na Utunzaji wa Siri za Serikali.
Naibu Mkuu wa Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo Dkt. Michael Msendekwa akizungumza kwa niaba ya mkuu wa chuo hicho wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya TAMISEMI, Hamisi Mkanga akitoa taarifa ya mafunzo hayo.
Mhadhiri kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo kiliichopo Dodoma, Paul Faty wakati akitoa mada kwenye mafunzo hayo hayo.
Mhadhiri Petro Nziku kutoka Chuo cha Serikali ya Mitaa Hombolo akitoa mada kuhusu Sera na Sheria zinazosimamia Tawala za Mikoa na MSM.
Mhadhiri kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma, (TPSC), Dk. Hosea George akiwajibika.
Mafunzo yakiendelea.
Watendaji Kata na Maafisa Tarafa wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea.
Washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa.
Taswira ya mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea.
Watendaji Kata na Maafisa Tarafa wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Picha ya pamoja na viongozi meza kuu.
Picha ya pamoja.
Picha ya pamoja.
Picha ya pamoja.

No comments:

Powered by Blogger.