Mabingwa Tennis duniani waitangazana Tanzania
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki amewaalika wawekezaji kutoka Marekani na duniani kwa ujumla kuja kuwekeza nchini katika sekta ya Utalii na sekta nyingine kwa kuwa Tanzania imebarikiwa raslimali za kutosha na uongozi bora wa Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Kairuki ametoa rai hiyo kwenye hafla maalum ya kuukaribisha ujumbe wa mabilionea kutoka Marekani wakiongozwa na Mchezaji namba moja duniani na mtu anayetambulika kama “Pele” au “Mohammed Alli” wa Tennisi duniani, John McEnroe na mdogo wake Patrick ambao wamekuja nchini za wenzao zaidi ya 70 kutalii lakini pia kushiriki tukio la kihistoria la kucheza tennis (#TennisInSerengeti) Desemba 5 mwaka huu katikati ya Hifadhi ya Serengeti.
Amesema sekta ya utalii ni miongoni mwa sekta zinazokua kwa kasi hapa nchini na duniani kwa ujumla ambapo amesema programu ya filamu ya "The Royal Tour" iliyochezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, Samia Suluhu Hassan ni miongoni mwa mikakati iliyosaidia kukua kwa utalii hapa nchini.
Akifafanua amesema matokeo chanya ya The Royal Tour ni pamoja ongezeko la watalii kutoka nje ambapo waliongezeka kutoka watalii milioni 1.3 Oktoba 2022 hadi kufikia watalii milioni 1.7 Oktoba 2023.
Amesema Sera ya Utalii ya mwaka 1999 inasisitiza ushirikishwaji madhubuti wa wadau wote kwenye mnyororo wa thamani wa sekta ya utalii ambapo amesema Serikali itaendelea kuzingatia ushirikishwaji huo na amepongeza Kampuni ya Insider Expeditions na Gosheni Safari kwa kushirikiana kuwaleta wageni hao kupitia program ijulikanayo kama EPIC Tour ambapo mwanzoni mwa Novemba mwaka huu iliwaleta watalii mabilionea zaidi ya 150.
Ametaja baadhi ya maeneo yenye fursa ya uwekezaji kwenye mnyororo wa thamani kwenye sekta ya utalii kuwa ni pamoja na makazi, kumbi za mikutano, usafirishaji wa wageni, ujenzi wa mahoteli na utalii wa bahari kwa juapande wa Tanzania bara na Zanzibar.
Pia Kairuki amesema amefafanua kuwa katika kuhakikisha kuwa sekta ya Utalii inaendelea kukua, Serikali imejikita katika kuboresha miundombinu ya Reli ya Kisasa ya SGR ili kuweza kufikia vivutio katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo pia amesema kumekuwa na kuimarishwa na kuongeza huduma za usafiri wa anga na maboresho kwenye miundombinu ya viwanja vya ndege.
Kwa upande wake na kwa niaba ya ujumbe wa wageni hao John McEnroe amesema wanashukuru mapokezi mazuri waliyoyapata kutoka Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii huku akiahidi kuimarisha uhusiano baina yao na Tanzania.
Amesema wameamua pamoja na lengo la kuja kutalii pia kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuutangaza Utalii wa Tanzania duniani kupitia mchezo wa tennis na kunyanyua vipaji vya watoto
Mara baada ya kuwasili jijini Arusha leo wamefanya program maalum ya kuwafundisha na kucheza na vijana mchezo wa tennis.
Hafla hiyo imepambwa na vikundi mbalimbali vya Sanaa kama Wanne Star na Sholo Mwamba na kukonga nyoyo za wageni hao ambao hawakusita kupanda jukwaani.
Imeandaliwa na John Mapepele
No comments: