LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wafanyabishara wadogo Mwanza wahimizwa kuzingatia usafi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga katika masoko na midana mkoani Mwanza, wametakiwa kuzingatia suala la usafi katika maeneo yao ya biashara, hatua itakayosaidia kuepukana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu.

Rai hiyo imetolewa Jumatano Januari 24, 2024 na Afisa Efya, Elimu na Uhamasishaji kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani mwanza, Rose Nyemele wakati akizungumza na wafanyabiashara wadogo katika soko jipya lililopo Mtaa wa Nyanda, Kata ya Nyasaka wilayani Ilemela.

Nyemele amesema uchafuzi wa mazingira katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya biashara unasababisha magonjwa ya mlipuko ambayo yatawafanya washindwe kuendelea na biashara zao.

"Endeleeni kuzingatia taratibu zote zinazotolewa na wataalam wa afya pamoja na matumizi sahihi ya vyoo ili muweze kufanya kazi zenu katika mazingira salama, gharama ya kusafisha mazingira yenu ni kidogo ukilinganisha na gharama mtakazozitumia kwa ajili ya matibabu" amesema Nyemele.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Nyasaka wilayani Ilemela, Abdulrahman Simba amewaomba wafanyabiashara kuweka mpango kazi wa kushirikiana na wakala anaekusanya uchafu ili kuwa na mazingira rafiki na salama katika masoko.

"Lengo letu siyo kufunga minada, tunahitaji watu wafanye kazi zao kwa kuzingatia usafi ili waweze kujikwamua kiuchumi. Afya ni mtaji hivyo zingatieni usafi kwa masilahi mapana ya uchumi wenu" amesema Simba.

Amesema licha ya kuwepo kwa changamoto ya vyoo vya soko hilo kufungwa kutokana na ukosefu wa maji, amewaomba wafanyabiashara kuendelea kutumia choo cha kulipia ambacho kipo katika maeneo ya soko hilo wakati Serikali ya Mtaa ikiendelea kufanya marekebisho.

Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Nyanda wilayani Ilemela, Mponeja Igali amewasihi wafanyabiashara kushirikiana katika usafi ili wazidi kulinda mazingira yao ya kazi huku akiwataka kila mmoja kuwa mlinzi wa mwenzake.

Naye Mwenyekiti wa wafanyabiashara katika masoko na minada mkoani Mwanza, Justine Sagara ametoa ombi kwa Mtendaji na Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyanda kushirikiana na polisi jamii kupanga utaratibu mzuri wa kulinda mazingira kwa baadhi ya wafanyabishara wasiozingatia usafiri.

"Tujitahidi kufanya usafi wa mazingira tunayofanyia kazi ili tuendelee kuyalinda maeneo tuliyopewa na Serikali, msipozingatia usafi katika kipindi hiki cha mlipuko wa kipindupindu, tunaweza kufungiwa kufanya biashara" amesema Moniko.

Naye Annastazia Andrea ambaye ni miongoni mwa wafanyabiashara wa soko jipya amewasihi wenzake kuendelea kuzingatia maelekezo anayopewa na wataalam wa afya ikiwemo kunawa mikono na maji tiririka.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Mwenyekiti wa wajasiriamali katika masoko na minada Mkoa wa Mwanza, Jastine Moniko Sagara akiwahimiza wafanyabiashara kuzingatia usafi katika maeneo ya kazi.
Mratibu wa usalama wa vyakula Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, Francis Dogani akiwaasa wafanyabiashara wa soko jipya kuzingatia usafi hatua itakayosaidia kujikinga na magonjwa ya mlipuko.
Mtendaji wa Mtaa wa Nyanda uliopo Kata ya Nyasaka Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, Mponeja Igali akizungumza na wafanyabiashara wadogo (hawapo pichani) kuhusu umuhumu wa usafi ili waweze kufanya kazi zao katika mazingira salama.
Baadhi ya wafanyabiashara wa soko jipya lilipo Mtaa wa Nyanda, Kata ya Nyasaka Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza wakiwa kwenye kikao.
Wafanyabiashara wakianza kupanga biashara zao baada ya kumaliza kikao na viongozi wa Serikali pamoja na wataalam wa afya.

No comments:

Powered by Blogger.