TTB yazindua “Likizo Time” kuhamasisha utalii wa ndani
Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imezindua Kampeni maalum ijulikanayo kama “Likizo Time” ili kuhamasisha watanzania katika kipindi cha likizo ya mapumziko ya Krismas na mwaka mpya 2024 kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Damas Mfugale amesema Kampeni ya “LIKIZO TIME” imebuniwa na TTB kwa kushirikiana na Kampuni maarufu nchini ya burudani ya Tanzania House of Talents (THT) ambapo kumeandaliwa vifurushi (packages) mbalimbali vya utalii.
Amesema lengo kuu la Kampeni hiyo ni kuhamasisha utalii wa ndani ili kuijengea uwezo sekta katika vipindi vyote vya misimu ya utalii na wakati yanapotokea majanga.
“Dhamira yetu kama Serikali ni kuhamasisha watanzania kuanza kutembelea vivutio vyetu katika kipindi cha likizo za mwisho wa mwaka hali hii ikiboreka itasaidia kuwa na misimu mirefu (high season) mwaka mzima pia kipindi cha majanga kama wakati wa uviko maeneo yetu kuendelea kupata wageni” amefafanua Mfugale.
Aidha amesema kampeni hiyo inakwenda kutumia mashindano ya kwenye mitandao na vyombo vya habari ambapo washindi watapata fursa ya kutembelea katika vivutio vya utalii na kukaa kwenye mahoteli ya kitalii.
Amesema kampeni hiyo itachukua wiki nne ambapo inaanza Desemba 02, 2023 hadi Januari 05, 2023 na itahusisha hifadhi za Mikumi, Arusha, Tarangire, Ruaha, Mlima Kilimanjaro na Mlima Meru.
Mfugale amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Tanzania. Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kucheza Filamu ya The Royal Tour ambapo amesema imesaidia kuhamasisha siyo tu watalii nje ya Tanzania kuanza kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini bali pia watalii wa ndani.
Mwakilishi wa THT Kemi Mutahaba ametoa wito kwa watanzania kushiriki kikamilifu katika kampeni hii ili kuchangia kwenye uchumi wa taifa.
Na John Mapepele
No comments: