LIVE STREAM ADS

Header Ads

Baraza la wafanyakazi Jiji la Mwanza lajadili bajeti ya mwaka 2024/25

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Baraza la wafanyakazi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza limejadili mapendekezo ya bajeti ya halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha ujao wa 2024/25 na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuandaa bajeti inayotekelezeka.

Kikao cha kujadili rasimu ya bajeti hiyo kimefanyika Alhamisi Februari 08, 2024 ambapo pia kimejadili utekeleaji wa bajeti inayoelekea ukingoni kwa mwaka wa fedha 2022/23 ambapo wajumbe wa baraza hilo wameipongeza Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa kuendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi kupitia bajeti yake.

Mwenyekiti wa kikao cha baraza hilo ambaye alikuwa Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Peter Lehhet amewahimiza wafanyakazi na watumishi wa halmashauri hiyo kila mmoja kufanya kazi kwa weledi na uadilifu hususani kuongeza ukusanyaji wa mapato hatua itakayosaidia mwajiri pia kutimizia ipasavyo stahiki zao.

Lehhet amesema mwaka 2023/24 Halmashauri ya Jiji la Mwanza iliidhinisha bajeti ya shilingi bilioni 107.2 na mwaka unaofuata wa 2024/25 inaomba kuidhinisha bajeti ya shilingi bilioni 111.9 ambapo imezingatia masuala mbalimbali ikiwemo maslahi ya watumishi.

"Kila mmoja katika nafasi yake, tubanane ili kuongeza ukusanyaji wa mapato huku tukidhibiti mianya ya upotevu wa mapato kwa kuhakikisha tunatumia mashine za POS. Katika Zahanati na Vituo vya Afya, tukafunge CCTV Camera ili kurahisisha mifumo ya ufuatiliaji" amesema Lehhet.

Katibu wa Baraza hilo, Witness Mlero amewahimiza wafanyakazi kuendelea kutimiza ipasavyo wajibu wao huku wakitoa taarifa za kila siku za utendaji kazi kupitia mfumo uliowekwa hatua itakayosaidia kufikia mipango na malengo iliyowekwa baina ya mwajiri na mwajiriwa.

Baadhi ya wajumbe wa baraza hilo akiwemo Mwl. Sholi Maduhu ambaye pia ni Mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Nyamagana na Diana Mashilanga ambaye ni Katibu wa TALGWU Wilaya ya Nyamagana wamesema wafanyakazi anapotimiza wajibu wake ikiwemo kuongeza ukusanyaji mapato ni vyema pia mwajiri naye akatimiza wajibu wake wa kuboresha maslahi yao.

Awali Afisa Kazi Mkoa Mwanza, Goodluck Luginga amehimiza sera ya ushirikishaji wafanyakazi katika eneo la kazi kuzingatiwa hatua itakayosaidia kuboresha utendaji kazi na pia kutatua changamoto za wafanyakazi na hivyo kuboresha zaidi utendaji na mahusiano baina yao na mwajiri.

Baraza hilo limepitisha mapendekezo ya bajeti hiyo na kutoa maoni kwa ajili ya maboresho ambapo yatawasilishwa katika Kamati ya Uchumi na Fedha kwa maboresho zaidi kabla ya bajeti hiyo kuwasilishwa katika kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa ajili ya kujadiliwa na kuidhinishwa.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Peter Lehhet (katikati) akizungumza kwenye kikao hicho. Kulia ni Katibu Baraza la Wafanyakazi Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Witness Malero na kushoto ni Katibu Msaidizi wa Baraza hilo.
Katibu Baraza la Wafanyakazi Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Witness Malero akizungumza wakati wa kikao cha kujadili bajeti ya Halmashauri hiyo kwa mwaka 2024/25.
Katibu Msaidizi wa Baraza la Wafanyakazi Halmashauri ya Jiji la Mwanza akichangia hoja wakati wa kikao cha kujadili bajeti ya halmashauri hiyo kwa mwaka 2024/24.
Mchumi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Akim Albert akitoa ufafanuzi kuhusu mapendekezo ya bajeti ya halmashauri hiyo kwa mwaka 2024/25. 
Mjumbe wa baraza la wafanyakazi Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Mwl. Sholi Maduhu ambaye pia ni Mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Nyamagana akichangia hoja kwenye kikao hicho.
Mjumbe wa baraza la wafanyakazi wa halmashauri ya Jiji la Mwanza, Diana Mashilanga ambaye pia ni Katibu wa TALGWU Wilaya ya Nyamagana akichangia hoja kwenye kikao hicho.
Mjumbe wa baraza la wafanyakazi wa halmashauri ya Jiji la Mwanza, Martine Sawema akichangia hoja kwenye kikao hicho.
Afisa Kazi Mkoa Mwanza, Goodluck Luginga akizungumza kwenye kikao hicho.
Wajumbe wakifuatilia kikao hicho.
Mjumbe wa baraza la wafanyakazi wa halmashauri ya Jiji la Mwanza ambaye pia ni Afisa Utamaduni wa halmashauri hiyo akichangia hoja kwenye kikao hicho.

No comments:

Powered by Blogger.