LIVE STREAM ADS

Header Ads

DC Makilagi aongoza zoezi la kupanda miti, kuadhimisha miaka 62 ya Uhuru

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Amina Makilagi akitoa elimu kwa wanafunzi kuhusu umuhimu wa kupata miti na kuitunza ili kuhifadhi mazingira.



Na Hellen Mtereko, Mwanza
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza,  Amina Makilagi amewaongoza wananchi, walimu, wanafunzi na watumishi mbalimbali kwenye zoezi la kupanda miti katika shule za msingi za Bulale na Makilagi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Tanganyika/ Tanzania Bara.

Zoezi hilo la upandaji miti limefanyika Ijumaa Desemba 08, 2024 katika Kata ya Buhongwa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza.

Makilagi amesema wamepokea miche ya miti zaidi ya 700 kutoka kwa wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS) kwa ajili ya kuipanda katika shule hizo pamoja na pembezoni mwa barabara inayotoka Buhongwa kwenda Bulale.

"Sherehe hizi za Uhuru zimeendana na shughuli mbalimbali katika Wilaya yetu ikiwemo kufanya usafi na kupanda miti ikiwa ni kuenzi Uhuru wa Taifa letu kwani bila usafi, hata uhuru tusingeweza kuupata hivyo kila mtu ana wajibu wa kuilinda na kuitunza miti hatua itakayosaidia kuepukana na janga la ukame" amesema Makilagi.

Naye Emmanuel Mgimwa ambaye ni Mhifadhi Misitu TFS Wilaya ya Nyamagana, amesema wameshiriki kuhamasisha upandaji wa miti ya matunda 200, kivuli 200 pamoja na miti ya urembo 300.

"Sisi kama wakala tunatoa rai kwa wananchi waendelee kuitunza vizuri miti hii tuliyoipanda kwa kuiepusha na changamoto za mifugo" amesema Mgimwa.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Makilagi, George Kadago amesema atashirikiana na walimu wenzake kuitunza miti iliyopo na iliyopandwa ili mazingira ya shule yazidi kuwa rafiki.

Awali akizungumza kwenye zoezi hilo la upandaji miti, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Peter Juma amewaasa wananchi kuacha tabia ya kukata miti ovyo na badala yake wawe na utamaduni wa kupanda miti ikiwemo ya matunda ili kuhifadhi mazingira na kuondokana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi akishiriki zoezi la kupanda miti katika shule ya msingi Bulale ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 62 ya Tanganyika.
Mmoja wa wanafunzi akishiriki zoezi la kupanda miti.
Mkazi wa Bulale, Agness Erasto akishiriki zoezi la kupanda miti ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Tanganyika. Tanganyika ilipata Uhuru Disemba 09, 1961 na mwaka 1964 ikaungana na Zanbiar na kuzaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wanafunzi wa shule ya msingi Makilagi wakishiriki zoezi la kupanda miti ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika/ Tanzania Bara.

No comments:

Powered by Blogger.